Bawacha Yapanga Kumuona Kikwete kwa Maandamano
Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) limetangaza maandamano kwenda Ikulu kumuomba Rais Jakaya Kikwete asikubali kutia saini Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iwapo itapitishwa na Bunge.
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee alisema jana
kwamba maandamano hayo yatafanyika mwishoni mwa wiki ijayo, baada ya
maandalizi yatakayofanyika kwa siku saba kuanzia jana kukamilika.
Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe, alisema baraza
hilo limeamua kuitisha maandamano hayo ili kuwakilisha kilio cha
wanawake ambao ndiyo waathirika wa kwanza pale nchi inapokuwa katika
mfumo usio wa haki.
Alivitaka vyombo vya dola hasa polisi kujitokeza
kuwasindikiza na kuandamana nao kwa kuwa nao ni miongoni mwa Watanzania
ambao wataathiriwa na uamuzi usiolenga kujenga umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, Polisi imetahadharisha kuwa itaendelea
kuwachukulia hatua za kisheria wanachama wa Chadema watakaojiingiza
katika maandamano yaliyopigwa marufuku nchini.
Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba alisema, “Kauli
yetu haijabadilika, maandamano ya Chadema ni batili. Yeyote
atakayeandamana atakuwa anakiuka utii wa sheria bila shuruti. “Jukumu
letu ni kuwalazimisha wote wasiotaka kufanya hivyo, kuitii kwa shuruti.”
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment