Header Ads

FAHAMU: Kisukari kinavyosababisha upofu wa kudumu tiba isipofanywa mapema


Lawrence Mashati (si jina lake halisi), anahudhuria kliniki ya ugonjwa wa kisukari katika moja ya hospitali binafsi jijini. Ugonjwa ambao unamsumbua kwa miaka kadhaa sasa.
Amepata matibabu kulingana na maelekezo ya madaktari na wauguzi katika kliniki hiyo. Hata hivyo, katika hali ambayo anaona si ya kawaida, uwezo wake wa kuona unapungua.
Tofauti na miezi kadhaa nyuma, hivi sasa hata kuweka vocha katika simu yake hawezi tena. Sasa inabidi amuombe mtu mwingine amsaidie.
Mbaya zaidi hata ukubwa wa maandishi anayotumia katika kompyuta yake anayofanyia kazi
ameyarekebisha na sasa ni makubwa zaidi tofauti na awali. Hajui tatizo hilo linatokana na nini.
Mashati ni mmoja kati ya watu milioni 346 ulimwenguni wanaougua ugonjwa wa kisukari ambao ni sawa na asilimia 6.4 ya watu wote. Kati ya hao, asilimia 80 wanatoka katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa miongoni mwake.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inabainisha kuwa hapa nchini, kati ya watu 10, watatu wana kisukari na ugonjwa huo umesababisha upofu kwa asilimia 4.8 ya wagonjwa wote nchini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (Muhas) na daktari bingwa wa magonjwa ya macho katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk John Kisimbi anasema upofu unaotokana na kisukari ni tatizo linalozidi kukua.
Anasema wagonjwa wengi wa kisukari wapo katika hatari ya kupata upofu wa kudumu kutokana na kushindwa kuhudhuria kliniki ya macho kujua athari za kisukari katika mfumo wa kuona.
Kisukari ni nini?
Anasema sukari inahitajika kwa ajili ya ustawi wa mwili wa binadamu na kwa kawaida, mfumo ndiyo ambao unaruhusu kuwapo kwa kiwango kinachohitajika mwilini.
Anasema ugonjwa wa kisukari unatokana na hitilafu katika mfumo mzima wa kudhibiti kiwango cha sukari mwilini.
Daktari huyo anasema katika mwili wa binadamu, sukari inahitajika kwani baada ya kuchomwa mwilini ndipo hutoka nguvu ambayo kufanya kazi mbalimbali sanjari na kupumua. Anasema chakula anachokula binadamu kwa kawaida hufyonzwa katika utumbo na kiasi cha sukari kinachohitajika hubaki mwilini baada ya kukutana na vimeng’enyo au kwa jina jingine insulini, kutoka katika kongosho.
SOURCE: MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.