Bunge la Katiba:Kura kupigwa ughaibuni
Mbunge wa Bunge Maalum la Katiba, Said Arfi,
akichangia hoja ya kurekebisha kanuni za bunge hilo jana ili kutoa
nafasi kwa wajumbe walio nje ya bunge hilo kupiga kura. Picha/ Khalfan
Said.
Hali hiyo ilijitokeza wakati wajumbe waliokuwa wakipinga kufanyika kwa marekebisho hayo alipokuwa akiwaingilia na kuwakatisha na wakati mwingine kuwatuhumu kuwa ni waongo na wanazua kwamba, azimio hilo ni la kulazimisha ili wapige kura.
Alifanya hivyo wakati wajumbe watatu kwa nyakati tofauti walipokuwa wakichangia kuhusu marekebisho ya kanuni za Bunge hilo jana.
Mjumbe wa kwanza kukumbana na hasira na ubabe Mwenyekiti huyo wa Bunge alikuwa Ezekiah
Oluoch, aliyeambiwa kuwa ni muongo.
Wengine ni Said Arfi, ambaye alilazimika kukatisha muda wake baada ya kulumbana na Mwenyekiti alipotamka kuwa haoni sababu ya kuwalazimisha na kuwatafuta watu waje kupiga kura kwa kuwa siyo matakwa ya demokrasia.
Kauli hiyo ilimfanya Mwenyekiti kumkatisha kwa kumtaka Arfi aeleze ni nani anawalazimisha wajumbe hao walio nje ya Bunge kupiga kura.
“Nani anakwambia wanalazimishwa, nani anakwambia wanalazimishwa? Hakuna mtu anayewalazimisha,” alisema.
Kitendo cha Mwenyekiti kuingilia mara kwa mara michango ya wajumbe wanaopinga marekebisho ya kanuni, ilimfanya Arfi kumweleza kuwa wananchi wanaomsikiliza akiwaingilia wajumbe wakati wa michango yao, wanampima.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotuingilia katika michango yetu, Watanzania wanakupima kama unafaa kuliongoza taifa hili,” alisema Arfi.
Hali hiyo ilimfanya Mwenyekiti naye kumweleza Arfi ‘kiutu uzima’ kuwa anaheshimika sana, lakini anachozungumza wakati mwingine siyo sawasawa.
Arfi alisema hakubaliani na azimio hilo kwa sababu kanuni ya 38 ya Bunge hilo ilikuwa tayari imeshaweka utaratibu mzima na hakuna sababu ya kuifanyia marekebisho.
“Jambo hili tunalofanya ni kubwa sana. Kuandika Katiba ya taifa letu ni lazima tuwe na nia zilizokuwa njema ili tuweze kulipatia taifa hili Katiba ambayo itaridhiwa na Watanzania,” alisema.
Alisema haoni sababu zozote za msingi za kutaka wajumbe, ambao hawamo ndani ya Bunge hilo kupewa fursa ya kupiga kura.
“Kwa uzoefu wa mabunge mengi duniani, inapofika wakati wa kupiga kura, hupiga kura wajumbe, ambao wamo ndani ya ukumbi wa Bunge…huu ndiyo utaratibu unaotumika dunia nzima. Sasa hii ya kwenda kuwatafuta watu huko waliko na huna uhakika kwamba, huyu anayepiga kura ndiye yeye, ni shaka tupu, alisema.
Oluoch alituhumu kauli za mkanganyiko, ambazo zilitolewa bungeni kwa nyakati tofauti na mwenyekiti wa Bunge hilo pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, kuhusu utata wa akidi ya wajumbe.
Hali hiyo inasababisha kushindwa kujulikana kwa idadi halisi ya wajumbe wanaopaswa kupiga kura.
“Waziri wa Sheria na Katiba alipotoa taarifa yake wiki iliyopita alilijulisha Bunge hili kuwa waliopo ndani ya Bunge hili wapo 500. Mwenyekiti uliposimama kuelezea tatizo, ambalo hivi sasa umelileta kwetu, ulieleza kwamba, wanaotakiwa kupiga kura ni watu 460. Asubuhi hii uliposimama umetuambia waliopo hapa ni kama watu 480,” alisema Oluoch.
Hata hivyo, Mwenyekiti alimkata kauli kwa kusema kuwa takwimu alizozitoa ni za makadirio, huku akimtuhumu Oluoch kwa kusema uongo.
Oluoch alisema licha ya Mwenyekiti kumwita mwongo, haungi mkono hoja ya kufanya marekebisho ya kanuni kwa sababu anaamini inavunja sheria za nchi na haijawahi kutokea katika mabunge mahali popote duniani kwa mtu kupiga kura akiwa nje ya ukumbi wa Bunge.
Alisema kutunga kanuni inayopingana na sheria mama ya nchi ni uvunjaji wa sheria, ambao hatakubaliana nao hata kama atabaki peke yake katika suala hilo.
“Mwenyekiti, naeleza hili kwa misingi hii kuwa kila raia ana haki ya kupiga kura, katiba yetu inaeleza ilimradi awe na miaka 18. Lakini haki hiyo imewekewa pia utaratibu wa kisheria. Taratibu tulizonazo katika nchi hii, hazijaweka utaratibu wa kwamba mtu, ambaye hayupo kwenye eneo la kupigia kura akaruhusiwa kupiga kura…hatujawa na sheria hiyo mheshimiwa mwenyekiti,” alisema.
Hata hivyo, mwenyekiti aliendelea kumkata kauli Oluoch kwa kumuuliza ni aina gani ya kura anazozungumzia.
“Kura zipi, ambazo wewe unazungumzia? Ebu nionyeshe kifungu…unasema uwongo mtupu…wewe unazungumzia sheria ya uchaguzi. Tunamchagua nani hapa?” alihoji Mwenyekiti wa Bunge hilo.
Oluoch alisema: “Haya Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja na mimi niendelee japokuwa umeniita muongo…” na kuongeza:
“Ninaomba kwamba, kama kanuni zetu zitaruhusu na kuna jambo, ambalo linaleta utata, anaweza akaitwa mtu akalitolea ufafanuzi.”
Alikiomba kiti kumpeleka bungeni Sheikh Mkuu wa Tanzania ili awafafanulie wajumbe wa Bunge hilo kama wajumbe waliokwenda Hijja wanaweza kupata muda wa kupiga kura.
“Mimi siungi mkono jambo hili. Na uamuzi huu wa kuwataka waliokwenda Hijja, ambao hawapo ndani ya Bunge hili kupiga kura. Mimi siliungi mkono,” alisema.
Alisema uamuzi wowote ambao utafanywa na Bunge hilo kwa ajili ya utashi wa kisiasa kwa jambo linalopingana na sheria, atasimama peke yake ndani ya Bunge kulikataa.
Mjumbe wa mwisho kufanyiwa ‘ubabe’ na Mwenyekiti, alikuwa Ally Omar Juma, ambaye alishambuliwa kwa kudai kuwa azimio hilo linalenga kulazimisha wajumbe kupiga kura.
Omar Juma alisema msingi wa maridhiano ndiyo chemchem ya kuanzishwa kwa Katiba mpya.Alisema nguvu yoyote, vitisho au husuda havitasaidia kitu katika katiba hiyo.
“Nashauri busara zako. Mimi nakuamini, sina ugomvi na wewe na nakuheshimu sana…hivyo Mwenyekiti, Katiba hii ni maridhiano ya nchi mbili huru.
Si busara, hasa kwa maslahi ya taifa letu kuharakisha kupiga kura kwa watu, ambao hawapo ndani ya Bunge hili. Ni mvurugano mkubwa wa kisheria, ambao utaleta ufa mkubwa wa kisheria kama ambavyo ufa huo umeshajitokeza ndani ya Bunge hili baina ya sisi tuliomo ndani ya Bunge hili na upande wa Ukawa, ni hasara kwa taifa,” alisema.
Alisema haungi mkono azimio linalotaka kupitishwa la kufanya marekebisho ya kanuni ili kuruhusu wajumbe, ambao wapo nje ya Bunge hilo kupiga kura kwa sababu waliokwenda Hijja hawatakuwa na muda wa kupiga kura.
“Mheshimiwa mwenyekiti, mimi ni muumini wa dini ya Kiislamu. Moja ya nguzo muhimu katika dini ya Kiislamu ni Ibada ya Hijja katika nguzo tatu za Kiislamu…kumpelekea mtu, ambaye yupo Hijja, amekwenda maalumu kwa ajili ya shughuli za ibada, ukiwa katika ibada ile kuna masharti yake…hata kukata kucha unapokuwa pale au kunyoa nywele huruhusiwi,” alisema.
Aliwaomba wajumbe kusitisha suala la kupiga kura ili kutoa fursa pana zaidi ya mashauriano kwa ajili ya wajumbe wote ili wahudhurie katika Bunge hilo.
Kwa upande wa wajumbe, ambao michango yao ilionyesha kuwa wanakubaliana na hoja ya kufanya marekebisho ya kanuni za Bunge hilo ili kutoa fursa kwa watu walio nje ya Bunge kupiga kura, walidai kutokana na wajumbe wenzao kushiriki kwenye mjadala mzima ni busara na haki kuwapatia fursa ya kuhitimisha kazi hiyo kwa wao pia kupiga kura hata kama wako nje ya nchi.
WAJUMBE WAUNGA MKONO
Goodluck Ole Madeye pamoja na kuunga mkono marekebisho ya kanuni hizo, alishauri Bunge hilo kuweka utaratibu wa kuainisha vituo vya kupigia kura ndani na nje.
Alisema hali hiyo itaonyesha uwazi na kuwapa wajumbe uhakika wa kweli kwamba kura hizo zinapigwa toka maeneo hayo.Mwingine kuunga mkono hoja hiyo, ni Pindi Chana, ambaye alidai iwapo wataruhusiwa wajumbe walio nje ya Bunge kupiga kura itakuwa ni moja ya utekelezaji wa haki za binadamu.
“Wajumbe watakaokuwa nje watatekeleza haki yao kwa kupiga kura katika ofisi za balozi zetu,” alisema.Alisema utaratibu wa upigaji wa kura nje ya nchi uliopitishwa na Bunge hilo ni tofauti na ule wa uchaguzi.
Sheikh Thabit Jongo, kwa upande wake, aliunga mkono kwa wajumbe kupiga kura nje ya nchi, lakini akijikita zaidi kwa wajumbe, ambao watakuwa wameenda kuhiji Macca.
Alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuzuka kwa mvutano miongoni mwa wajumbe kuhusu uhalali wa wajumbe hao kupiga kura wakiwa wameenda kuhiji hoja, ambayo awali ilipingwa na mjumbe Ally Omary Juma, ambaye alisema wakiwa kwenye hija waumini wa dini hiyo hawaruhusiwi kufanya kitu chochote nje ya suala la hija.
“Kwa kuwapo Macca na Madina, wajumbe wetu wanaweza kupiga kura, kuna wakati, ambao wanaruhusiwa kufanya hivyo, isipokuwa tarehe 3 Oktoba,” alifafanua.
Wengine waliounga mkono hoja hiyo ni Paul Makonda, Suleiman Jaffu, Sixtus Mapunda, Mohammed Raza, Dk. Khamis Kigwangalla, Lucas Charles Malunde na Constantine Akitanda.
MAREKEBISHO YA KANUNI BUNGE LA KATIBA
Mapema akiwasilisha azimio la Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho, mjumbe wa kamati hiyo, Amon Mpanju, alisema marekebisho hayo yanalenga kumuwezesha mjumbe aliye nje ya maeneo ya Bunge hilo kwa ruhusa ya maandishi ya mwenyekiti kupiga kura.
Alisema ni haki ya kila mjumbe wa Bunge hilo kujadili rasimu ya katiba na hatimaye kupiga kura kwa lengo la kupitisha ibara za sura za rasimu ya katiba zilizoandikwa upya kwenye rasimu ya mwisho ya Katiba.
Mpanju alisema haki hiyo haiondolewi na jambo lolote isipokuwa kama mjumbe mwenyewe amehiari kutoitumia haki hiyo au kifo.
Alisema mchakato wa kufanya marekebisho hayo unazingatia kanuni ya 59 (1) ya kanuni za Bunge hilo, ambayo inatoa mamlaka ya kupeleka mapendekezo ya kuzifanyia marekebisho au mabadiliko kanuni zake katika Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum.
Mpanju alisema mwenyekiti alitumia mamlaka hayo kuwasilisha kwenye kamati mapendekezo ya kuzifanyia mabadiliko kanuni ya 36 na 38.
Alisema kanuni ya 36 (1) inaweka sharti kwamba, sura za rasimu ya katiba zilizoandikwa upya zitapigiwa kura ibara kwa ibara, kwa muda usiozidi siku saba.
Mpanju alisema uzoefu uliopatikana wakati wa kamati za Bunge hilo zilipokuwa zikipiga kura ibara kwa ibara ulidhihirisha kwamba, zoezi hilo linachukua muda mrefu zaidi ya muda uliowekwa na kanuni.
“Hivyo kuna haja ya kurekebisha kanuni ya 36 kwa lengo la kupendekeza utaratibu mwepesi wa kupiga kura utakaokidhi mahitaji ya kanuni.“Marekebisho yanayopendekezwa yataruhusu wajumbe kuzipigia kura ibara zote za sura moja au zaidi.
“Chini ya utaratibu huo, mjumbe anayepiga kura ya wazi, atalazimika kutamka ibara anazozikubali na asizokubali na mjumbe anayepiga kura ya siri, ataonyesha kwenye karatasi ya kupigia kura, ibara anazozikubali na asizozikubali,” alisema.
Alisema utaratibu unaopendekezwa utawawezesha wajumbe wote kupiga kura ndani ya muda ulioainishwa kwenye kanuni ya 36 (1).“Haki hiyo haiondolewi na jambo lolote isipokuwa, kama mjumbe mwenyewe amehiari kutoitumia haki hiyo au kifo,” alisema.
Kuhusu kanuni ya 38 alisema imeweka utaratibu wa kupiga kura utakaotumiwa na wajumbe waliomo ndani ya ukumbi wa mkutano wa Bunge Maalum pekee.
RASIMU YA KATIBA JUMATANO
Hatimaye Kamati ya Uandishi ya Bunge, ambayo ipo chini ya Mwenyekiti wake, Andrew Chenge, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), kesho (Jumatano) inatarajiwa kuwasilisha rasimu ya tatu ya Katiba bungeni na baadaye wabunge kupata muda wa kuipitia.
Mwenyekiti wa Bunge hilo, alisema jana kuwa baada ya kamati hiyo kuwasilisha bungeni rasimu hiyo, wabunge kupitia kwenye kamati zao 12, watapata nafasi ya kuijadili ili kuona kama yaliyomo ni sahihi.
Alisema baada ya hapo kamati hiyo itaandika upya wakijumuisha hoja mbalimbali, ambazo awali zilikuwa zimeachwa au kufanyiwa marekebisho na kwamba, kazi hiyo itafanywa kwa siku mbili, kuanzia Septemba 27 hadi 28, mwaka huu.
Alisema baada ya hapo, wajumbe wataanza kuipigia kura rasimu hiyo, kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 2, mwaka huu.
Imeandikwa na Emmanuel Lengwa, John Ngunge, Jacqueline Massano na Editha Majura, Dodoma.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment