HABARI KAMILI KUHUSU BOMU LA KURUHSWA KUUA WATATU, DEREVA WA JAJI AUAWA KATIKA MLIPUKO HUO HUKO KIGOMA
Watu watatu wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa baada ya mtu
anayesadikiwa kuwa ni jambazi, kurusha bomu ndani ya basi dogo aina ya
Toyota Hiace lililokuwa likitoka Kilelema kwenda Kasulu, Kigoma.
Akizungumza kwa simu jana, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilelema, Benedicto
Mahuta alisema tukio hilo lilitokea saa 11:00 alfajiri kwenye Pori la
Kasesema, lililopo kati ya kijiji hicho na Kambi ya Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ) Migongo, Wilaya ya Buhigwe.
Mahuta alisema wakati gari hilo likipita eneo hilo, mtu mmoja alionekana
amesimama katikati ya barabara huku ameshika bunduki, hali iliyomlazimu
dereva kuongeza kasi.
Alisema hatua 15 baada ya kumpita, walimuona mtu mwingine akiwa
amesimama pembeni mwa barabara na baada ya kumpita, abiria waliokuwa
wameketi nyuma ya basi hilo walishtukia kitu kizito kikitupwa ndani.
Mmoja wa abiria aliamua kukirusha nje lakini kililipuka na kusababisha vifo vya watu wawili na mtoto mdogo.
Mmoja wa abiria walionusurika, Mwalimu wa Shule ya Msingi Kilelema,
Augustino Mkubhaka alisema baada ya mlipuko huo, gari lilipelekwa katika
kambi ya JWTZ kwa ukaguzi.
Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya ya Buhigwe, Samwel Utonga alisema
inasadikiwa kuwa watu waliorusha bomu hilo ni majambazi wanaotokea nchi
jirani.
Dereva wa jaji EACJ auawa
Dereva wa mmoja wa majaji wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EACJ), Ibrahim Msagati amefariki dunia kwa kupigwa risasi iliyofyatuka
kutoka kwenye bastola ya mlinzi wa jumuiya hiyo.
Tukio hilo lililoibua majonzi na simanzi miongoni mwa wafanyakazi wa EAC
lilitokea jana saa saba mchana muda mfupi baada ya kikosi cha ulinzi
cha Jumuiya kumtia mbaroni mtu mmoja aliyefika Makao Makuu ya EAC kwa
tuhuma ambazo hazikujulikana mara moja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alisema tukio hilo ni
la bahati mbaya kwani risasi ilifyatuka kutoka kwenye silaha ya mmoja wa
maofisa usalama wa EAC.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma wa EAC, Richard Otieno-Owora
alimtaja ofisa usalama ambaye risasi ilifyatuka kutoka kwenye bastola
yake kuwa ni Jackson Oula.
SOURCE: MWANANCHI
Post a Comment