Mbowe kutinga polisi na mawakili
Dar/Dodoma. Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe leo atasindikizwa na mawakili watano
atakaporipoti Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam alikoitwa
kuhojiwa kuhusu kauli yake ya kuitisha maandamano nchi nzima kushinikiza
kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Mawakili hao wataongozwa na Makamu Mwenyekiti
wake, Profesa Abdallah Safari, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu,
Halima Mdee, Mabere Marando na Peter Kibatala, huku makada wa chama
hicho wakialikwa kuandamana naye kumsindikiza.
Mbowe alitoa kauli hiyo katika Mkutano Mkuu wa
chama hicho Septemba 14, mwaka huu, akisema maandamano hayo yatafanyika
katika siku ambayo itapangwa katika mikoa yote.
Siku moja baadaye, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Kamishna Paulo Chagonja alimkemea akisema iwapo atafanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa. Pia, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) alimwandikia barua akimwita kuhojiwa.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema
jana kwamba uamuzi huo ni moja ya maazimio matatu ya kikao cha kwanza
cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho iliyokutana Dar es Salaam juzi.
“Mbowe ameitwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi
kesho (leo). Polisi wameandika barua ya wito huo lakini hawajasema kosa
lake ni nini. Itakuwa saa tano asubuhi na atakwenda na mawakili wote wa
chama,” alisema Dk Slaa mbele ya viongozi wote wa sekretarieti mpya ya
chama hicho.
Akizungumzia wito huo jana, DCI Mngulu alisema
ingawa leo atakuwa Songea, ofisi yake ina watumishi wengi na kwamba
ameshawasiliana naye kwa ujumbe kumfahamisha hilo.
Katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema
(Bara), John Mnyika alisema, “Tunawaomba wanachama wa Chadema kujitokeza
Makao Makuu ya Polisi ili kumsindikiza mwenyekiti atakayekuwa
akihojiwa.”
Kwa upande wake, Lissu alisema katika barua ya
wito, polisi wametaja vifungu vya sheria, lakini hawakueleza kosa la
Mbowe ni nini, jambo ambalo linaonyesha jinsi wanavyofanya kazi nyuma ya
kivuli cha chama tawala, CCM.
Akizungumzia madai hayo, Mngulu alisema Kifungu
cha 10 cha Sheria ya Makosa ya Jinai kinajieleza wazi. Kifungu hicho
kinazungumzia kudhamiria kutenda kosa.
Maandamano
Akizungumzia maandamano hayo, Dk Slaa alisema
tarehe rasmi itatajwa baada ya viongozi wa Ukawa kukutana... “Maandamano
yatafanyika nchi nzima, tayari taratibu zimeanza kufanywa mikoani.
Tutaeleza tarehe hiyo. Tumepinga kwa maneno tukitaka Bunge lisitishwe
lakini wenzetu wameweka pamba masikioni. Sasa tunaonyesha chuki na
hasira, polisi watambue kuwa wao wapo 35,000 na wananchi wapo milioni
45.
SOURCE: Mwananchi
SOURCE: Mwananchi
Post a Comment