MUNGU WANGU! FEDHA ZA ESCROW ZINGEJENGA VIWANJA VYA TAIFA SITA
GUMZO kubwa kwa sasa nchini ni wizi wa jumla ya shilingi
bilioni 306 zilizoibiwa kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Uchotaji wa fedha kwenye akaunti hiyo, umetikisa nchi
ikiwa ni pamoja na kuwataja vigogo mbalimbali wakiwemo wakubwa serikalini.
Ripoti hiyo imewataja hadi viongozi wa dini kuhusika
katika mgawo wa uchotaji wa mamilioni ya fedha hizo ambazo ni mali ya wananchi.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac) ndiyo
iliyofichua uchotwaji wa fedha hizo na kuweka mambo yote hadharani, moto bado
unaendelea bungeni.
Katika sehemu ya taarifa ya Pac iliyosomwa na
Mwenyekiti, Zitto Kabwe ilieleza namna watu walivyokwenda benki kugawana fedha
hizo wakiwa na mifuko, maboksi na hata magunia.
Waliogawana fedha hizo kwa maboksi na magunia ni wale
waliochota kiasi cha Sh bilioni 77. Hapo ndiyo tunarejea kwenye michezo.
Tanzania ni kati ya nchi yenye matatizo makubwa sana
katika maendeleo ya michezo mbalimbali, acha tuutumie ule wa soka unaopendwa
zaidi.
Kuna upungufu wa mambo mengi sana na hasa miundombinu
ambayo ukosekanaji wake unafanya kuzorota kwa mchezo wa soka na maendeleo
kwenda kwa mwendo wa kobe.
Hakuna vifaa na hasa viwanja, hata Ligi Kuu Bara imekuwa
ikilalamikiwa kwa kuwa viwanja vinavyoweza kuchezewa na wachezaji wakaona wako
kwenye uwanja sahihi ni vitatu tu.
Kimoja kinamilikiwa na serikali, ambacho ni Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam. Kingine ni mali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kambarage,
Shinyanga na kile cha Azam Complex, mali ya Azam FC, kiko Mbagala, Dar.
Ukirejea kwenye viwanja vingine vyote vilivyobaki, yaani
Sokoine-Mbeya, Jamhuri-Morogoro, Mkwakwani-Tanga, Kaitaba-Kagera, vyote ni
matatizo makubwa.
Kwa fedha Sh bilioni 306, Tanzania ingeweza kuwa na
viwanja bora zaidi ya sita. Mfano kama ingeamua kutengeneza viwanja vyenye
uwezo ukubwa kama ule wa Uhuru wa jijini Dar es Salaam, basi ingepata hata
zaidi ya kumi.
Ukisema, serikali ingeamua kujenga viwanja kama vile ya
Uwanja wa Taifa ambacho ni kati ya viwanja bora barani Afrika, basi ingeweza
kujenga viwanja sita. Yaani vitano vya ukubwa kama huo Uwanja wa Taifa na mmoja
kama Uwanja wa Uhuru.
Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam wenye uwezo wa kuingiza
watu hadi 60,000 uliojengwa na kampuni ya Beijing Construction Engineering ya
China kwa kitita cha Sh bilioni 56.4, serikali ya Tanzania ikiwa imetoa Sh
bilioni 25 na Serikali ya China ikatoa kiasi kilichobaki.
Jiulize, nchi yenye viwanja saba kama Uwanja wa Taifa,
kwa kuwa tayari Dar es Salaam kipo kimoja na mmoja mdogo wa kisasa kama ule wa
Uhuru, kweli nchi itashindwa kupiga hatua kimichezo?
Kama fedha hizo zingetumika kujenga viwanja ambavyo
vingekuwa katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga, Shinyanga, Morogoro na Dodoma (mfano). Hamasa ya maendeleo,
ingepanda.
Kawaida hamasa ingekuwa juu, wengi wangependa kushiriki
michezo na hasa watoto na vijana, ingekuwa rahisi timu mbalimbali kutoka nje
kucheza hadi mikoani na kiwango cha soka nchini kingepanda kwa kuwa ushindani
ungekuwa sahihi kwenye viwanja vinavyotakiwa.
Ingesaidia hamasa kwa michezo mingine kama mpira wa
kikapu, ngumi na riadha kwa kuwa kungekuwa na sehemu nzuri ambayo ingetumika
kwa ajili ya kuchezea.
Kwa viwanja kama hivyo, Tanzania ingekuwa ina uwezo wa
kuandaa mashindano makubwa zaidi duniani kama Kombe la Dunia au Kombe la
Mataifa Afrika bila ya hofu hata chembe kama utazungumzia masuala ya viwanja.
Fedha hizo ambazo mjadala wake bado unaendelea,
zingeweza kutumika kwa maendeleo ya michezo au shughuli nyingine za kijamii,
basi zingesaidia kupatikana kwa maendeleo makubwa kuliko ambavyo wachache
wamegawana kwenye maboksi, magunia na mifuko ya sandarusi.
Hii inaonyesha kiasi gani kuna fedha zinatumika ovyo,
ujanja mwingi na huenda huu ndiyo wakati wanasiasa na wafanyabiashara, kuionea
huruma nchi yetu.
Fedha nyingi zinazoibiwa si kwenye Escrow pekee, hata
kwenye kashfa lukuki za wizi zinazojitokeza, bado Tanzania ingeweza kufanya
mambo makubwa ya maendeleo, ingeondokana na utegemezi na kufika mbali
kimaendeleo.
Fedha tunazo kibao, matumizi yake ndiyo tatizo na faida
inakwenda kwa wachache huku watoka jasho wananchi wakiwa wanateseka.
Ingawa bado mjadala unaendelea bungeni na kwingineko,
serikali ikisema si fedha za umma inaonekana haitakwepeka kwamba fedha hizo
zimechotwa na wachache wasiofika hata idadi ya watu 40.
Na Saleh Ally
Post a Comment