Header Ads

Mbelgiji Akamatwa na Fuvu la Kichwa cha Binadamu -Dar

Matukio ya wasafiri kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakiwa na nyara za Serikali na dawa za kulevya, yanazidi kuchukua sura mpya baada ya raia mmoja wa Ubelgiji kukamatwa akiwa na fuvu la binadamu.

Raia huyo, Balcjan Christine Weejktgns (49), alikamatwa Jumatatu saa 2.30 usiku wakati
akiwa katika taratibu za kuingia uwanjani hapo tayari kwa safari ya kuelekea Ubelgiji kupitia
Zurich, Uswisi.

Tukio la kukamatwa kwa Mbelgiji huyo ni mwendelezo wa matukio ya aina yake uwanjani hapo baada ya watu wengine wawili kukamatwa kwa nyakati tofauti kwenye uwanja
huo wakiwa na kucha za simba na kenge walio hai.

Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Hamisi Selemani alisema mtu huyo alikutwa ameficha fuvu hilo la binadamu kwenye mfuko wa
plastiki.

“Alivyopita kwenye mashine za ukaguzi tulimtilia shaka na tulipompekua tulimkuta
amebeba fuvu la kichwa cha binadamu kikiwa kimewekwa kwenye mfuko wa plastiki ndani ya
sanduku alimokuwa ameweka nguo zake na vitu mbalimbali,” alisema Selemani.

Raia huyo anadaiwa kuwa ni mkazi wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro na inadaiwa kuwa alikuwa nchini kwa ajili ya
kufanya utafiti.

Kamanda Selemani alisema baada ya askari wa kikosi cha polisi cha kimataifa cha mwali Julius Nyerere kumhoji kwa undani madhumuni ya kubeba fuvu, alisema ni mali yake na kuwa alikuja nalo nchini kutoka
Ubelgiji.

“Kwa maelezo yake alidai kuwa fuvu hilo analimiliki muda mrefu tangu alipoingia nchini mwaka 2000 akitokea Ubelgiji akidai kuwa yeye ni mtafiti,” alisema.

Pamoja na raia huyo wa Ubelgiji kujitetea kuwa ni mtafiti, Kamanda Selemani alisema sheria za nchi haziruhusu mtu kumiliki viungo vya binadamu hivyo anayekiuka lazima akamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Jeshi la polisi haliwezi kuona taratibu za nchi zikivunjwa hata kama ni raia wa kutoka nje ya
nchi ambaye amekuja kufanya utafiti nchini. Lazima afuate sheria,” alisema na kuongeza

“Wito wangu ni kwamba watu wote wanatakiwa kufuata taratibu za nchi. Huyu raia ameona kitu cha kawaida kuishi na fuvu la kichwa, lakini hapa ni tofauti na nchini kwao,” alisema.

Alisema polisi inaendelea na upelelezi ili kujua sababu ya Mbelgiji huyo kusafirisha fuvu hilo na kuahidi kuwa uchunguzi ukikamilika, atafikishwa mahakamani.

No comments

Powered by Blogger.