Malinzi kuzuru Kanda ya Kaskazini, mechi za Electronic kupigwa TA, BK
TIMU za Mgambo Shooting na African Sports za Tanga zitapambana Jumapili (Agosti 31 mwaka huu) katika mechi ya majaribio ya matumizi ya tiketi za elektroniki itakayochezwa kwenye Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga kwa kiingilio cha sh. 1,000 tu.
Mechi nyingine ya tiketi za elektroniki siku hiyo itachezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kwa kuzikutanisha timu za Kagera Sugar na Geita Gold SC ya mkoani Geita. Geita Gold iko Daraja la Kwanza.
Kabla ya mechi hizo, Ijumaa (Agosti 29 mwaka huu) saa 3 asubuhi kwenye viwanja hivyo kutakuwa na mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki pamoja na jinsi mfumo huo unavyofanya kazi.
Washiriki wa mafunzo hayo ni wasimamizi wa vituo vya Tanga na Bukoba, viongozi wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Kagera (KRFA) na Tanga (TRFA), makatibu na maofisa habari wa klabu za Kagera Sugar, Mgambo Shooting, African Sports na Geita Gold, mameneja wa viwanja vya Kaitaba na Mkwakwani na wasaidizi wao, maofisa usalama wa TRFA na KRFA, wachanaji tiketi, wasimamizi wa milangoni, wasaidizi (stewards) na waandishi wa habari.
Wakati huo huo Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atatembelea mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Katika ziara hiyo atakutana na viongozi na kuangalia hali hali ya mpira wa miguu katika mikoa hiyo na mahitaji yake. Pia atazungumzia maono (vision) ya TFF katika mpira wa miguu.
Rais Malinzi atawasili mkoani Manyara, Agosti 29 mwaka huu, na ataanza ziara rasmi katika mkoa huo Agosti 30 mwaka huu. Agosti 31 mwaka huu atakuwa Arusha, na kumalizia Septemba 1 mkoani Kilimanjaro.
Katika ziara hiyo, Rais Malinzi atafuatana na Mkurugenzi Msaidizi (Wanachama) wa TFF, Eliud Mvella. Pia Septemba 8 mwaka huu, Rais Malinzi ataanza ziara ya mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe.
Post a Comment