KIVUMBI CHA LIGI KUU TANZANIA BARA NI LEO....YANGA WATAFANYA NINI MORO?
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
PAZIA la ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa
2014/2015 linafunguliwa leo kwa mechi sita kupigwa viwanja mbalimbali nchini.
Macho na masikio ya mashabiki wengi wa soka nchini
yatanarajia kuwa katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro ambapo Mtibwa Sugar
watakuwa nyumbani kuikaribisha Yanga ya Dar es salaam.
Homa ya pambano hilo ni kubwa mjini humo na tayari
majina ya Wabrazil wawili, Genilson Santos Santana ‘Jaja’ na Andrey Coutinho
yamekuwa gumzo huku jezi zao zikiongoza kuuzwa.
Mechi nyingine leo hii ni baina ya mabingwa
watetezi, Azam fc ambao watakuwa uwanja wa nyumbani wa Azam Complex kuchuana na
Polisi Morogoro.
Stand United itakuwa uwanja wa nyumbani wa
Kambarage mjini Shinyinga kuoneshana kazi na wageni wenzao, Ndanda fc kutoka
mkoani Mtwara.
Katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga, wenyeji Mgambo
JKT watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar kutoka mkoani Kagera.
Maafande wa Ruvu Shootings watasaka pointi tatu
muhimu mbele ya Tanzania Prisons ‘Wajelajela’ katika uwanja wa Mabatini,
Mlandizi, mkoani Pwani.
Mechi nyingine kali itapigwa uwanja wa Sokoine
mkoani Mbeya ambapo wenyeji Mbeya City wanaikaribisha JKT Ruvu ya Pwani.
Ligi hiyo itaendelea kwa mechi moja kupigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kwa kuwakutanisha Simba sc dhidi ya Coastal Union.
Post a Comment