Chadema wapinga mchakato upigaji kura wa maoni bila Daftari la Kudumu la Wapigakura kuboreshwa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kimesema kitapinga kwa nguvu zote mchakato wa
upigaji kura ya maoni kuamua kuikubali au
kuikataa katiba inayopendekezwa, kuendeshwa
bila Daftari la Kudumu la Wapigakura kuboreshwa
kwanza.
Kadhalika, chama hicho kimelalamikia baadhi ya
kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa kwa
madai kwamba, zina upungufu.
Msimamo huo wa Chadema ulitangazwa na
Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe,
alipokuwa akifungua kikao cha siku mbili cha
Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, jijini Dar es
Salaam jana.
Alisema tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)
imekwisha shauri kwamba uandikishaji wa
wapigakura unatakiwa ufanyike upya kwa kuwa
daftari lililopo hivi sasa halina sifa ya kutumika.
Hata hivyo, alisema mchakato wa Katiba
ulivyoendeshwa kupitia Bunge Maalumu la Katiba
na Rais Jakaya Kikwete alivyobadili kauli kwa
nyakati tofauti kuhusu suala hilo, ni dalili kuwa
serikali imedhamiria kura hiyo iendeshwe bila
daftari hilo kuboreshwa.
Alisema mwaka 1995, Baba wa Taifa, Hayati
Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema kuwa
Watanzania wanahitaji mabadiliko ama kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM) au nje ya chama
hicho.
Hata hivyo, Mbowe alisema namna mchakato wa
Katiba ulivyoendeshwa, imeonyesha kuwa serikali
haina dhamira ya kuleta mabadiliko ambayo
Watanzania wanayataka na hivyo, kushindwa
kumuenzi Mwalimu Nyerere.
Alisema pamoja na mambo mengine, mchakato
huo umeonyesha hila, ukiukwaji wa matakwa ya
wananchi na wizi wa kura.
Kutokana na hali hiyo, alisema mara kwa mara
Chadema imekuwa ikionya kuwa kama kuna watu
watasababisha machafuko nchini, basi
watakaostahili kulaumiwa ni CCM ambao
hawatakwepa kubeba lawama hizo.
Alisema jinsi Rais Kikwete alivyozungumza na
viongozi wa vyama vya siasa sivyo alivyokuja
kuzungumza baadaye kuhusu mchakato wa
katiba.
“Ni dalili kuwa wanaonyesha kuwa wanadhamiria
kufanya kura ya maoni bila kuboresha daftari la
wapigakura. Hatutakubali. Tutapinga mchakato
wowote utakaofanyika bila daftari la wapigakura
kuboreshwa,” alisema Mbowe.
Aliongeza: “Tutafanya kazi na washirika wetu,
wakiwamo kutoka ndani ya Ukawa (Umoja wa
Katiba ya Wananchi) kupinga mambo hayo.”
Alisema hila zinafanywa na serikali kwa kuwa
wanajua kuwa hawana uwezo wa kuwashawishi
vijana kuikubali Katiba inayopendekzwa katika
mchakato wa upigaji kura ya maoni.
Mbowe alisema vyama vya upinzani vimekuwa
vikilalamika kuhusu daftari hilo kutokuboreshwa
na kwamba, walifanya hivyo pia hata wakati wa
uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la
Kalenga, mkoani Iringa.
Alisema CCM ni mdau wa kisiasa kama ilivyo kwa
vyama vingine vya siasa, hivyo haina haki ya
kujipa mamlaka kuviongoza vyama vingine katika
jambo lolote la kisiasa, likiwamo linalohusu
Katiba.
Mpekuzi
Post a Comment