Rasimu ya Warioba sasa mifupa mitupu
Dodoma. Kamati za Bunge Maalumu, zimekamilisha kazi ya kujadili na kuchambua Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku ikiwa imefanyiwa mabadiliko makubwa tofauti na ilivyokuwa awali.
Wajumbe wanatarajiwa kuanza kukutana kama Bunge
zima kuanzia Jumanne ijayo, Septemba 2, 2014 wakati kamati zitakaposoma
taarifa zake baada ya kufanya uchambuzi wa sura 15 za Rasimu ya Katiba
kwa zaidi ya wiki tatu, huku yakitarajiwa mabadiliko makubwa.
kwa zaidi ya wiki tatu, huku yakitarajiwa mabadiliko makubwa.
Mabadiliko yaliyofanywa yameondoa mambo makubwa
yaliyokuwa yakiifanya rasimu hiyo kuonekana mpya, hivyo sasa baadhi ya
wachambuzi wa mambo wanaiona rasimu kama ‘Katiba ya 1977 iliyofanyiwa
marekebisho.’
Mwelekeo wa kubadili karibu misingi yote muhimu
iliyojengwa na tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba akiwa
mwenyekiti, ilianza baada ya kuwekwa kando kwa mfumo wa muungano wa
Serikali tatu uliopendekezwa na badala yake kurejea katika muundo wa
sasa wa serikali mbili.
Uamuzi huo uliathiri mtiririko na muundo mzima wa
sura na ibara za rasimu hiyo, kwani sasa wajumbe wa Bunge Maalumu
walilazimika kutengeneza Katiba yenye mwelekeo wa serikali mbili na siyo
tatu tena zilizokuwa zimependekezwa na tume.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad
aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba mwelekeo wa uchambuzi wa rasimu kwa
sura hizo 15, lazima ufuate kile ambacho kamati zilikiamua katika
uchambuzi wa awali wa sura ya kwanza na ya sita.
Miongoni mwa mambo ambayo yameachwa baada ya
kurejesha mfumo wa serikali mbili ni muundo wa uongozi wa juu wa nchi
hususan nafasi ya Makamu wa Rais, muundo wa Bunge la Jamhuri, kupunguzwa
mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge na ukomo wa
ubunge.
Kadhalika, habari kutoka ndani ya kamati zilisema
suala la kuwekwa kwa maadili ya uongozi kwenye Katiba nalo lilizua
mjadala mkali kutokana na baadhi ya wajumbe kutaka liondolewe kwa
maelezo kwamba linapaswa litajwe kwenye sheria na siyo Katiba.
Mambo ya muungano
Miongoni mwa mambo ambayo kuna kila dalili kwamba
yatabadilika ni Bunge Maalumu kuongeza mambo ya muungano kutoka saba
yaliyopendekezwa na tume na huenda idadi yake ikazidi 22 yaliyomo kwenye
Katiba ya sasa.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa katika baadhi
ya kamati za Bunge hilo na kuthibitishwa na baadhi ya wenyeviti wake,
umebaini kuwa yapo mapendekezo ya mambo ya muungano kuongezwa, tofauti
na mtazamo wa awali kwamba yangepungua kama moja ya njia za kuondoa kero
za muungano.
Tume ya Jaji Warioba ilipendekeza mambo saba tu
kwenye orodha ya muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu, mfumo ambao
hata hivyo ni dhahiri umeshawekwa kando na Bunge Maalumu na kurejesha
muundo wa serikali mbili.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI
Post a Comment