Uamuzi mgumu,Rais hataongeza muda Bunge la Katiba
Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania, John Cheyo akizungumza
kwenye mkutano na waandishi wa habari, alipokuwa akitoa tamko kuhusu
mchakato wa Katiba na Uchaguzi Mkuu wa 2015, mjini Dodoma jana.
Dodoma. Makubaliano baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kutaka Bunge Maalumu lifikie ukomo Oktoba 4, mwaka huu yamezua sintofahamu mjini hapa huku uamuzi huo ukionekana kuwachanganya viongozi wa Bunge hilo.
Kutwa nzima ya jana, viongozi wa Bunge Maalumu
walishinda kwenye vikao vya mashauriano huku wabunge wa CCM wakitarajiwa
kukutana jana usiku kwenye makao makuu ya chama hicho kupewa taarifa
rasmi za uamuzi huo.
Katika makubaliano baina ya TCD na Rais Kikwete, imeamuliwa kuwa uamuzi wa Rais kupitia Tangazo la Serikali (GN) 254 la kuongeza siku 60 hadi Oktoba 4 uheshimiwe na baada ya tarehe hiyo Bunge liahirishwe.
Uamuzi huo ni kinyume cha azimio la Bunge Maalumu
la Agosti 5, 2014 ambalo lilirekebisha Kanuni ya 14 (4) na kuifuta
Jumamosi katika siku zilizotajwa kuwa za kazi, pia sikukuu na siku za
Jumapili.
Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alikaririwa
akiwaambia wajumbe wa Bunge hilo kwamba Rais alikuwa ameridhia kwamba
siku 60 alizotoa hazingejumuisha Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu.
Ni kwa msingi huo, Bunge hilo likapanga kwamba
lingeendelea na shughuli zake hadi Oktoba 31, wakati Mwenyekiti wa Bunge
atakapokabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais Kikwete.
Hata hivyo, makubaliano yaliyofikiwa baina ya
viongozi wa TCD na Rais yanaonekana kuvuruga kabisa ratiba ya Bunge hilo
ambalo jana na juzi, Kamati ya Uongozi ilikutana mara kadhaa kuona
jinsi ya kunusuru mchakato huo.
Ingawa haikufahamika mara moja kama vikao hivyo
vya kamati ya uongozi inayoongozwa na Sitta mwenyewe vinajadili nini,
lakini taarifa zimedai huenda kukawa na mabadiliko makubwa ya ratiba.
Habari nyingine zinadai kwamba mabadiliko hayo
huenda yakapunguza muda wa baadhi ya shughuli za kazi za Bunge hilo ili
liweze kukamilisha kazi yake ikiwamo wajumbe kupiga kura ya uamuzi.
Katika kikao cha jana asubuhi, kamati hiyo
ilishindwa kurekebisha ratiba yake ili iendane na siku zilizosalia,
hivyo kuahirishwa kwa kuwapa kazi wataalamu wake kuleta mapendekezo
ambayo yangejadiliwa jana mchana.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad
alithibitisha jana kwamba ratiba ya Bunge imebadilika kutokana na hoja
nyingi kukubalika ndani ya kamati.
“Kamati ya uongozi itakutana baadaye (jana)
kuangalia vipengele ambavyo hawakukubaliana kwenye kamati ndivyo
wavipangie muda na ratiba itajulikana baada ya kikao hicho,” alisema
Hamad.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI
Post a Comment