Header Ads

Picha za Albino Walivyotwangana Ngumi Jana IKULU, Ziko Hapa!

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), wamepigana ngumi
na mateke wakigombea kuingia kumwona Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo la aina yake lilitokea jana majira ya saa nne asubuhi ambapo lilianzia kwenye eneo la
mapokezi Ikulu mara baada ya walemavu hao kukaguliwa na kuwekwa kwenye chumba
maalumu cha kupumzikia wageni.

Baada ya muda, ofisa wa Ikulu alifika kwenye chumba walipokuwa walemavu hao akiwa na
karatasi yenye orodha ya watu 15, ambao ndiyo
waliopaswa kumwona Rais.

Baada ya ofisa huyo kuanza kusoma majina ya wahusika, albino wote waliokuwa kwenye chumba
hicho walinyanyuka kutoka kwenye viti vyao na kusimama karibu na mlango, ambako alikuwa
amesimama.

Kila ofisa huyo alipokuwa akisoma jina, mhusika
alitoka nje ya chumba hicho tayari kwa kwenda
kumwona Rais.

Baada ya ofisa huyo kumaliza kusoma majina hayo, alisema: “Hawa ndio wanaokwenda
kuwawakilisha kwa sababu hamuwezi kuingia
kundi lote hili.”

Baada ya majina hayo kutajwa, mmoja wa albino hao, Nuru Chagutu, ambaye hakutajwa, alisema hakubalini na kitendo cha viongozi pekee
kumwona Rais ili hali wajumbe wengine ambao
pia ni wahathirika wa mauaji ya albino wakibaki
getini.

Alisema pia yeye na wanaharakati wenzake wa Chama cha Tunataka Haki ya Kuishi (THK),
hawamtambui Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Ngozi Tanzania (TAS), Ernest
Kimaya, ambaye alikuwa kwenye orodha ya watu 15 waliopangwa kumwona rais.

Alihoji pia sababu za Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shivyawata),
Amon Mpanju, ambaye si mlemavu wa ngozi, kuwamo kwenye orodha hiyo huku akiwa si mlemavu wa ngozi.

“Kama huyu mtu mweusi (Mpanju) ataingia pamoja na mwenyekiti (Kimaya) na sisi tutaingia,
vinginevyo mkutano ufe,” alisema Nuru.

Baada ya maelezo hayo, watu waliokuwa wamechaguliwa nao walionekana kutoridhishwa
na kauli ya Nuru, hivyo kukaibuka kurushiana maneno kati ya pande hizo mbili.

“Kama sisi hatuingii, chukueni simu zenu tutoke wote, hakuna kubaki mtu ndani, wote tuondoke,
mkutano umekufa,” alisikika mtu mwingine akisema.

Baada ya kurushiana maneno kuzidi, ofisa mmoja na Ikulu aliamuru walemavu hao pamoja na
waandishi wa habari waliokuwa kwenye eneo hilo watoke nje.

Baada ya amri hiyo, watu wote walitoka nje ya chumba hicho cha mapokezi na kuendelea
kurushiana maneno wakiwa kwenye viwanja hivyo vya Ikulu.

Ofisa huyo wa Ikulu aliwafuata tena na kuwaambia: “Ninaposema mtoke nje, ninamaanisha ni nje ya geti.”
Baada ya kauli hiyo, wale waliokuwa wametajwa majina tayari kwenda kumwona Rais, walirudi
tena kwenye chumba cha mapokezi kuchukua simu zao tayari kwa kutoka nje ya geti.

“Chukueni simu tuondoke, hakuna kubaki mtu, leo hakuna kusaini (kuchukua fedha),” alisikika
mmoja wa walemavu hao akisema.
Baada ya kutoka nje ya geti la Ikulu, waliendelea kumwandama Kimaya kwamba hawamtambui na
kuwa hata ofisi alizokuwa akizitumia kwa sasa
zimefungwa.

“Yanapotokea matukio ya mauaji tunapowaambia viongozi wetu atumwe hata mwakilishi, wamekuwa wakikataa huku wakisema ‘kufa, kufaana’, hiyo si sahihi, wao wananeemeka na kuota vitambi na kupewa magari, lakini sisi tumekuwa tukiendelea kuteseka,” alisema Nuru.

Baada ya kauli hiyo, Kimaya alimpiga teke Nuru huku akimwambia; “huwezi kutunyima haki ya kuingia kwenye kikao kumsikiliza Rais.”

Baada ya Kimaya kumpiga Nuru, walemavu wengine waliokuwa wakimpinga mwenyekiti huyo
wa TAS, walianza kumshambulia kwa maneno.

“Kwanini unampiga Nuru wakati anakwambia ukweli? Kwanza muda wako ulishakwisha. TAS hakuna viongozi na ofisi zimefungwa…hatukubali, tunakupiga na kwenye kikao tunaingia wote?” alisikika mmoja wa walemavu hao aliyetambulika kwa jina la Amon Anastaz.

Baada ya vurugu hizo kuendelea kwa dakika kadhaa, ofisa wa Ikulu aliyekuwa na beji kifuani yenye jina la Andrew M.M.S, aliwataka walemavu  hao kupanda magari waliyokuja nayo na wakachaguane ili wapate wawakilishi wanaowataka.

Walemavu hao kwa ujumla wao walitii amri hiyo na kuondoka na kisha kurudi tena mchana ambapo walifanya kikao na mheshimiwa Rais .

Source; Mpekuzi

No comments

Powered by Blogger.