Header Ads

Mbowe tena Chadema, achaguliwa kwa kishindo kuongoza chama hicho

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbowe alisema: “Sikuwa na nia ya kugombea lakini wazee waliponiomba niliamua kukubali. Lakini hii kazi ni ngumu, chama hiki kimefika hatua ya juu na uenyekiti wa Chadema ya leo ni ‘risk’ (jambo la hatari) ya kifo.


Freeman Mbowe amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Chadema katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika jana.
Katika uchaguzi huo, Mbowe alipata kura 789 sawa na asilimia 97.3 na kumshinda mpinzani wake ambaye hakuwa na nguvu kubwa, Gambaranyera Mongateo aliyeambulia kura 20 sawa na asilimia 2.5
Hiki ni kipindi cha tatu kwa Mbowe kupewa ridhaa ya kuongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini. Katika kinyang’anyiro hicho, wagombea walikuwa watano, wawili walienguliwa na mmoja, Kansa Mbarouk alijitoa.
Baada ya matokeo hayo kutangazwa ukumbi ulilipuka kwa furaha ukihanikizwa na wimbo wa “Happy Birthday to you.” Jana pia ilikuwa siku ya kuzaliwa kwa Mbowe akiwa amefikisha miaka
53.
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Bara), Profesa Abdallah Safari aliibuka mshindi kwa kupata kura 775 sawa na asilimia 95 baada ya kubaki mgombea pekee kwani mpinzani wake, Fred Mpendazoe alijitoa. Kura za hapana zilikuwa 34 sawa na asilimia 2.3. Jumla ya wapiga kura walikuwa 811.
Kabla ya uchaguzi huo, nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Said Arfi ambaye alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo.
Upande wa Zanzibar, Said Issa Mohamed alitetea nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti kwa kupata kura 645 sawa na asilimia 79.6 dhidi ya Hamad Yusuf aliyepata kura 164 sawa na asilimia 20.2. Waliopiga kura ni 810.
Wakati wa maswali, alipotakiwa kutaja falsafa na itikadi ya Chadema, Mongateo , alijibu kwa mkato akisema “falsafa ipo katika katiba zetu”, jibu lililowafanya wajumbe kulipuka vicheko.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbowe alisema: “Sikuwa na nia ya kugombea lakini wazee waliponiomba niliamua kukubali. Lakini hii kazi ni ngumu, chama hiki kimefika hatua ya juu na uenyekiti wa Chadema ya leo ni ‘risk’ (jambo la hatari) ya kifo.
“Uchaguzi ni uchaguzi, kila mmoja aingizwe katika uchaguzi... Kura mtakazonipa zitanifunza, kuliko kupata kura asilimia 95 za hila ni bora nipewe asilimia 53 au ziro kabisa ili nikapumzike.”
SOURCE: MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.