Header Ads

VIJIMAMBO: KIKONGWE ANUSURIKA KUUAWA NA WANANCHI, AKIDHANIWA KUWA NI MCHAWI

Katika hali isiyokuwa ya kawaida bibi mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa Miaka (65) ambaye hakujulikana jina lake wala makazi yake amenusurika kuuawa na wananchi baada ya kudhaniwa kuwa ni mchawi.

 Tukio hilo lililoshangaza na kushtua wakazi wa wilaya ya Geita mkoani Geita limetokea jana Septemba 02,2014,majira ya saa 3.30 asubuhi katika mtaa wa Tambuka reli ikiwa ni kilomita chache tu kufika Stendi ya Magari madogo yanayokwenda katika vijiji vya mkoa huo.
Akizungumzia tukio hilo mmoja wa mashuhuda, Joyce Mcherwa ambaye ni mfanyabiashara wa eneo hilo alisema yeye alikuwa anafagia nje ya kibanda chake na kushangaa mama huyo anaanguka kutoka angani bila kuwa na kitu chochote.
Alisema mama huyo alikuwa uchi wa mnyama amejifunga kitambaa chekundu kichwani na hirizi shingoni.
Joyce aliongeza kuwa mama huyo alikuwa hajitambui huku akihangaika kupaa tena kwa  kurusha mikono yake na kupiga kelele za  kuomba msaada wa kutaka kupewa maji ya kunywa.
Muda mfupi baadaye alikata kauli (hakuweza kuongea tena) na kukaa kimya kama bubu.
Kufuatia hali hiyo shuhuda alipiga kelele kuomba msaada kwa wananchi waliokusanyika na  kutaka kumuua wakidai kuwa vikongwe kama hao wamekuwa wakisumbua wananchi kwa kuwaroga.
Hata hivyo baada ya wananchi kufika na kutaka kumuua kwa kumchoma moto askari polisi wa kituo kidogo kilichopo katika stendi hiyo waliweza kunusuru mama huyo  na kumpeleka katika Hospitali ya wilaya ya Geita kwa kuwa alikuwa ameumia kichwani.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita Adam Sijaona alikiri kumpokea mama huyo na kuongeza kuwa ameumia kichwani kwa kuangukia jiwe lakini alikuwa hajitambui wala alikuwa haongei na kulazwa wodi namba saba (7) kwa ajili ya matibabu zaidi.
Jeshi la Polisi Mkoani hapa limedhibitisha kutokea kwa tukio hilo na uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea kubaini chanzo chake.

No comments

Powered by Blogger.