Header Ads

Vyeti vya Miss Tanzania 2014 vyaanza kuchunguzwa na RITA, ikibidi Polisi kuhusishwa

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA),
imeanza uchunguzi wa vyeti vya Miss Tanzania
2014, Sitti Abbas Mtemvu, baada ya kuibuka utata
wa taarifa za kuwapo vyeti viwili vinavyotofautiana
maelezo.
Uchunguzi wetu umethibitisha kuwapo upekuzi
maalumu wa nyaraka alizowasilisha Sitti katika
ofisi za RITA Temeke ili kubaini kwanza uhalali wa
cheti, kabla ya kutafuta ukweli wa taarifa
zilizowasilishwa chini ya kiapo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo
(Sura ya 108 Toleo la 2002), ni kosa la jinai kutoa
taarifa za uongo kwa Msajili na pia ni kosa la jinai
kughushi, mambo ambayo yakithibitika RITA
watalazimika kulikabidhi suala hilo kwa Jeshi la
Polisi.
Mkurugenzi wa Sheria wa RITA Emmy Hudson,
amesema kuwa mamlaka hiyo inachunguza suala
hilo kwa umakini ili kuhakikisha haki inatendeka
kwa mhusika.

Uchunguzi wa RITA unahusisha pia nyaraka zote
za watoto waliozaliwa Temeke katika miaka ya
1980 hadi 1990 kipindi ambacho Sitti alizaliwa.
Kipindi hicho kulikua tayari na mradi maalumu wa
uandikishaji wa watoto wanaozaliwa hospitalini na
majumbani na hivyo kuwapo kumbukukumbu
zote.
Katika mashindano ya Miss Temeke yaliyofanyika
Jumamosi Agosti 23, 2014, Sitti aliyeibuka
mshindi alidai amezaliwa mwaka 1991 kabla ya
kupata cheti kilichodaiwa kutolewa na RITA
Septemba 9, 2014 kikionyesha kazaliwa nyumbani
Temeke Mei 31, 1991.
Cheti hicho kinaonekana kimetolewa wiki chache
kabla ya kilele cha mashindano ya kumtafuta
mrembo wa Tanzania ambayo tena Sitti huyo
alitangazwa mshindi.
Hata hivyo, kupitia mtandao wa JamiiForums
ulibuliwa ushahidi wa hati ya kusafiria ya Sitti
ikionyesha alizaliwa Mei 31, 1989 na si 1991
kama alivyodai. Hati hiyo namba AB202696
ilitolewa Dar es Salaam, Februari 15, 2007.
Lilipoibuka suala la umri Mratibu wa Miss
Tanzania, Hashim Lundenga alisema: “Acha watu
waseme, ni upepo tu utapita” na baada ya
kuibuka kwa hati ya kusafiria aliita waandishi wa
habari na kuonyesha cheti ambacho kimeibua
mazito zaidi yanayoweza kulifikisha suala hilo
mahakamani.
Uchunguzi wa kiitelijensia umegundua
kuhusishwa kwa vyombo zaidi vya serikali
kutokana kuwapo kwa sheria tofauti zinazogusa
suala hilo na taarifa zinasema, “uchunguzi ni
mzito kuliko tunavyoweza kusema.”
Katika cheti cha kuzaliwa inaonekana kwamba
Sitti ambaye ni binti wa Mbunge wa Temeke,
Abbas Mtemvu alikula kiapo kuomba cheti hicho.
Kusema uongo chini ya kiapo ni kosa la jinai.

Credit: Fikrapevu

No comments

Powered by Blogger.