Header Ads

Daktari Feki Anaswa Muhimbili


Wimbi la madaktari feki limezidi kushika kasi nchini baada ya ‘daktari’ mwingine wa aina hiyo
kukamatwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa Ubongo (Moi) Muhimbili,
jijini Dar es Salaam.

Daktari huyo feki alikamatwa jana ikiwa imepita miezi 10 tangu kukamatwa mtu kama huyo katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es
Salaam.

Mtu huyo alikamatwa baada ya daktari mwingine feki kukamatwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC,
iliyoko Moshi, mkoani Kilimanjaro, Septemba, mwaka jana.

Aliyekamatwa Moi jana, ametambuliwa kwa jina la
Dismas Macha (35), ambaye ni mkazi wa Upanga
Magharibi, jijini Dar es Salaam mzaliwa wa Moshi
vijijini, mkoani Kilimanjaro
Alikamatwa baada ya kukutwa akihudumia wagonjwa katika moja ya wodi za taasisi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dk. Athuman Kiloloma, akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo, alisema mtuhumiwa alikamatwa saa 3:00 asubuhi jana akiwa amevaa sare za taasisi hiyo.

Alisema daktari huyo alikutwa akiwa na nyaraka za Moi na vifaa mbalimbali vya kutibu wagonjwa, zikiwamo glovu, Vitu vingine alivyokutwa navyo ni ripoti za wagonjwa, dawa na vifaa vya kutolea mimba.

“Hili ni tatizo kwa mtu asiye na sifa kujiita daktari na kuanza kukusanya michango kutoka kwa madaktari kwa kisingizio kuwa mkewe amefariki nchini India, hivyo alikuwa akikusanya fedha ili kuwezesha mwili kurudishwa nchini,” alisema Dk. Kiloloma.

Alisema mtu huyo alikamatwa baada ya kuonekana
akihudumia wagonjwa akiwa na karatasi yenye orodha ya majina ya zaidi ya watu 30, wakiwamo madaktari na wafanyakazi wa taasisi hiyo Dk. Kiloloma alisema karatasi hiyo inaonyesha kuwa, mtu huyo alikuwa anawaomba madaktari na wafanyakazi hao mchango kwa ajili ya kupata fedha za kusafirisha mwili wa mkewe, ambaye amefia nchini India.

Alisema baada ya kukamatwa na kuhojiwa, mtu huyo alidai kuwa yeye ni mkazi wa Buguruni.

Hata hivyo, alisema baada ya kupekuliwa, alikutwa na kitambulisho cha kupigia kura kinachoonyesha kuwa ni mkazi wa Upanga Magharibi, jijini Dar es
Salaam, Naye Dk. Kiloloma alisema jana haikuwa ni mara ya kwanza kwa ‘daktari’ feki huyo kuonekana Moi.

Alisema mara ya kwanza, mtu huyo alionekana Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas) na kwamba, katika mahojiano, alidai kuwa yeye ni mwanafunzi wa chuo hicho wa shahada ya uzamili.

Dk. Kiloloma alisema baada ya kuonekana Muhas,
uongozi wa MNH ulibandika tangazo na picha ya mtu huyo lililokuwa likieleza kuwa hahusiki katika hospitali hiyo.

Pia, Alisema baada ya kukamatwa na kuhojiwa, awali alidai kwamba, alikwenda Moi kwa ajili ya kumuona
mgonjwa, lakini baadaye akasema alikwenda kumuona ndugu yake, ambaye ni daktari katika taasisi hiyo.

Aidha, Kuhusu nyaraka alizokutwa nazo, Dk. Kiloloma alisema mtu huyo alipoulizwa, alisema alinunua
kwa matumizi yake binafsi.

‘Daktari’ feki huyo alifikishwa katika kituo cha polisi Salender Bridge, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa Ilala, Mary Nzuki, hakupatika kuzungumzia tukio hilo.

No comments

Powered by Blogger.