Header Ads

ISIS inavyotesa Wayazidi nchini Iraq

 

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la ISIS wameyafanya maisha ya jamii ya Yazidi kuwa mabaya kwa kuwa wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Irbil, Iraq. Kipi kibaya zaidi: Kuwa mkimbizi au kubaki nchini mwako ufe kwa njaa na kiu?

Ni swali gumu lisilojibika kwa urahisi. Lakini pia ni vigumu kuipata picha halisi ya maisha ya raia wa Iraq wa jamii ya Yazidi ambayo imekuwa ikiyapitia katika kipindi cha wiki mbili baada ya kuwakimbia wapiganaji wa kikundi cha Islamic State of Iraq and Syria ( ISIS).

“Kwa macho yangu nilimshuhudia mbwa akila mzoga wa binadamu,” Tariq kutoka jamii ya Kiyazidi alikiambia kituo cha televisheni cha CNN.

Alisema: “Huu siyo mgogoro. Ni maafa.”

Inapofika usiku, kwa mbali huona mwanga wa taa kutoka katika mji walioukimbia. Wapo juu ya mlima unaowawezesha kuziona vyema nyumba zao, lakini hali ilivyo hawajui kama wataweza tena kurejea huko.

Mlima ambao wamejifadhi kwa sasa, upo karibu na mpaka wa Syria. Kama isingekuwa machafuko nchini humo, huenda ingekuwa kimbilio la Wairaq hawa lakini usalama sasa ni kubakia hapo walipo.

Wanachemsha chai katika kopo dogo, hivyo inawalazimu kurudia mara nyingi ili walau kila mmoja apate kitu cha moto tumboni.

Jua linapochomoza, sauti za ndege za kivita huunguruma juu ya vichwa vyao. Mawazoni mwao hudhani wakati wowote zitadondosha misaada ya chakula na maji, lakini mwishowe muungurumo huo hupotea na kurudi tena baadaye.

Siyo ndege za misaada kama wanavyodhani, bali zipo katika doria ya kulinda mali za wawekezaji katika miji mbalimbali nchini humo.

Inaelezwa kuwa ndege hizo ni za ulinzi wa mji wa Irbil ambao una miradi mingi ya wawekezaji kutoka nchi za Magharibi pamoja na hoteli za kifahari.

Katika mazingira ya nyuzi joto 45.7, wengi wameanza kuchoshwa na njaa na maji ya kunywa yamewaishia.

source: Mwananchi

No comments

Powered by Blogger.