Header Ads

UBAGUZI WA RANGI WAMTOA CHOZI RONALDINHO



WAKATI mwingine nimekuwa najiuliza mambo maswali mengi sana kuhusiana na suala la ubaguzi wa rangi ambalo linaonekana wakati mwingine kulielemea Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Nianze na mkasa wa juzi ambao umemtokea kiungo nyota wa Brazil, Ronaldinho Gaucho ambaye hivi karibuni amejiunga na klabu ya Querétaro ya nchini Mexico ambako anaamini ndiyo atamalizia mpira wake.
Ronaldinho amebaguliwa, amedharauliwa na kuitwa sokwe, licha ya kwamba hakuwa na kosa hata punde.
Aliyembagua ni mwanasiasa maarufu wa chama kinachojulikana kama National Action Party (Pan) ambaye pia amewahi kuwa waziri wa serikari ya Mexico.
Jamaa anaitwa Carlos Manuel Treviño ambaye ameingia kwenye kundi la wapuuzi na wajinga wanaoamini ubaguzi wa rangi ni nyenzo.




Kisa cha kumbagua Ronaldinho ni kwa kuwa mwanasiasa huyo alikuwa akitokea katika mihangaiko yake anarejea nyumbani, kukawa na foleni kubwa sana njiani na mwisho aligundua inatokana na mashabiki wa klabu ya Queretaro waliokuwa wakitokea kwenye Uwanja wa Corregidora kumpokea kiungo huyo alipokuwa anatambulishwa.
Akaamua kuweka maneno ya kashfa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook akimuita sokwe ambaye amesababisha yeye kuchelewa kufika nyumbani.

Mpira ni burudani kubwa lakini ni chombo bora kabisa cha kuwaunganisha watu mbalimbali wakiwemo wale waliogombana, wasiopendana au kutoelewana.
Nchi nyingi zilizoingia kwenye vita hasa vile vya wenyewe kwa wenyewe, mwisho zimetumia nguvu zaidi kwenye mchezo wa soka ili kurejesha hali ya utulivu.
Mfano mzuri ni Wanyarwanda ambao baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994, soka ndiyo chombo kilichosaidia kwa asilimia kubwa kuwaunganisha, pia kujitahidi kusahau mabaya na makali yaliyopita.

Sasa jiulize, wakati wengine wanatumia soka kama chombo unganishi, vipi hao wanatumia mchezo huo kama chombo tenganishi kwa lengo la kudharau, kuonea au kubeza bila hata sababu yoyote ya msingi.
Ninazungumzia Wazungu, ninazungumzia watu weupe wanaoamini ni bora kuliko Weusi hata kama heshima yao haiko juu kama wanavyofikiri.
Wakati mwingine unaweza kufikiri hata wao Fifa ni wababaishaji kwenye hili kwa kuwa hakuna adhabu kali zaidi kwa wanaofanya hivyo viwanjani.
Kuna kila sababu ya kuliangalia zaidi kwa kuwa wale wanaowabagua weusi, wanakuwa hawana heshima ya kimatendo au hata fedha dhidi yao.
Angalia waliombagua Samuel Eto’o au Yaya Toure kule Urusi. Mfano mwingine wale mashabiki ambao huwabagua wachezaji Waingereza au kule Hispania.
Ajabu hili linafanywa hata na wachezaji kwa wachezaji, nafikiri ndiyo ungekuwa mfano mzuri zaidi kuwaonya wabaguzi wengine.
Ikitokea mchezaji kambagua mwenzake, halafu ushahidi ukawa umepatikana kwa uhakika, basi afungiwe msimu mzima.
Wale mashabiki wanaweza kujifunza kupitia adhabu kali ambazo watapata wachezaji, makocha, viongozi na hata waamuzi ambao wataonyesha ubaguzi.
Nani kasema ngozi nyeupe au ngozi ya mzungu ndiyo akili? Upuuzi mtupu!
Tunajua Fifa ina Wazungu wengi kuliko Weusi, huenda linaonekana si suala kubwa sana na mapambano yake yako kwenye mapango tu bila ya vitendo.
Huenda adhabu ingekuwa kali sana kama Waafrika wangekuwa na nafasi ya kuwabagua Wazungu pia. Fifa bado inahusika na inapaswa kujua upole wake katika hilo, unazidi kufanya liendelee.
Wazungu wanaobagua Weusi ni wapuuzi, Fifa haipaswi kuacha upuuzi huo uendelee kwa kuwa si Weupe tu ndiyo wanaoujua kuucheza mpira na mfano mzuri wa kuwa Weusi wanaujua mpira, jikumbushe kwa Pele.
Wajinga kama mwanasiasa yule wa Mexico aliyembagua Ronaldinho ambaye sasa tayari yuko katika hali mbaya kisiasa kutokana na kusakamwa sana na mashabiki wa soka, wanapaswa wapate joto ya jiwe kama anayokutana nayo, la sivyo hawataacha.
Lakini kwa Fifa na mashirikisho ya soka Ulaya, nayo yapambane kuzuia hilo kwa kuwa inakuwa ajabu, hata Wazungu wenye njaa, nao wanawadharau Waafrika wenye mafanikio zaidi eti kisa ni Weupe. Huu ni upuuzi mkubwa.
 Na Saleh Ally

No comments

Powered by Blogger.