Namshangaa Sitta - Warioba
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Jaji Joseph
Warioba akizungumza na waandishi wa habari.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema anashangazwa na
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kung’ang’ania
kuendelea na Bunge hilo licha ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia lifikie
kikomo Oktoba 4 mwaka huu.
Hivi karibuni, Rais Kikwete alikutana na viongozi
wa vyama vya siasa vilivyo chini ya Kituo cha Demokrasia (TCD) na
kukubaliana kusitisha mchakato wa Katiba hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa
2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu wiki hii
jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba alisema ameshangazwa na uongozi wa
Bunge Maalumu la Katiba kuendelea na vikao wakati uwezekano wa
kukamilisha mchakato haupo.
“Hivi kuna haraka gani ya kuwa na rasimu katika
Bunge hili? Mimi nilivyoelewa makubaliano ya Rais na TCD ni kama
walikuwa wanasema kwa ustaarabu hebu twende polepole. Nimeambiwa kuwa
Rais alitoa muda mpaka Oktoba 4, lakini uongozi wa Bunge ukapanga mpaka
mwisho wa Oktoba,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Mimi nafikiri makubaliano kati ya Rais na
viongozi wa vyama ni kukataa kuongeza muda. Hiyo
kwangu ni lugha ya kistaarabu kwa Bunge kwamba hamwezi kumaliza kazi hii kwa kipindi hiki,” alisema Jaji Warioba.
kwangu ni lugha ya kistaarabu kwa Bunge kwamba hamwezi kumaliza kazi hii kwa kipindi hiki,” alisema Jaji Warioba.
Alimtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,
Sitta kukubali kukosolewa kama yeye anavyokubali kukosolewa kuhusu
Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume yake, badala ya kujihami.
“Nilipoanza wakati ule mengi yalisemwa, lakini
nilijua, ukipewa kazi maalumu lazima upate maoni ya watu ya kila aina.
Kuna wale ambao watakusifu na wengine watakusema vibaya. Nilisemwa mengi
sana. Lakini kwa kuwa nimefanya kazi ya Taifa siwezi kuhangaika na mtu
mmoja mmoja,” alisema na kuongeza:
“Sitta asikilize wale wanaosema kuwa ana kasoro, asije akafikiri kuwa hana kasoro.”
Aliongeza: “Nashangaa sana mambo yanavyoendelea
kwenye Bunge, hata siku hizi siangalii tena. Ni wakati fulani mtu
anaweza kunipigia simu, hebu angalia wanavyosema....”
Alisema hatua ya uongozi wa Bunge kung’ang’ania kuendelea na mchakato ni kupingana na Rais Kikwete.
“Lakini mimi inanishangaza ilikuwaje Rais anatoa
nyongeza ya hadi Oktoba 4, uongozi wa Bunge unaongeza hadi mwisho wa
mwezi? Rais anasema hivi na Bunge linasema hivi. Mimi naomba uongozi wa
Bunge utafakari tena,” alisema na kuongeza:
“Kinachofanywa na uongozi wa Bunge la Katiba hakina shinikizo la CCM , bali ni uamuzi ambao unatokana na matakwa yao.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI
Post a Comment