MABINTI PACHA WALIOUNGANA KUHITIMU KIDATO CHA NNE MAKETE
Hatua
ya kwanza ya ndoto ya kuzama katika elimu ya mabinti pacha walioungana
kiwiliwili, Consolata na Maria Mwakikuti (18) wa Kijiji cha Ikonda wilayani
Makete mkoa mpya wa Njombe, inatarajiwa
kutimia Novemba mwaka huu, wakati mabinti hao watakapofanya mtihani wa kuhitimu
kidato cha nne.
Itakumbukwa
kwamba walipokuwa wakimaliza elimu ya msingi mwaka 2009 kijijini kwao Ikonda,
walikuwa na umri wa miaka 13 na katika ndoto zao kwa pamoja walisema wanataka
kuwa wasomi waliobobea katika utaalamu wa kompyuta. Lakini, kwa sasa, wanasema
wanatamani kufanya kazi ya Ukatibu Muhtasi.
Wanafunzi
hao ambao mwaka 2010 walichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana
ya Jangwani, Dar es Salaam.
Kwa
sasa wanasoma katika Shule ya Sekondari ya Maria Consolata iliyopo Kidabaga
wilayani Kilolo
mkoani Iringa.
mkoani Iringa.
Shule
hiyo inamilikiwa na Kituo cha Nyota ya Asubuhi ya Wamisionari Wakatoliki wa
Italia, kinachosaidia kuwatunza watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hii shuleni hapo hivi karibuni, walisema wanafurahi kuwa
miongoni mwa watahiniwa watakaofanya mtihani huo wa kidato cha nne mwaka huu.
"Tunafurahi,
tunajiandaa tunasoma kwa bidii, mtihani uko karibu tunataka tufaulu vizuri
masomo yetu, ili ile ndoto yetu ya kuwa Makatibu Muhtasi itimie," walisema
Maria na Consolata, ambao wanatumia baiskeli maalumu kuwapeleka darasani,
ambako pia wana kiti maalumu.
Pacha
hao wameshangaza watu wengi kwa jinsi walivyo, ambapo kila mmoja ana madaftari
yake. Wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi wanazopewa, mmoja huanza
kuandika, akimaliza na mwingine huandika.
"Wala
hatupati shida tumezoea, kila mmoja anafanya kazi yake, mimi naandika kwa mkono
wa kushoto na Maria anaandika kwa mkono wa kulia," anasema Consolata,
ambaye anaonekana kuwa mchangamfu zaidi.
Shule
hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne. Ilianzishwa mwaka 2006 na
hivi sasa ina jumla ya wanafunzi 183. Wote wanaishi kituoni hapo na wote
wanatoka kwenye mazingira magumu.
Changamoto
kubwa iliyokuwa shuleni hapo ni ukosefu wa nishati ya umeme, ambapo uongozi wa
shule na kituo hicho unalazimika kutumia jenereta na umemejua, jambo ambalo
mapema wiki hii Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA), imewaondolea adha kwa
kuwapelekea umeme.
Pacha
hao walizaliwa mwaka 1996 wakiwa wameungana katika Hospitali ya Ikonda wilayani
Makete mkoani Iringa.
Walifaulu
mtihani wa darasa la saba mwaka 2010, ambapo kila mmoja alipata alama 151,
ingawa walitofautiana ufaulu kwenye masomo
yao.
Katika
somo la Maarifa ya Jamii, Consolata alipata alama 29 na Maria alama 25, kwenye
somo la Kiingereza, Maria alipata alama 36 na kumzidi Consolata aliyepata alama
34, wakati kwenye somo la Sayansi, Maria alimzidi Consolata kwa kupata alama 31
dhidi ya 29.
Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliwapanga pacha hao kujiunga na kidato cha
kwanza katika Shule ya Sekondari Jangwani jijini Dar es Salaam.
Hata
hivyo hawakujiunga na sekondari hiyo, kutokana na hali yao na pia umbali kutoka
Iringa hadi Dar es Salaam. Ndipo Wamisionari hao wakawachukua mwaka 2011 na
kuanza kidato cha kwanza.
Walizaliwa
kwenye Hospitali ya Misheni ya Ikonda mwaka 1996. Lakini, taarifa zao
hazikufahamika hadi pale walipoandikishwa kuanza elimu ya msingi Ikonda na
kutafutiwa mlezi wa kuwaangalia, baada ya wazazi wao kufariki dunia wakiwa bado
wadogo.
Post a Comment