Mh. Sitta avitaka Vyombo vya Habari kuandika habari bila kupotosha Umma
MWENYEKITI
wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta (pichani juu) amevitaka
vyombo vya habari nchini kuacha uchochezi na chuki wakati
vinapohabarisha umma kuhusiana na mchakato wa Katiba Mpya.
Kauli
hiyo nimetolewa leo na Mhe. Sitta wakati alipokutana na baadhi ya
waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma huku akiviasa
vyombo vya habari kuachana na kuandika habari zenye kuleta uchochezi na chuki ili kuvuruga mchakato wa Katiba Mpya.
Mhe. Sitta amesema kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa na dhana tofauti kuhusu kazi ifanywayo na Bunge Maalum la Katiba, hivyo ni vema kuepukana nao na kuhabarisha umma taarifa sahihi ili Katiba Mpya iweze kupatikana.
”Kusema
tunafanya kazi ya Tume ni upotoshaji mkubwa, sisi tunafanya kazi
tuliyotumwa tena kwa uadilifu mkubwa.upotoshwaji mwingine unafanywa
na baadhi ya watu ambao hawalitakii mema Taifa letu na hawapendi kuona
mchakato wa Bunge la Katiba unaendelea vizuri,” alisema Mhe. Sitta.
Mhe.
Sitta ameongeza kwa kutolea ufafanuzi juu ya baadhi ya makundi
yaliyowasilisha mapendekezo yao katika Bunge hilo, kwa kusema kuwa maoni
yanayoletwa na makundi mbalimbali kwa lengo la kuboresha Rasimu Mpya ya
Katiba yanapokelewa lakini sio maoni tu ya mtu binafsi au mwananchi,
bali wanapokea maoni kupitia makundi maalum kama yalivyo kwa wafugaji,
Wasanii na Wakulima ambao wameshawahi kuwasilisha maoni na mapendekezo
yao katika iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba lakini hayakuonekana na mengine yalisahaulika katika Rasimu hiyo.
“Tuna haki na wajibu wa kuyapokea makundi haya ili kutoa Katiba iliyo rafiki kwa wananchi wote,” alisisitiza Mhe. Sitta.
Wakati
huohuo, baadhi ya Wenyeviti wa Kamati mbalimbali za Bunge hilo,
wamesema wamemaliza kazi ya kuchambua Rasimu hiyo vizuri katika Kamati
zao.
Akizungumzia kuhusu kazi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu ya Bunge hilo, Dkt. Francis Michael amesema suala la ardhi lilionekana kuwa nyeti katika Kamati yake.
Dkt. Francis aliongeza kuwa suala la kupokea mapendekezo kutoka kwa makundi mbalimbali si kwamba kila kitu kitawekwa kwenye Katiba Mpya bali ni yale mambo ya msingi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja ya Bunge hilo, Mhe. Ummy Mwalimu
Ally na Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba Kumi na Moja, Mhe. Hamad
Massauni walisema kuwa katika Kamati zao majadiliano yalikwenda vizuri.
Post a Comment