Header Ads

"Haturuhusu Wafungwa Kufanya Tendo la Ndoa Gerezani"- Wizara ya Mambo ya Ndani

SERIKALI imesema Tanzania haina sheria ya kuwaruhusu wafungwa kukutana faragha na wenzao wao.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Pereira Ame Silima alikiri kwa Tanzania kutokuwa na sheria hiyo na akajibu kuwa ujauzito ambao huwapata wafungwa wanawake, unatokana
na wafungwa hao kuupata nje ya Magereza.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Maalumu, Rukia Kassim Ahmed (CUF) ambaye alitaka kujua ni kwa namna gani wafungwa wanawake wanapata ujauzito wanapokuwa ndani ya magereza yao.

Pia, alihoji kama magerezani kuna usiri, ni kwa namna gani mahabusi ambao ni mashekhe kutoka Zanzibar wanafanyiwa vitendo vya ulawiti gerezani.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema jeshi la Magereza lina utaratibu wa kutenganisha wafungwa wa kiume na wa kike kwani kila watu hutunzwa kwa sehemu zao na hulindwa na watu wa jinsia zao.

Kuhusu tuhuma za kulawitiwa kwa mashekhe wa Zanzibar, Waziri wa Mambo ya Ndani Mathias Chikawe, alisema sakata la Shekhe Salum Ali Salum linafanyiwa kazi na kwamba kiongozi huyo ameshafanyiwa uchunguzi wa awali katika Hospitali ya Amana.

“Jambo hilo lipo mikononi mwetu, tumempeleka Hospitali ya Amana na kesho (leo) tutampeleka Hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi, lakini tunachunguza pia tabia ya kiongozi huyo na mwenendo wake kabla ya kuingia gerezani,” alisema Chikawe.

Hata hivyo, Chikawe alisema kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwa watuhumiwa hao, kwani tangu mwanzo hakuwa ameripoti vitendo hivyo, lakini alipofika mara ya nne gerezani ndipo akaripoti kufanyiwa vitendo hivyo na mmoja wa polisi.

Hii ni mara ya tatu kwa serikali kutoa majibu hayo, kutokana na maswali ya wabunge ambapo
mara kadhaa swali hilo limekuwa likiulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Salum
Msabaha (Chadema).

Credit; Mpekuzi

No comments

Powered by Blogger.