Header Ads

IKULU YALITEGA BUNGE

KATIBU Mkuu Kiongozi , Balozi Ombeni Sefue, amesema kuwa Rais Jakaya Kikwete hawezi kuchukua hatua kwa sasa dhidi ya viongozi
wanaodaiwa kuchota mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow , hadi uchunguzi juu
ya kashfa hiyo ukamilike.

Bunge lilitoa maazimio nane kuhusiana na tuhuma hizo , ambayo yameshafika mezani kwa Rais Kikwete na kuwa , hatua
zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kuwa
na makosa yakiwemo ya kimaadili .

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Balozi Sefue, alisema Rais ataagiza vyombo vya uchunguzi ambavyo vitatoa ripoti yake na hatua zitachukuliwa kwa kuwa atakuwa amepata undani wa suala hilo.

Balozi Sefue, alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitaka kuona Rais Kikwete akilishughulikia pamoja na kuchukua hatua
katika suala hilo baada ya kukabidhiwa maazimio ya Bunge .

“ Yapo makundi mbalimbali yanayotaka kuona Rais Kikwete akiwawajibisha na kuchukua
hatua zaidi baada ya kupokea maazimio nane ya Bunge , jambo hilo haliwezekani kushughulikiwa hivyo , ” alisema.

Alisema kuwa , vyombo vya uchunguzi vina utaratibu wa kufanya kazi na kuwa haviwezi kufanya kazi hadharani, kwani sio taratibu za kiuchunguzi.

“ Uchunguzi kuhusu uchotwaji wa mabilioni hayo uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG ) , pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru ), ni sehemu ya uchunguzi, ” alisema.

Balozi Sefue, alisema kuwa maazimio ya Bunge yaliyolewa ni mazuri na yana umuhimu wake, kwani sio ya kupuuzwa, lakini katika ngazi ya Rais Kikwete, inapaswa naye apate muda zaidi pamoja na taarifa za uchunguzi ili kufahamu kwa undani suala hilo.

“ Vyombo vinavyofanya uchunguzi kuhusiana na suala hili ni vile ambavyo vilitajwa kufanya hivyo katika maazimio manane ya Bunge , ” alisema.

Baadhi ya maazimio ya Bunge ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama viwachukulie watuhumiwa wote hatua stahiki, Kamati tatu za kudumu za Bunge ziwavue nyadhifa zao wenyeviti watatu wa kamati husika waliotajwa kuchukua fedha za Escrow.

Pia maazimio mengine ni Rais aombwe kuunda tume ya kijaji kuwachunguza majaji wawili kuhusu tuhuma za utovu wa maadili , mamlaka husika za kifedha zichunguze baadhi ya benki kujihusisha na utakatishaji wa fedha , Serikali iwasilishe muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Takukuru ili kushughulikia na kupambana na rushwa kubwa.

CHANZO: TANZANIA DAIMA

No comments

Powered by Blogger.