BUZWAGI YATUMIA BILIONI 3.7 KWA AJILI YA UJENZI WA BARABARA KATIKA MJI WA KAHAMA
Imeelezwa
kuwa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi umetumia zaidi ya shilingi bilioni 3.7
kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita tano kwa
kiwango cha lami katika mji wa Kahama mkoani Shinyanga.Hayo
yamesemwa na meneja mahusiano wa kampuni hiyo Bi Dorothy Bikurakule
mbele ya timu ya majaji kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa tuzo ya Rais
ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji ambayo inaendelea na zoezi hilo katika
mkoa huo.Bi
Bikurakule alisema kuwa mara baada ya uongozi wa mgodi huo kufanya
mazungumzo na mkuu wa wilaya pamoja viongozi wa halmashauri, ilikubaliwa
barabara kujengwa katika kiwango cha lami katika mji wa Kahama ili
kuchochea ukuaji wa uchumi wa mji huo.“Barabara
ilikuwa ni moja ya vipaumbele muhimu vilivyowasilishwa katika mkutano
mkuu wa viongozi wa halmashauri na mkuu wa wilaya, hivyo kama mgodi na
viongozi tulikubaliana na kuanza kujenga barabara mara moja” alisema
Akielezea
miradi mingine iliyotekelezwa na mgodi wa Buzwagi Bi Bikurakule
alieleza kuwa ni pamoja na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 234
wanaosoma elimu ya sekondari katika shule mbalimbali zilizopo katika
wilaya hiyo ambapo gharama yake ilikuwa ni shilingi milioni 39.4
Alisema
lengo la ufadhili huo lilikuwa ni kuwawezesha wanafunzi wanaotoka
katika familia zenye kipato cha chini kupata msingi wa elimu bora
itakayopelekea kuwa wataalamu wa sayansi na kufanya kazi katika migodi
ya madini.
Akielezea
mikakati iliyofanywa katika kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na
uwepo wa mgodi huo, Bi Bikurakule alisema kuwa mgodi uliwezesha vijana
kuunda vikundi vidogo vidogo na kuwapatia elimu pamoja na vifaa kwa
ajili ya kufyatua matofali mradi ambao tayari umeanza kutekelezwa.
Aidha,
alisisitiza kuwa mgodi umekuwa ukitoa elimu na kuwezesha wananchi
kuanzisha kampuni kwa ajili ya kutoa huduma katika mgodi huo ingawa
kumekuwepo na changamoto ya kutotoa huduma kwa wakati au chini ya
kiwango kinachohitajiwa na mgodi.
Akielezea
mikakati iliyofanywa na mgodi katika kukabiliana na changamoto hizo Bi.
Bikurakule alisema mgodi uliandaa mkutano wa wasambazaji wa ndani ya
nchi ambapo elimu ya ujasiriliamali, sera na fursa ilitolewa.
Aliongeza
kuwa katika kipindi cha Februari hadi Agosti 2014, wasambazaji wa ndani
wapya 7 walisajiliwa na kusisitiza kuwa lengo ni kufikisha wasambazaji
10 mapema Desemba mwaka huu.
Wakati
huo huo akizungumza na timu ya majaji Mkuu wa Wilaya ya Kahama Bw.
Benson Mpesya alisema kuwa mgodi wa Buzwagi umekuwa chachu kubwa ya
ukuaji wa uchumi wa mji wa Kahama hususani katika kutengeneza fursa
kwa vijana wa kitanzania.
Aliongeza
kuwa awali hali ya usalama haikuwa nzuri mgodini hapo lakini baada ya
mgodi kuanza kuajiri wanavijiji wanaozunguka katika mgodi huo kama
walinzi hali ya usalama mgodi hapo imeimarika
Alisisitiza
kuwa mgodi hutumia shiligi milioni 53 kwa ajili ya kulipa wananchi
wanaolinda mgodi huo na kusisitiza kuwa fursa zinazohitaji wataalamu
zichangamkiwe na vijana ili kuchangia katika maendeleo ya nchi.
SOURCE: Greyson Mwase, Kahama
Post a Comment