Mambo manne magumu Bunge Maalumu la Katiba
Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba limebaini mambo manne magumu ambayo yameonekana kuzua mivutano isiyo na mwafaka katika vikao vya kamati zake.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta
ameyataja mambo hayo kuwa ni mahakama ya kadhi, uraia pacha, muundo wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano na kamati ya pamoja ya fedha ya muungano.
Sitta alisema taarifa kutoka kwa wenyeviti wa
kamati za Bunge hilo zinathibitisha kuwapo kwa mijadala mikali na
mivutano, jambo ambalo limeisukuma Kamati ya Uongozi kuunda kamati
maalumu ya watu 10 kuyafanyia kazi mambo hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini
hapa jana, Sitta alisema kamati hiyo ndogo itaongozwa na Makamu wake,
Samia Suluhu Hassan.
“Kamati hii italeta mapendekezo ambayo
yatahitimisha masuala yenye utata kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho wa
kupiga kura,” alisema Sitta.
Alisema Muundo wa Bunge umeingizwa katika mambo
hayo kwa sababu kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, mambo yanayohusu muungano yamepunguzwa kutoka 22 hadi saba.
“Kwa hiyo wakikuta kuwa sura ina mambo hayo wanaahirisha mjadala na kusonga mbele ili wapate ufafanuzi,” alisema Sitta.
Alisema ameagiza ufanyike utaratibu wa kuwaita
wataalamu wa juu wa fedha wakiwamo makatibu wakuu kutoka Serikali ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Gavana wa Benki
Kuu (BoT), kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwao...
“Wanakuja hapa Jumamosi, kuzungumza na hizi kamati (za Bunge).”
Kuhusu uraia pacha, Sitta alisema suala hilo lina
matatizo kutokana utekelezaji wake katika nchi mbalimbali. Alisema
wamewaita wataalamu kutoka Idara ya Uhamiaji na Profesa Boniventure
Rutinwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa somo kuhusu
suala hilo la uraia pacha.
Alisema pia Bunge limewaalika wataalamu wa sheria
akiwamo Profesa Issa Shivji ambao watatoa ushauri wa kitaalamu kuhusu
aina ya muundo wa Bunge unaofaa.
Muundo wa Bunge ni moja ya mambo yaliyozua mvutano
kwenye kamati kiasi cha kuwagawa wajumbe na tayari baadhi yao wameamua
kwamba wataandika maoni ya wachache baada ya kutokubaliana na wenzao.
Katika Kamati Namba Tano, wajumbe waligawanyika na
wale wanaotoka upande wa Zanzibar wakitaka muundo wa sasa uendelee,
hoja inayopingwa na wajumbe wa Bara wanaotaka muundo ubadilishwe na kuwa
na Bunge moja lenye sehemu tatu.
Post a Comment