MAMA FEZA KESSY AKUTWA NA MAKUBWA, NUSRA AUAWE NA MAJAMBAZI - ARUSHA
Mshiriki wa shindano la Big Brother Africa, Feza Kessy.
WAKATI hofu ya mauaji ya wanawake ikiwa bado imetanda mkoani Arusha, mama mzazi wa mshiriki wa shindano la Big Brother Africa, Feza Kessy ameponea chupuchupu baada ya kuvamiwa na majambazi wawili kisha kuporwa fedha.
Akizungumza
na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka jijini humo, Feza alisema mama
yake aitwaye Rose Kessy alikutwa na masaibu hayo mchana wa saa nane,
Jumatano iliyopita akiwa hatua chache kutoka nyumbani kwake, eneo la
Boma ya Siara, Moshono.
“Watu wawili wakiwa na pikipiki
walimsimamisha akiwa garini anarejea nyumbani, wakamteremsha na kuanza
kumsachi, wakachukua pochi yake ambayo ilikuwa na shilingi laki tatu
ndani. Wakati wanafanya tukio hilo watu walikuwa wanatazama tu bila
kufanya lolote.
“Watu wengine walipita na gari
wakataka kusimama, lakini wakaonyeshwa bastola na kupewa ishara ya
kuendelea na safari. Yaani walikuwa wanafanya wakiwa
hawana wasiwasi utafikiri ni askari vile, hivi hapa ndiyo nimerudi
kutoka polisi,” alisema mshiriki huyo ambaye pia aliwahi kushiriki
shindano la Miss Tanzania miaka ya nyuma.
Alisema wakati wa tukio hilo, mama huyo
anayefanya kazi Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita wa Rwanda
(ICTR) alikuwa ameambatana na mtoto wa msanii
huyo wa Bongo Fleva, aitwaye Jayden mwenye umri wa miaka mitano.Alisema
baada ya majambazi hao kuondoka, Polisi walifika nyumbani kwao kwa
ajili ya uchunguzi zaidi.

Post a Comment