Ukweli kuhusu; Askari auawa wakati akiokoa mtoto asiuawe
Askari polisi mwenye namba G.7168 PC Joseph Swai (29) ameuawa kikatili jana asubuhi baada ya kukatwa na panga kichwani
wakati akimuokoa mtoto mwenye umri wa miezi nane asiuawe na baba yake mzazi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani Dodoma, David Misime amesema tukio hilo
lilitokea jana majira ya saa 5 asubuhi katika kata ya Chang’ombe Juu iliyopo katika
Manispaa ya Dodoma.
Amesema chanzo cha kuuawa askari huyo ni kwamba alipigiwa simu na Mtendaji wa kata ya
Chang’ombe juu akimjulisha kuwa amepokea taarifa ofisini kwake kutoka kwa Oliver Baltazar
(52) ambaye ni mkazi wa Chang’ombe juu kuwa kijana wake aitwaye, Tisi Malya
anamtesa mtoto wake mdogo wa miezi nane aitwaye Valerian Malya.
Ameongeza kuwa mama huyo alihisi mtoto huyo ameshakufa kwani alikuwa halii tena.
Aidha, Amesema Mtendaji huyo alimpigia simu askari huyo ambapo walikwenda naye mpaka kwenye
ofisi ya mtendaji wa mtaa na kuongozana naye pamoja na kijana mmoja ambaye ni mtetezi wa
watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi hadi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.
Pia, Amebainisha kuwa alipofika askari huyo aligonga mlango akijitambulisha kuwa yeye ni
askari hivyo alimtaka mtuhumiwa huyo atoke
nje.
“Alichokifanya mtuhumiwa huyo ni
kumnyanyua mtoto wake mdogo wa miezi nane juu kwa mkono mmoja huku miguu ikiwa juu kichwa chini na kutaka kumkata na panga,
na kusema namkata shingo na sitaki kuona mtu hapa,” alisema Misime.
Ameongeza kuwa, “Askari wetu aliamua kumwokoa mtoto huyo na alipomrukia mtuhumiwa kwa bahati mbaya aliteleza na
ndipo mtuhumiwa akamkata kichwani askari
wetu na akadondoka chini kutokana na jeraha
kubwa alilomsababishia.”
Misime amesema kuwa hata hivyo mtuhumiwa
huyo aliendelea kumkatakata kwa panga
ambapo mtendaji na kijana waliyekuwa naye
ambaye ni mratibu wa watoto wanaoishi katika
mazingira magumu iliwabidi kukimbia huku
wakipiga kelele za kuomba msaada.
Hata hivyo waliporudi walimkuta askari huyo
ameshafariki dunia palepale.
“Mtuhumiwa baada ya kufanya kitendo hicho cha kinyama alikimbia huku nguo zake zikiwa zimetapakaa damu huku akiwa na panga
mkononi,” Alisema Misime.
Amesema msako bado unaendelea ili kuweza kumtia nguvuni mtuhumiwa huyo
aliyesababisha kifo cha askari huyo wakati akijitolea maisha yake kwa ajili ya kumwokoa
mtoto mdogo.
Naye mtoto huyo alipookolewa mama yake mzazi ambaye hakufahamika jina lake mara
moja na ambaye anasemekana kuwa ana matatizo ya akili alimchukua mwanaye na
kukimbia mahali pasipojulikana ambapo kamanda amesema kuwa hata hao wanatafutwa ili kujua usalama wao.
Source: EATV
Post a Comment