RASIMU YA KATIBA MPYA ILIYOPENDEKEZWA KUWASILISHWA BUNGENI SEPTEMBA 24 MWAKA HUU
Katibu wa Bunge Maalum la Katiba Ndg. Yahya Khamis Hamad akielezea kuhusu mabadiliko ya ratiba ya bunge hilo.
…………………………………………………………………………….
Na Benedict Liwenga na Magreth Kinabo.
RASIMU ya Katiba Mpya iliyopendekezwa inatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba Septemba 24, mwaka huu.
Mabadiliko
hayo yametangazwa jana jioni na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahya
Khamis Hamad wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake.
Aidha
Katibu huyo amesema uamuzi wa mabadiliko hayo, umetokana na kufanyika
kikao baina ya Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo na Mwenyekiti wa Kamati
ya Uandishi.
Hata
hivyo Katibu huyo amesema kuwa kazi ya uandishi wa Rasimu hiyo
imeshakamilika na kazi iliyobakia ni kuipitia kwa makini, hali
iliyosababisha mabadiliko ya uwasilishaji wa Rasimu hiyo katika Bunge
hilo, uliopangwa kufanyika hapo kesho Septemba 22, mwaka huu.
“Uwasilishwaji
wa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa sasa utafanywa siku ya Septemba 24,
mwaka huu, ” alisema Katibu wa Bunge hilo.
“Kamati
ya uongozi imeona kuwa ni busara na kupewa siku mbili kwa ajili ya
kuipitia upya ile kazi ambayo wameifanya ili kufikia tarehe 24 kutoa
kitu makini, napenda niwahakikishie wananchi kuwa kitu kizuri kinakuja.
Aliongeza
kuwa Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, inatarajia kukabidhiwa Rasimu ya
Katiba Mpya iliyopendekezwa tarehe 23 Septemba, mwaka huu kutoka kwa
Kamati ya Uandishi wa Bunge hilo.
Aidha,
Katibu huyo ameeleza sababu ya uairishwaji wa uwasilishwaji wa Rasimu
hiyo Bungeni hapo kutokana na ugumu, umakini na uzito wa kazi yenyewe.
“Tulikuwa
tumepanga hapo tokea awali kufanya kikao na Kamati ya Uongozi asubuhi
tukafanya mchana na hata jioni kila wakati Kamati ya Uandishi ikawa bado
haijamaliza hiyo kazi na tulivyofanya kikao cha Kamati ya Uongozi hii
jioni tukamuita Mwenyekiti wa Kamati ya uandishi akaonyesha kwamba hiyo
kazi walikuwa wakiifanya usiku na mchana na hadi sasa wamesema
wamemaliza kuandika.
“Lakini
kutokana na namna walivyokuwa wakiifanya hiyo kazi kwa uharaka na ingawa
walikuwa wakiifanya kwa umakini lakini wanahitaji muda wa kuanza
kuipitia kwa makini zaidi kuanzia mwanzo mpaka mwisho hivyo wakaomba
wapewe muda wa siku mbili ya kesho na keshokutwa ili kuweza kuipitia
kazi hiyo kwa umakini,”alisema.
Katibu
wa Bunge hilo, aliongeza kwamba mabadiliko hayo hayataweza kuathiri
upigaji kura uliopangwa kufanyika Septemba 29 hadi 2 Oktoba mwaka huu.
“Tumeacha
siku ya Septemba 29, mwaka huu ili iwe siku ya kuanza kupiga kura na
tumalize 2 Oktoba, mwaka huu ili tuhakikishe kwamba Oktoba 4 , mwaka
tumemaliza hili zoezi,” alisisitiza.
Aidha Katibu huyo alifafanua kuwa ratiba kuhusiana na masuala hayo ataitoa leo.
Post a Comment