WATOTO WAMWOKOTA BABA YAO AKIWA AMECHINJWA
MFANYABIASHARA aliyefahamika kwa jina la Melasi Lutebula Ndabi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mtaa wa Muhimbili 2, Kata ya Pemba, Wilaya ya Temeke jijini Dar, ameuawa kwa kuchinjwa na watu wanaodaiwa kufika kwake kwa ajili ya kukodi shamba la kulima matikiti.
Mwili wa Melasi Lutebula Ndabi ukiwa umetupwa baada ya kuchinjwa.
Habari zinadai kuwa, marehemu mbali na kuwa mfanyabishara na kiongozi
katika eneo hilo, pia alikuwa akijishughulisha kwa kilimo na ufugaji,
kazi ambazo amekuwa akizifanya tangu afike katika eneo hilo mwaka
2005.Akizungumza kwa uchungu na Uwazi, mke wa marehemu aitwaye Rehema Shaban (pichani), alisema siku za nyuma kuna watu watatu walifika nyumbani hapo wakihitaji kukodi shamba kwa ajili ya kulima matikiti.
Watu hao ambao inadaiwa si wakazi wa eneo hilo na wala hawajulikani walisema wanatokea Kijiji cha Lisu wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora walielekezwa kwa marehemu huyo.
Ilielezwa kuwa, kwa mara ya kwanza watu hao walifika nyumbani kwa marehemu Septemba 5, mwaka
huu baada ya mazungumzo ya kina, marehemu aliwaonesha eneo la ekari tatu.
Mke na watoto wa Lutebula Ndabi wakiwa na uzuni.
Mke huyo alisema hata yeye tukio hilo limemchanganya kwani aliamini
wale vijana walikuwa ni watafutaji na ndiyo maana mumewe aliwapa shamba,
kumbe walikuja kutafuta roho ya mume wake.Alisema tangu watu hao wafike, siku tatu mbele ndipo walipogundua mumewe amechinjwa na vijana hao watatu hawajaonekana tena. Alisema siku ya tukio, mume wake aliondoka na vijana hao kwa madai wanakwenda kumtolea pesa kwenye mtandao wa simu ili wamlipe kwa ajili ya shamba hilo.
Kwa mujibu wa Rehema, watoto wake wawili (mmoja miaka 7, mwingine 4) ndiyo waliogundua mwili wa marehemu baba yao akiwa amechinjwa walipokwenda kuchunga ng’ombe.
Jeneza la marehemu, Lutebula Ndabi.
“Nikiwa bado najiuliza aliko mume wangu, mara mtoto wangu Ashura
(mkubwa) akaja anakimbia huku ana wasiwasi, akasema, mama nimeona shati
la baba, ndala na mguu wake. Ndipo tukaenda huko na watu lakini Ashura
alikataa kufika kwa awamu nyingine.“Tulipofika tuliukuta mwili wa mume wangu. Niliona amekatwa kichwani na pembeni kulikuwa na panga. Baada ya hapo nilihisi mwili ukiishiwa nguvu, sikujua nini kilichoendelea,” alisema mwanamke huyo.
Mpaka sasa Jeshi la Polisi Wilaya ya Temeke linawashikilia watu watatu,
wawili wakiwa ni wale waliowakaribisha wale vijana huku mmoja wao akiwa mwenyeji wa kijiji cha jirani, alikamatwa kutokana na maelezo ya bahasha iliyokutwa kando ya mwili wa marehemu ikisema ‘kumbuka yaliyotokea mwaka 2013’ ambapo baadhi ya watu walisema mtuhumiwa huyo aliwahi kutofautiana na marehemu.
SOURCE: GPL
Post a Comment