RYAN GIGGS, HUYU NI ZAIDI YA MFANO DUNIANI
Na Saleh Ally
WAKATI Ryan Joseph Giggs anacheza mechi yake ya
kwanza ya Ligi Kuu England mwaka 1990, Wayne Rooney alikuwa na miaka mitano tu,
akiongozwa na wazazi wake.
Mwaka huo Gazeti la Championi lilikuwa halijaanzishwa,
wahariri wake wote akiwemo Saleh Ally walikuwa hawajaanza uandishi hadi sasa
ndiyo gazeti bora la michezo Tanzania!
Giggs amecheza Ligi Kuu England kwa miaka 24,
tena timu moja tu ya Manchester United ambayo alijiunga nayo akiwa kinda akitokea
Manchester City baada ya Alex Ferguson kufanya kazi ya ziada kumshawishi mama
yake.
Asili ya Giggs ni Bara la Afrika katika nchi ya
Sierra Leone, ndiye mchezaji mwenye rekodi lukuki za Ligi Kuu England pia kwa
wanasoka kutoka Uingereza.
Yuko kwenye Muungano wa Uingereza (Great
Britain) kwa kuwa anatokea Wales, nchi ya asili ya mama yake mzazi na ndiye
mchezaji gwiji zaidi sasa tangu kuanzishwa kwa Man United.
Rekodi zake ni kubwa na za juu zaidi kuliko
zile za wachezaji wengine wote wa enzi hizo na sasa ukijumlisha akina Bobby
Charlton, Denis Law hadi kizazi cha kina Steve Bruce na baadaye Eric Cantona.
Kufikia alichokifanya inabidi uwe mtu kweli kwa
kuwa Ligi Kuu England ina ushindani wa juu sana, hivyo si rahisi kufanya
aliyoyafanya yeye kwa kipindi chote hicho na leo ukimtupia uwanjani, pamoja na
kwamba ana miaka 40, kazi utaiona.
Giggs ni mchezaji mwenye vionjo vingi zaidi kwa
maana ya kasi, mvuto wa pasi, chenga kuliko mwingine yeyote aliyewahi kutokea
kwenye Ligi Kuu England.
Kawaida haihesabiwi lakini inaaminika, Giggs
ndiye mchezaji aliyewapita mabeki wengi zaidi kwenye Ligi Kuu England kwa maana
ya kumtoka mmoja, wawili au watatu na kupiga krosi iliyozaa bao au kufunga bao.
Makombe:
Hakuna mchezaji anayefikia rekodi yake ya kutwaa
makombe, amebeba 13 ya Ligi Kuu England, si kitu kidogo. Mbali na hivyo
ameshinda makombe matatu ya FA.
Pia Giggs amebeba makombe ya ligi mawili na
mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Usisahau amekuwa kwenye kikosi cha Manchester
United kilichofanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England, mara
tano.
Nahodha & kocha:
Anaingia kwenye listi ya waliowahi kuwa tegemeo
kwenye kikosi cha Man United, baadaye nahodha halafu kocha. Hii hufanyika kwa
wachezaji wachache sana na hasa katika timu moja.
Giggs amekuwa tegemeo kubwa la Man United
lakini msimu wa 2007-08 alichukua nafasi ya nahodha baada ya Garry Neville
kuondolewa kutokana na kuwa majeruhi.
Hali kama hiyo ni nadra sana kutokea kwa
wachezaji wengi wa soka kwa kuwa ushindani unakuwa uko juu kwa mchezaji kupata
nafasi hizo.
Binafsi:
Tuzo za timu, ndiye anashikilia rekodi ya juu,
lakini bado unaweza kumuingiza kuwa bora na mwenye kiwango cha juu kwa zile
binafsi.
Ana rekodi ya kutwaa mara mbili mfululizo tuzo
ya PFA (wachezaji wa kulipwa) vijana.
Alifanya hivyo mwaka 1992 na 1993 na kuwa
mchezaji wa kwanza kufanikiwa kuibeba tuzo hiyo mara mbili mfululizo. Baada ya
hapo hakushinda tena tuzo hiyo hadi alipokuja kuibeba ya wakubwa mwaka 2009.
Nyavu zake:
Rekodi zake zinaonyesha Giggs ni mtu tofauti na
wachezaji wengine wengi na anayetaka kumpata, lazima afanye kazi ya ziada.
Hadi kufikia msimu wa 2012−13, Giggs
alishikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza na kufunga kwenye kila msimu wa
Ligi Kuu England tangu mwaka 1991.
Msimu pekee aliofeli kufunga ni uliofuatia
yaani uliopita na ndiyo aliostaafu. Hakuna mchezaji amefanya kama yeye.
Lakini usisahau, wakati anastaafu, Giggs
alikuwa amebaki mchezaji pekee aliyekuwa anacheza Ligi Kuu England mpya wakati
aliwahi kucheza ile ya zamani na mfumo wa kizamani. Ndiyo maana alichaguliwa
kwenye timu ya karne ya PFA.
Asisti:
Asisti ni neno la Kiingereza, likiwa na maana
iliyozaa bao au pasi ya mwisho kabla ya mfungaji kumalizia wavuni. Linatoholewa
kuwa asisti, Giggs ndiye anayeongoza kwa kutoa asisti nyingi zaidi kwenye Ligi
Kuu England tangu kuanzishwa kwake.
Giggs ametoa asisti 271 kwa timu yake ya Man
United. Achana na kufunga mabao 114 katika mechi 672, ametengeneza kwa idadi
hiyo ambayo hakuna kiungo mshambuliaji bora kila unayemjua anaifikia.
Sehemu moja:
Amekaa Man United tangu mwaka 1990, hakuna
mchezaji aliyethubutu kufikia muda huo na mtu pekee ambaye anamzidi kwa kufanya
kazi muda mwingi zaidi kwenye kikosi hicho ni Alex Ferguson tu.
Kocha huyo alitua Man United mwaka 1986
akitokea Aberdeen, maana yake anamzidi miaka minne tu. Kwa wachezaji hakuna
anayefikia mziki wake wa kukaa muda mwingi kwenye timu moja, pia Man United.
Walimuacha:
Giggs ameachwa na wachezaji wengi sana na ambao
walimkuta Manchester United.
Aliingia kama kinda, baadaye mkongwe na sasa ni
kocha. Utaona hata kundi la akina David Beckham, Nick Butt, kina Neville ambalo
lilijulikana kama Class of 1992, yeye ndiye mkongwe.
Giggs alikuwa ndiye kaka wa kundi hilo na wengi
wao walimkuta, lakini mwisho wakaondoka na kumuacha. Wapo waliong’ara wengine
wakapewa unahodha, lakini yeye akaendelea kubaki Man United, hadi leo.
Wapo ambao tangu wameondoka Man United
wamecheza zaidi ya timu tano, lakini yeye ameendelea kuichezea timu hiyo kwa
mafanikio makubwa.
Amecheza na wengi:
Ndiye anayeshikilia rekodi ya kukutana na
wachezaji wengi zaidi kwenye sehemu mbili tofauti.
Kwanza akiwa Man United, kwa kuwa ameshindana
namba na wachezaji wengi na pia wengi ameshirikiana nao akiwa klabuni hapo.
Pia kwenye Premier League, Giggs anashikilia
rekodi nyingine ya kukutana na wachezaji wengi zaidi wa timu pinzani wakati
akiwa na Man United.
Ikiwa na maana amekabwa mara nyingi zaidi na
wachezaji wengi zaidi kuliko mchezaji mwingine wa Man United.
MAKOMBE 13 PREMIER LEAGUE:
1992-93, 1993-94, 1995-96, 1996-97, 1998-99,
1999-2000, 2000-01, 2002-03, 2006-07, 2007-08, 2008-09, 2010-11, 2012-13.
145 - Ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi
zaidi za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
632 - Ndiye aliyecheza mechi nyingi zaidi
katika kikosi cha Manchester United kwenye Ligi Kuu England.
794 - Ndiye mchezaji aliyeanza mechi nyingi
zaidi za kikosi cha Manchester United katika michuano yote.
100 - Ndiye mchezaji aliyefunga mabao 100 kwa
mara ya kwanza kwa wachezaji wa Man United.
100 - Kiungo wa pili kuwa na mabao 100 katika
Ligi Kuu England baada ya Matt Le Tissier wa Southampton.
1 - Ni mmoja wa wachezaji wanne tu wa
Manchester United waliofanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, mara
mbili. Wengine ni Paul Scholes, Gary Neville na Wes Brown.
WALIOCHEZA MECHI NYINGI PREMIER LEAGUE:
1. Ryan Giggs 632
2. Frank Lampard 577
3. David James 572
4. Gary Speed 535
5. Gareth Barry 529
6. Emile Heskey 516
7. Jamie Carragher 508
7. Mark Schwarzer 508
9. Phil Neville
505
10. Sol Campbell 503
Post a Comment