Mgawanyo wa mapato watikisa Bunge Maalumu
Vigogo hao wa fedha jana walikutana na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu, kujaribu kupata mwafaka wa jinsi suala hilo litakavyowekwa kwenye Katiba Mpya.
Bunge la Katiba limelazimika kuwaita Dodoma
watendaji hao ili kusaidia kukwamua mgogoro wa mapato ya muungano, ambao
uliwagawa wajumbe wa kamati za Bunge hilo wakati wa mjadala wa sura ya
14 kwenye Rasimu ya Katiba.
Pamoja na Profesa Ndulu, wengine waliokuwapo ni
Katibu Mkuu Hazina, Dk Servacius Likwelile na mwenzake kutoka Zanzibar,
Mussa Omar ambao walikuwa na kibarua kigumu cha kupunguza ufa
uliowatenga wajumbe wa Bunge hilo katika misingi ya Ubara na Uzanzibari.
Sura ya 14 ya rasimu ndiyo inayozungumzia masuala ya mapato ya muungano na mgawanyo wake.
Suala la mgawanyo wa mapato ni moja ya mambo manne
magumu yaliyosababisha mvutano mkubwa katika kamati za Bunge hilo kiasi
cha kusababisha Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu kuunda kamati ndogo
ili kulifanyia kazi.
Kutokana na kusababisha mivutano hiyo, Kamati
Namba Moja iliamua kutolijadili kabisa suala hilo na badala yake, kuomba
uongozi wa Bunge uwalete watendaji wakuu wa masuala ya fedha ili watoe
mwongozo wa kuwawezesha wajumbe kujadili na kupata mwafaka wa jinsi
fedha zitakavyoweza kusimamiwa na kugawanywa. Mwenyekiti wa kamati hiyo
ambaye pia ni Naibu Waziri - Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu
alisema walishindwa kupigia kura sura ya 14 baada ya kuona ina utata.
“Ni kweli hatukupigia kura sura ya 14 pekee,
tuliona ina utata mkubwa ambao unahitaji ufafanuzi wa kina na bila shaka
baada ya semina ya leo (jana) tutakutana kufanya uamuzi,” alisema
Mwalimu.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Hamis Hamad
alisema: “Kamati zote zimemaliza kazi, isipokuwa Namba Moja haikupigia
kura sura ya 14 wakitaka ufafanuzi wa kitaalamu, ndiyo maana tumewaleta
wataalamu leo.”
Alisema pamoja na kupigia kura sura hiyo, lakini
hata kamati nyingine zilionekana kutoelewa vizuri sura hiyo, hivyo ujio
wa wataalamu ulilenga kuwawezesha kujadili sehemu hiyo ya Katiba wakiwa
na uelewa mpana.
Habari zinasema sura iliyojitokeza kwenye mijadala
ya kamati zote 12 ilihamia kwenye semina hiyo, ambako ufa ulidhihirika
baina ya wajumbe wa pande hizo mbili za muungano, lakini watendaji hao
kwa kushirikiana na wataalamu wengine walifanikiwa kutoa mwelekeo wenye
matumaini.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI
Post a Comment