BIASHARA HARAMU YA WATOTO: Serikali yatoa saa 48 kuhakiki wageni
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama
Serikali mkoani Kilimanjaro, imetoa saa 48 kwa maofisa watendaji kata, vijiji na mitaa, kufanya zoezi maalum la uhakiki wa wageni, wanaodaiwa kutumia mwavuli wa dini kuendesha biashara haramu ya wizi wa watoto.
Agizo hilo limekuja siku chache baada ya kugundulika mahali
walipofichwa watoto 29, wanaodaiwa kupotea kwenye mazingira ya
kutatanisha katika mikoa 13 nchini na kuhifadhiwa kwenye makazi hayo
kinyume cha sheria za nchi.
Mkuu wa mkoa huo, Leonidas Gama, akizungumza na NIPASHE Jumapili,
kuhusiana na uhakiki huo, alisema unalenga kusaidia kupunguza hofu na
hasira ya umma kuhusiana na usalama wa watoto hao; na mahali
wanakopelekwa baada ya kupatiwa mafunzo maalum ya kujihami pamoja na
elimu ya dini.
“Nimeagiza ndani ya saa 48, kila mtendaji kwenye ngazi za vijiji,
mitaa na kata, wawe wamewatambua watu wote na kuwasilisha taarifa za
siri kwa wakuu wa wilaya zao. Baada ya zoezi hilo nitatoa taarifa rasmi
kwa umma, Jumanne ya wiki ijayo kuhusu hali ya usalama katika mkoa
wetu,” alisema Gama.
Watoto walio okolewa hadi sasa, baada ya kugunduliwa kwa matukio
hayo ni wenye umri wa miaka miwili hadi 16, ambao walikutwa
wamehifadhiwa kwenye nyumba moja, iliyopo karibu na uwanja wa Mandela,
Kata ya Pasua, Manispaa ya Moshi, mali ya mfanyabiashara wa nguo nchini
Kenya, Abdelnasir Abdurahaman, maarufu kama Karata (33), huku watoto
wengine 11, wakiokolewa pia katika kituo cha UMM Sakhail, kilichopo
Lyamungo, Wilaya ya Hai.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Tangazo la Serikali namba 280 la mwaka
2002, pamoja na kifungu cha 353 cha Sheria ya Elimu, iliyofanyiwa
marejeo mwaka 2002; mzazi yeyote au mlezi atakayeshindwa kuhakikisha
mwanae anapata elimu ya msingi kwa wakati husika, atashtakiwa,
kulipishwa faini au kupata adhabu ya kifungo, iwapo atashindwa kutimiza
matakwa ya sheria hiyo.
Kufuatia taharuki hiyo kuikumba mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na
Manyara, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu, juzi
alilazimika kukutana na kutetea kwa zaidi ya saa sita na timu ya
makachero wa makao makuu ya jeshi hilo pamoja na maofisa wake wa mkoa wa
Kilimanjaro, ikiwa ni siku tano baada ya kukamatwa kwa wafanyabiashara
wanaodaiwa kuwahifadhi watoto kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Alipoulizwa iwapo watoto hao, wanatokea mikoa ipi ya Tanzania;
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, alisema uchunguzi wa
awali unaonyesha kuwa watoto hao ni wakazi wa mikoa ya Tanga, Mtwara,
Mbeya, Tabora, Manyara, Arusha, Kagera, Mara, Kilimanjaro, Dodoma na
Shinyanga.
Post a Comment