Ukawa wazidi kulitesa Bunge
Fahmy Dovutwa
Kiti jana kilitumia nafasi yake kuwashambulia Ukawa huku kikitoa
muda mwingi kwa mjumbe wa Kituo cha Demokrasia (TCD), Fahmy Dovutwa,
kuwashambulia Ukawa ndani ya bunge hilo. Pia nafasi kama hiyo ya
mashambulizi ilitolewa kwa Hamad Rashid kumshambulia Maalim Seif Hamad
hivi majuzi.
Mwenyekiti wa Bunge hilo, akionyesha kuendelea kukerwa na Ukawa
kukaa nje ya bunge, alisema wameendelea kubadilika badilika huku
wakitaka bunge hilo liahirishwe akidai ni kinyume na walivyokubaliana na
Rais Jakaya Kikwete katika mkutano na wajumbe wa Kituo cha demokrasia
Tanzania(TCD).
Akiongea kwa mifano, Mwenyekiti huo wa bunge alisema ndani ya siku
18 tangu kuanza kwa Bunge hilo mwaka huu, wajumbe wa kundi hilo walikuwa
wakionyesha vituko.
“Tulipoanza Bunge la Katiba, kulikuwa na mjadala mkubwa kura za
wazi au za siri, wao walitaka kura za siri, tulipokubali kura zote
zitumike, za wazi na za siri, wao wakapinga za wazi,” alisema kiongozi
huyo.
"Sijui kama wenzangu mnaona kile ninachokiona, baadhi ya viongozi
hawa wa Ukawa wana kipaji cha uigizaji, waigizaji wazuri sana” alisema.
Alisema baada ya muda wajumbe hao walitoa hoja ya kutaka hati ya
Muungano, baadae wakatoa hoja binafsi kwamba Bunge hilo lisiendelee hadi
hati ya Muungano ipelekwe.
“Ilipopelekwa nakala ya hati hiyo kwa wajumbe, walikataa na
kupelekea serikali kuonyesha hati halisi. Baada ya kuonyeshwa hati
halisi ambayo inahifadhiwa kwa uangalifu mkubwa, wenzetu wakasusia Bunge
hadi leo,” alisema.
WATAHADHARISHWA
Aliwataka viongozi wa umoja huo kusubiri uchaguzi mkuu wa mwakani
waone watakavyoanguka kwenye uchaguzi huo na kurudi kwenye kazi yao ya
usanii.
Aidha, alisema katika tukio la hivi karibuni Rais Kikwete
alipokutana na viongozi hao na kufikia makubaliano na baada ya siku moja
kukana maafikiano hayo, ni mwenendo wa uigizaji wanaofanya.
“Mheshimiwa Rais alikutana nao mara mbili kwa muda wa saa saba,
walifikia maafikiano, walipotoka siku moja baadaye walikana yote, hivyo
wananchi waendelee kuwapima…mimi nawashauri tu watakaposhindwa vibaya
uchaguzi mkuu ujao, warudi na kujikita zaidi kwenye fani yao ya
uigizaji” alisema kiongozi huyo.
DOVUTWA ATISHIWA MAISHA
Mjumbe wa Kituo cha Demokrasia (TCD), Fahmy Dovutwa, aliwavaa
viongozi wa Ukawa kwa kuwaita wapotoshaji wa makubaliano kati yao na
Rais.
Kauli ya Dovutwa imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa TCD, John
Cheyo, kuwashutumu viongozi hao kuhusu ukweli wa makubaliano hayo.
Akizungumza wakati wa mjadala wa sura mbalimbali za Rasimu ya
Katiba Mpya, bungeni Dodoma jana, Dovutwa, alisema upotoshaji huo
unafanywa kwa makusudi kwa ajili ya kuleta uchonganishi na kuhatarisha
amani ya nchi.
Alisema katika kikao cha Rais na TCD ambacho yeye alihudhuria,
walikubaliana kuwa mchakato wa kutengeneza Katiba mpya uendelee hadi
Bunge Maalum litakapotoa Katiba inayopendekezwa, tofauti na kauli ya
viongozi wa Ukawa kuwa hakukuwa na makubaliano hayo.
Alisema kikao hicho kilifanyika Septemba 8, mwaka huu, Ikulu ndogo
ya Kilimani, Dodoma na viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa ni wenyeviti
na makatibu wakuu kutoka vyama vya CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, UPDP
na UDP.
“Nashangaa hawa Ukawa walikuwa na nafasi ya kukataa na kumwambia
Rais awape muda warudi ili wajadiliane, lakini hawakufanya hivyo,
walikubali na Rais kumuomba Mwenyekiti wetu (John Cheyo, ) pamoja na
sisi viongozi wenzake tukatangaze kwa wananchi”:
“Kitendo cha kukubali na kisha kujitoa ni hatari na uchonganishi kwa wananchi,” alisema.
Alisema kutokana na jina lake (Dovutwa) kuhusishwa na usaliti,
maisha yake yapo hatarini baada ya kupokea simu tatu zikimtishia maisha.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, jina langu ni sehemu ya walengwa, Katibu wa
CUF, Maalim Seif Hamad ananishutumu eti mimi ni kibaraka wa CCM jambo
ambalo nashangaa, Dovutwa miye na chama changu nawezaje kuhujumu CUF,
Chadema na NCCR-Mageuzi,” aliongeza.
Alisema ndani ya kikao hicho kulizuka mvutano kati ya Rais Kikwete
na Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, baada ya kumtaka Rais kusitisha
Bunge.
“Kilichotokea ndani ya kikao, Lissu alimuomba Rais alivunje Bunge,
lakini Rais alimwambia bwana Lissu wewe ndiye ulisimamia rais asiwepo
kwenye Bunge....kwa sasa hakuna mwenye mamlaka ya kufanya hivyo, Lissu
alishindwa kujibu,” alisema.
Dovutwa alisema ushauri wa Lissu wa kutaka kuvunjwa chombo hicho
hauwezekani kwani kipo kwa mujibu wa sheria, kwani hatua pekee iliyobaki
ambayo Rais anaweza ni kuvunja Bunge la Muungano na kutangaza hali ya
hatari, jambo ambalo ni hatari kwa nchi.
Akizungumzia tuhuma kwamba wamekataa kusaini nyaraka za
makubaliano, Dovutwa alisema wamefanya hivyo kutokana na kupewa nyaraka
hizo na wenzao mlango wa kuingilia Ikulu ili wasipate muda wa kuisoma na
kuelewa vizuri.
LUSINDE
Naye, mjumbe, Livingstone Lusinde maarufu Kibajaji, alipingana na
mapendekezo ya baadhi ya wajumbe wanaotaka sifa ya elimu ya mtu
anayetaka kugombea ubunge kuwa kidato cha nne, na badala yake ibaki
kujua kusoma na kuandika, akisema itawanyima watu wengi haki ya kikatiba
ya kuchagua viongozi na kuchaguliwa.
Lusinde ambaye pia ni Mbunge wa Mtera alisema badala ya suala la
elimu kuwa kigezo kikuu cha mgombea wa ubunge, kiwekwe kipengele cha
uadilifu.
“Nashangaa sana kwani darasa la saba, na kidato cha nne aliyepata
‘divisheni 0’ wanatofauti gani kama sio walitofautiana kwenye majibu tu?
Kinachotakiwa ni uadilifu ndio jambo la msingi, kwani mtu hata akiwa
msomi kama sio muadilifu ni kazi bure,” alisema.
“Suala la nani awe kiongozi tuwaachie wananchi wachague wao ndiyo
wanajua nani anawafaa awe amekwenda shule ama la, na si tuwanyime haki
zao ambazo ni za msingi,” alisisitiza Lusinde.
Alisema elimu kisiwe kigezo kikuu cha kuwanyima haki ya kugombea
wale ambao hawajasoma na kutoa nafasi hizo kwa wasomi kuja na mabegi ya
vyeti ili waweze kuonyesha, wakati kuna watu ambao hawajasoma lakini
wana uwezo mkubwa kuliko maprofesa.
Mjumbe huyo alitaka matajiri ambao wanamiliki mali nyingi na siyo
watawala wafuatiliwe na kueleza mali hizo wamezipataje badala ya
kuwabana madiwani na viongozi wengine pekee.
Imeandikwa na Moshi Lusonzo, Jacqueline Massano na Abdallah Bawazir.
SOURCE:
NIPASHE
Post a Comment