KUHUSU KUFUTWA KWA AJIRA 200 ZA UHAMIAJI
Katibu Mkuu, Wizara ya
Mambo ya Ndani, Mbarak Abdulwakil akizungumza jana kuhusu kufutwa kwa
ajira 200 Uhamiaji. Kulia ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya jinai
nchini (DCI), Isaya Mngulu. Picha na Venance Nestory
Wizara
ya Mambo ya Ndani imefuta ajira 200 za konstebo na koplo katika Idara
ya Uhamiaji baada ya kubaini kuwa kulikuwa na upendeleo katika usaili na
sasa zitatangazwa upya na kusimamiwa na wizara hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu
Mkuu wa wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil alisema hatua hiyo imechukuliwa
baada ya kamati maalumu ya kuchunguza ajira hizo kubaini wazi kwamba
waliopewa nafasi hizo hawakukidhi vigezo.
Abdulwakil alisema wizara imesikitishwa
na udhaifu huo baada ya kubainika wazi kwamba malalamiko yaliyotolewa na
wananchi na kusababisha wizara kuingilia kati na kufuta usaili wa
kuitwa kwenye ajira kwa watu 200 ulikuwa sahihi.
Alisema baada ya kubainika kwamba kweli
kulikuwa na upendeleo wa dhahiri kwani watahiniwa wenye sifa na
waliopata alama za juu wakati wa usaili hawakuitwa na kukiukwa kwa
vigezo vya wazi, ajira hizo zitatangazwa upya na kusimamiwa moja kwa
moja na wizara na siyo idara hiyo kama ilivyokuwa awali.
“Kamati hiyo iliyoanza kazi yake Agosti
Mosi, mwaka huu ilibaini kwamba hata kigezo cha umri, ambacho ni miaka
25 kwa konstebo na miaka 30 kwa koplo hakikuzingatiwa kwani wenye umri
zaidi ya huo waliitwa kazini... “Lakini zaidi, baadhi ya wasailiwa
walioitwa kazini ni ndugu na jamaa wa watumishi wa Idara ya Uhamiaji,”
alisema.
Alieleza kwamba utaratibu mpya wa
kuwapata watu wanaostahili utatangazwa kupitia vyombo vya habari na
mamlaka ya usimamizi imerejeshwa kwenye wizara husika badala ya kuachiwa
kwenye idara husika.
Alisema pamoja na kwamba miongoni mwa
udhaifu uliobainika ni kwamba matangazo ya kazi yaliyotolewa kwenye
vyombo vya habari hayakuainisha viwango na madaraja ya ufaulu kwa
waliomaliza kidato cha nne na cha sita, lakini hata wale waliofanya
vizuri katika usaili hawakuitwa kazini na hakuna sababu maalumu
zilizotolewa.
Alisema ajira hizo zilizofutwa zinahusisha pia nafasi 28 zilizokuwa zimetangazwa kupitia Idara ya Uhamiaji Zanzibar.
Alisema si kosa kwa ndugu na jamaa wa
watumishi wa Idara ya Uhamiaji kuajiriwa katika nafasi hizo iwapo
wanakidhi vigezo vyote, lakini inapotokea kwamba hakuna msimamizi huru
ni wazi kwamba kunakuwa na upendeleo kama ilivyotokea na idara hiyo
haichukui watumishi kutoka Sekretarieti ya Ajira, kwa kuwa wanaohitajika
ni askari.
Ajira hizo zilitangazwa Februari 17,
mwaka huu na watu 15,707 walijitokeza kuwania nafasi hizo 200, miongoni
mwao, waombaji 1,005 waliitwa kwenye usaili na 200 waliothibitishwa
waliitwa kazini.
Hata hivyo, baada ya tangazo la kuitwa
kazini malalamiko yaliibuka kupitia vyombo vya habari na baadhi ya
mitandao ya kijamii, kwamba baadhi ya walioitwa katika ajira hizo
walikuwa ni watoto, jamaa na ndugu wa maofisa wa Idara ya Uhamiaji.
Baada ya kuibuka kwa malalamiko hayo,
wizara iliingilia kati na kuunda kamati hiyo ya watu watano Julai 31,
ambayo ilipewa siku 10 kukamilisha kazi yake na kutoa matokeo.
Post a Comment