Header Ads

SIMBA SC: SINGANO “MESSI" DAWA YAKO IKO JIKONI

Simba SC imetishia kumchukulia hatua Ramadhani Singano Messi

SIMBA SC inajipanga kumchukulia hatua mchezaji wake, Ramadhani Singano ‘Messi’ kwa kuituhumu klabu hiyo kughushi Mkataba wake.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ‘Zungu’ amefanya Mkutano wa kwanza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Msimbazi tangu arejee kutoka Afrika Kusini kusaka vipaji kwenye Kombe la COSAFA.
Na Manara amesema kwamba Simba haijachezea mkataba wa Messi kama anavyodai, ila wanaamini hiyo ni janja yake kwa kushirikiana na klabu inayomtaka, kutaka kumchukua bila malipo.
“Simba inatambua mkataba wa Messi unamalizika mwakani na si mwaka huu kama anavyodai. Kama kuna klabu inamuhitaji mchezaji huyo, bora ijitokeze na kufanya mazungumzo ramsi na Simba ambayo ilimuibua nyota huyo,”amesema Manara.
Mtoto huyo wa kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Sunday Manara ‘Kompyuta’, amesema kwamba pia wanashangazwa na kuibuka kwa Meneja wa Messi.
Hajji Sunday Manara 'Zungu' akizungumza na Waandishi wa Habari leo Msimbazi

“Huyo anayejiita Meneja wa Messi, anatambulika wapi kisheria?”alihoji na kuongeza; “Kitendo alichokifanya Messi kinafanyiwa kazi na mamlaka za ndani za Simba na baadaye tutatoa tamko la hatua tuliyochukua,”.
Messi aliyeibukia timu ya vijana ya Simba SC miaka minne iliyopita, hivi karibuni ameibua shutuma dhidi ya klabu yake hiyo kwamba imeghushi Mkataba wake.
Messi anadai Mkataba wake halali ulikuwa unamalizika mwaka huu, na si huu wa sasa ambao inaelezwa utamalizika mwakani.
Na Messi si mchezaji wa kwanza kuishutumu Simba SC kughushi Mkataba wake, kwani wachezaji wengine za zamani wa klabu hiyo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Kevin Yondan wamewahi kutoa malalamiko kama hayo wakati wanahamia kwa mahasimu, Yanga SC.
 
 Na Princess Asia, DAR E SALAAM
 
 

No comments

Powered by Blogger.