Header Ads

Watano wafariki katika ajali wakitokea kwenye sherehe

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro,Leonard Paulo



Watu watano wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya gari lililokuwa likitoka kwenye sherehe kusukumwa na gari lingine na kuangukia bondeni katika eneo la Gairo kwenye barabara ya Morogoro inayokwenda Dodoma.
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard Paulo, alisema ajali

hiyo ilitokea Agosti 30, mwaka huu, saa 2:30 usiku katika eneo la Tabu Hoteli.
Alisema gari lenye namba za usajili T 697 AVY aina ya Toyota lililokuwa likiendeshwa na Joash Mrisho (25) likiwa na abiria watano likitokea mjini Gairo kwenda Mtumbatu, baada ya kumaliza sherehe kusukumwa na kuanguka kwenye bonde pembezoni mwa barabara.

Kamanda Paulo alisema gari hilo dogo lilisukumwa baada ya kuzidi mita moja au mbili kulia kwa barabara, huku likiwa linapandisha mlima na gari kubwa lenye namba za usajili T 700 CTG lililokuwa na tela lenye namba T 606 CTC aina ya Leland Daff na kusababisha vifo hivyo pamoja na majeruhi.

Aliwataja waliofariki dunia papo hapo kuwa ni dereva wa gari dogo, Mrisho Matonya Mganule (25), Bure Cyprian (30), ambao ni wakazi wa Tabu Hoteli, Neli Aidan (22), ambaye ni mkazi wa Mtumbatu na Sisemi Lesimila (23), ambaye ni mkazi wa Mtumbatu.

Alimtaja aliyejeruhiwa kuwa ni Mang’utu Chitojo (32), ambaye ni mkazi wa Mtumbatu aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa mkoani Morogoro.

Alisema chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana na kwamba, dereva wa gari kubwa anasakwa na polisi baada ya kukimbia.

Aliwaomba wahusika wa masuala ya usalama barabarani kuhakikisha wanakagua kwa umakini leseni za madereva wa magari makubwa wakizingatia muda wa dereva huyo kazini ili kuepusha ajali, ambazo zinaweza kutokea kutokana na dereva kuendesha gari kubwa bila kuwa na uzoefu.

 
SOURCE: NIPASHE

No comments

Powered by Blogger.