Header Ads

YANGA YABARIKI NGASA KUONDOKA JANGWANI

Uongozi wa Yanga SC umesema winga wake hatari, Mrisho Khalfan Ngasa, atakuwa huru kuondoka katika klabu hiyo ya Jangwani
baada ya kumalizika kwa msimu huu.

Tamko hilo la uongozi wa Yanga SC,
limetolewa ikiwa ni muda mfupi baada ya nyota tegemeo katika kikosi cha timu ya taifa
ya Tanzania (Taifa Stars) kuandika maneno na kutoa ishara za kuwaaga na kuwashukuru
mashabiki wake kwa kumpa sapoti katika kipindi chote alichokaa katika klabu hiyo ya Jangwani.

Ngasa, mfungaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwaka jana na mfungaji bora wa Yanga SC msimu uliopita, mwishoni mwa wiki alikisaidia kikosi cha wanajangwani kupata ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Platinum FC ya Zimbabwe kwenye Uwanja wa Taifa jijini hapa na kuwa na uhakika wa asilimia zaidi ya 90 kusonga mbele katika michuano ya kimataifa mwaka huu.

Katika mechi hiyo ya hatua ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Ngasa alifunga mabao mawili na kupika mengine mawili, lakini muda mfupi baada ya mechi hiyo kumalizika, mzaliwa huyo wa Jiji la Mwanza akaandika maneno kwenye ukurasa wake wa Instagram yanayoashiria kuondoka Yanga SC.“Kwa heri Yanga. Nakupenda, nashukuru kwa kila kitu,” ulisomeka ukurasa wa Ngasa wa instagram Jumatatu jioni.

Mtandao huu umeutafuta uongozi wa Yanga SC ambao umeweka wazi kwamba atakuwa huru kuondoka Jangwani baada ya msimu huu.
"Kwenye ukurasa ule yale si maneno yaNgasa, ninadhani kuna mtu ameamua kufanya
hivyo.

Hata hivyo, Ngasa hajasaini mkataba mpya na Yanga, hivyo yuko huru kujiunga na timu nyingine baada ya kumalizika kwa msimu huu," amesema Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC.

Katika mechi dhidi ya Platinum FC, Ngasa ambaye miezi miwili iliyopita aliweka wazi kutokuwa na furaha Yanga SC kutokana na deni la zaidi ya Sh. milioni 40 alizowalipa Simba SC kufanikisha kuwatumikia mabingwa hao mara 24 wa Tanzania Bara (Yanga SC), hakushangilia mabao yote waliyofunga Jumapili.

Aidha, Nyota alionekana akikutanisha viganja vyake ikiwa ni ishara ya shukrani huku pia akionyesha ishara ya kulia, kilio ambacho hata hivyo, kilihusishwa na kifo cha kocha Sylivester Marsh aliyemuibua.

Ngasa baada ya kufunga bao lake la pili na la tano kwa Yanga SC Jumapili, alionekana akikunja mikono miwili na kuiweka kifuani, jambo ambalo liliashiria kuomba msamaha, kisha akanyanyua mikono juu na chini kuashiria anatoa shukrani na baadaye akaonyesha ishara ya kulia akiweka mkono wake wa kushoto usoni.

Katika ukurasa wake huo, Ngasa aliposti picha yake ya mechi ya juzi akilia na aliambatanisha
na maneno hayo.

Mbali na Yanga SC, mkali huyo wa kufumania nyavu, amewahi kuzichezea timu za Kagera
Sugar FC, Azam FC na Simba SC.

Hata hivyo, Ngasa anahusishwa na klabu za Afrika Kusini na TP Mazembe FC ya DR Congo zinazowania saini yake.

No comments

Powered by Blogger.