HII KALI: FIESTA ISIWE SEHEMU YA KUWADHALILISHA WANAWAKE!!!!!
UMEKUWA ni kama
wimbo wa taifa unaoimbwa kwa ajili ya wasanii wa kike Tanzania, kutokana na
kurudiwa kwa maneno hayo hayo kila kunapokucha.
Serikali na baadhi
ya mashirikisho husika ya sanaa yamekuwa yakikemea suala la wasanii wa kike
kuvaa nguo za nusu uchi katika maonesho yao, lakini kwa
asilimia kubwa hakuna linalorekebishwa.
asilimia kubwa hakuna linalorekebishwa.
Sitaki kuamini kama
msanii anapovaa nguo za aina hiyo ndiyo anaimba vizuri au anacheza vizuri
tofauti na akivaa nguo za kumstiri mwili wake.
Hivi karibuni,
Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania, Kimela Billa,
aliutaka uongozi wa Shirikisho la Muziki Tanzania, umchukulie hatua za
kinidhamu msanii wa muziki wa mduara, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, kwa kosa la
kuvaa nguo ambazo hazikustahili kuvaliwa kwenye umati wa watu.
Sijajua kama msanii
huyo alichukuliwa hatua zozote au kuonywa, kwa sababu hadi sasa anaendelea
kuvaa nguo hizo katika matamasha mbalimbali ya Serengeti Fiesta 2013, ambayo
yanaendelea mikoani.
Ilikuwa ni tamasha
la mkoani Iringa ambako kiongozi huyo aliona msanii huyo amevuka mipaka, lakini
baada ya hapo akazunguka zaidi ya mikoa mitano akiwa anaendelea kuvaa nguo hizo
ambazo zinaijengea tafsiri mbaya tamasha la Serengeti Fiesta, ambalo lipo kwa
ajili ya kutoa burudani kwa wapenzi wa muziki.
Kwa mtu ambaye
anaona mbali na mwenye kujiheshimu, hawezi kwenda kushiriki katika matamasha
hayo kutokana na uvaaji wa wasanii wa kike kuwadhalilisha wanawake wote hata
wale ambao wanajiheshimu.
Si Shilole peke
yake, ni karibu wasanii wote wa kike kama kina Linnah, Recho, Snura na wengine,
naomba mbadilike, hata mkivaa nguo zenye maadili ya Kitanzania nyimbo zenu
zitasikilizwa, tena mtapata na wadau, ambao kwa sasa wanawashusha thamani
kutokana na mnavyojidhalilisha wenyewe kutokana na mavazi yenu.
Kwanini msiige mfano
wa msanii mwenzenu, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’? Nafikiri yeye anajikubali na
anajua umuhimu alionao katika jamii, ndiyo maana anavaa nguo za kujisitiri na
kumfanya aheshimike na kila mtu bila kuchagua rika.
Hata ukiangalia
katika shoo zake, watu ambao wanakwenda ni wale wenye kujiheshimu huku wengine
wakiongozana na wake zao, kutokana na kumkubali msanii huyo, kuanzia kazi zake
mpaka mavazi.
Huwezi kumkuta mtu
mzima na akili zake anakwenda kuangalia shoo ya Shilole na wenzake, hata kama
ana nyimbo nzuri, ataishia kuzisikiliza redioni tu, hiyo yote ni kutokana na
kukera watu na mavazi yao.
Matamasha ya
Serengeti Fiesta yamekuwa ni sehemu ya kuonesha maumbile yao jinsi yalivyo na
kujipotezea soko kwa mashabiki wao pasipo wao kujua.
Nawashauri wanawake
wenzangu, mjitahidi kuvaa nguo za kujisitiri angalau hata kidogo ili muweze
kulinda heshima zenu pamoja na vipaji vyenu kwa wadau wenu.
Msanii unatakiwa
kuwa kioo cha jamii, unapovaa nguo za aina hiyo unakuwa unaifundisha nini jamii
inayokuzunguka? Kwa asilimia kubwa hata wale mabinti ambao wanakuwa wanaiga
mifano ya dada zao kwa kuwaona katika nyimbo zao au matamasha mbalimbali.
Hata serikali nayo
pia inatakiwa kukemea jambo hili na kuwachukulia hatua wahusika wanaoruhusu
hali hii ili wasiharibu kizazi kinachokuja.
Ingekuwa ni mtu wa
mtaani anavaa hivyo, ingekuwa haina maana ya kukemea kadhia hii, lakini kwa
kuwa msanii ni kioo cha jamii na kila mmoja anamuangalia yeye, anapofanya hivyo
anaidhalilisha hata nchi yake, kwa kuwa dunia hivi sasa ni kijiji, hivyo hakuna
siri.
Kwa mtazamo wangu,
wahusika wa matamasha mbalimbali ya binadamu, hususan Fiesta, mjitafakati na
kadhia hii, vinginevyo hata malengo yenu mema yatapotea mbele ya jamii.
SOUCRE: TANZANIA DAIMA
Post a Comment