Header Ads

MATOKEO VPL: AZAM FC WAENDELEZA MACHINJIO CHAMAZI, SIMBA NGOMA NZITO, MBEYA CITY FC, MTIBWA SUGAR, STAND UNITED ZACHANUA!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
LIGI kuu soka Tanzania bara imeendelea leo kwa mechi tano kupigwa viwanja mbalimbali  nchini.
Wekundu wa Msimbazi, Simba walikuwa wenyeji wa Polisi Morogoro na dakika 90 za mechi hiyo zimemalizika kwa sare ya 1-1.
Bao la Simba lilifungwa na Emmanuel Okwi, wakati la Polisi lilitiwa kimiani na Danny Mrwanda.
 
Kabla ya mechi hiyo kupitia mtandao huu nilisema Simba wana asilimia kubwa  ya kushinda na nikatahadharisha kuwa wasiingie kichwa-kichwa kwasabababu Polisi wanaweza kubadilika kabisa na ndicho kilichotokea.
Nilisema Danny Mrwanda angewafunga Simba kutokana na aina ya uchezaji wake na uzoefu alionao. Kweli kawaadhibu waajiri wake wa zamani.
Mabingwa watetezi wa ligi kuu hiyo, Azam fc wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting ya Mkoani Pwani katika mechi iliyopigwa uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam.
Kabla ya mechi kupitia mtandao huu nilieleza kuwa Azam fc wana asilimia 80 dhidi ya 20 za Ruvu Shooting kushinda mechi ya leo. Uwanja wa Azam Complex umekuwa mgumu kwa timu pinzani.
Azam wamecheza vizuri na mabao mawili ya Didier Kavumbagu yameifanya timu hiyo ipande kileleni.
Kavumbagu sasa amefikisha mabao 4 katika mechi mbili za ligi kuu.  Ndiye anayeongoza katika orodha ya wafungaji.
Mechi nyingine iliwakutanisha Mtibwa Sugar dhidi ya Ndanda fc katika uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.
Mtibwa Sugar walioanza kwa kasi msimu huu kwa kuitandika Yanga 2-0 wikiendi iliyopita, leo wametoa kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya vijana wa Mtwara.
Ndanda walianza kwa kasi wikiendi iliyopita wakiifunga Stand United 4-1, lakini leo wameanza ligi rasmi na kuangukia pua mbele ya wakata miwa.
Huko Tanga, Mgambo JKT wamepoteza mechi yao kwa 1-0 dhidi ya  Stand United kutoka Mtwara.
Mechi hiyo imepigwa uwanja wa CCM Mkwakwani na wikiendi iliyopita, katika uwanja huo, Mgambo walishinda 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Mechi nyingine imepigwa uwanja wa CCM Sokoine Mbeya ambapo wenyeji wa uwanja huo, Mbeya City fc waliwakaribisha Coastal Union ya Tanga.
Dakika 90 za mechi hiyo zimemalizika kwa Mbeya City kuibuka na ushindi wa 1-0. Bao pekee la City limefungwa na beki Deogratius Julius..
Wikiendi iliyopita, Mbeya City fc walitoka 0-0 na JKT Ruvu, wakati Coastal wao walitoka sare ya 2-2 na Simba.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi mbili kupigwa ambapo Yanga itawakaribisha Tanzania Prisons uwanja wa Taifa, Dar es salaam.

Nao Maafande wa JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa Azam Complex.

No comments

Powered by Blogger.