CUF wasababisha sokomoko Tanga
Naibu Katibu Mkuu CUF Taifa, Magdalena Sakaya
Madiwani wa Chama cha Wananchi (CUF) wakiwa na wafuasi wa chama hicho jana walivamia ukumbi wa Ofisi za Mipango Miji katika Halmashauri ya Jiji la Tanga na kuvuruga kikao cha Kamati ya Fedha na Uongozi kilichokuwa kikiongozwa na Meya wa Jiji hilo, Omar Guled.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 4.00 asubuhi katika eneo la Mipango Miji, baada ya madiwani hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe, ambaye ni Diwani wa Kata ya Mwanzange, kuvamia ukumbi huo, huku wakidai kuwa kikao hicho ni batili.
Walikipinga kikao hicho kwa madai hawakubaliani na uwapo wa aliyekuwa Diwani wa CUF Kata ya
Marungu, Mohamed Mambeya, ambaye hivi karibuni alihamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wafuasi hao wa CUF waliingia katika ukumbi huo na kutawanya meza na viti na wajumbe kukimbia, wakiwamo wataalamu wa Halmashauri ya Jiji la Tanga waliokuwapo ndani ya kikao hicho pamoja na Mbunge wa Tanga Mjini, Omar Nundu.
Vurugu hizo zilizodumu kwa takriban dakika 15 kabla ya wafuasi hao wa CUF kuondoka eneo la tukio na kuelekea Majani Mapana kwenye Barabara Kuu ya Segera-Tanga kwa ajili ya kumpokea Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, Magdalena Sakaya, aliyekuwa njiani kwenda jijini humo.
Dakika 20 baadaye, askari wa Jeshi la Polisi walifika eneo la tukio katika ukumbi huo wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Tanga, Omar Ntungu, na kukuta wafuasi hao wa CUF wakiwa wameondoka. Askari hao walilizingira eneo hilo kuimarisha ulinzi.
Hata hivyo, dakika 15 baadaye, wafuasi hao wa CUF walirudi kwenye eneo hilo kwa maandamano, huku wakipiga mayowe kuwa wapo tayari kuuawa na kwamba, watahakikisha kikao hicho hakiendelei kwa sababu kinaendeshwa kinyume cha sheria.
Wafuasi hao wa CUF walikuwa wakitembea kwa miguu, kwa kutumia magari, pikipiki, wakiongoza msafara wa naibu katibu mkuu wao katika Barabara ya Chuda.
Hali hiyo ilizua tafrani kubwa baada ya askari polisi waliokuwa wameuzingira ukumbi huo, kulazimika kuwatawanya wafuasi hao wa CUF kwa mabomu ya machozi.
Hali hiyo ilizua vurumai kubwa na baadhi ya viongozi wa CUF, akiwamo Jumbe walivamia tena ndani ya ukumbi huo na kuwatawanya waliokuwa ndani ya kikao hicho.
Baadhi ya samani, vikiwamo viti na meza vilivyokuwamo kwenye ukumbi huo, vilivunjika.
Baada ya wafuasi hao kufanikiwa kupenya na kuwatawanya wajumbe wa kikao hicho mara ya pili, askari polisi waliendelea kupambana nao kwa kuwaondoa.
Akizungumza katika mahojiano na NIPASHE, Jumbe alisema Mambeya hana uhalali wa kuhudhuria kikao cha kamati ya fedha na uongozi ya halmashauri, kwani alishapoteza sifa mara tu alipohamia CCM.
Akizungumza na NIPASHE, Mambeya alisema alihudhuria kikao hicho kihalali baada ya kupata mwaliko kutoka kwa Mkurugenzi wa Jiji hilo, Juliana Mallange.
Meya wa Jiji hilo, Guled, alisema madiwani hao wa CUF wamevunja kanuni za halmashauri na kwamba, kamati ya maadili ya Baraza la Madiwani wa Jiji hilo itawachukulia hatua.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment