Header Ads

Maximo awashtukia



YANGA ipo vizuri katika safu za ulinzi na kiungo, kilichobaki sasa kocha wake, Marcio Maximo, anaifanyia marekebisho kwa nguvu safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Genilson Santos ‘Jaja’ na mwenzake Mrisho Ngassa ili ifunge mabao mengi.
Katika mechi tatu za kirafiki, bosi huyo hajaridhika na ufungaji wa wachezaji hao na anataka kuwapa
mbinu kwa haraka zaidi kabla msimu haujaanza Septemba 20. Katika mechi dhidi ya Chipukizi Yanga ilishinda bao 1-0, ikacheza na Shangani ikawachapa mabao 2-0 na kumaliza na KMKM iliowakung’uta mabao 2-0.
Katika mchezo dhidi ya Chipukizi, bao pekee la Yanga lilifungwa na Jaja, huku katika mchezo na Shangani, mabao ya Yanga yalitumbukizwa na Andrey Coutinho na Salum Telela. Mabao mawili ya Yanga dhidi ya KMKM yalifungwa na Coutinho na Hussein Javu.
Matokeo hayo yanamaanisha Yanga ina uwezo wa kushinda kuanzia bao moja hadi mawili, hivyo Maximo sasa anainoa safu yake ya ushambuliaji iweze kupata mabao mengi zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maximo alisema anafurahi kuona safu za ulinzi na kiungo zikifanya vizuri katika kuokoa na kuanzisha mashambulizi, lakini kuna kazi kidogo katika safu ya ushambuliaji ambayo anataka ifunge mabao mengi.
Katika mechi tatu ilizocheza Zanzibar, Yanga imefunga jumla ya mabao matano na haikuruhusu kufungwa hata bao moja.
“Safu ya ulinzi inafanya vizuri kama ilivyo ile ya viungo, maana katika mechi tatu tulizocheza Zanzibar hawakuruhusu bao. Kuna kazi inatakiwa kufanywa kwa washambuliaji ili kuwaongezea makali kidogo,” alisema.
“Siyo kwamba hawafai isipokuwa natakiwa kuwaongezea nguvu ili tuweze kupata mabao mengi kwani inaonyesha kuna tatizo dogo kwenye umaliziaji.”
Jana Jumatatu kwenye mazoezi ya Yanga yaliyofanyika Uwanja wa Sekondari ya Loyola, Maximo alitumia muda mrefu kuwaelekeza washambuliaji na viungo namna ya kupiga krosi na kuunganisha ili kutengeneza nafasi nyingi za kufunga na kupata ushindi mkubwa kwenye mechi.
Coutinho alionekana kuwa hodari katika kupiga krosi kutoka upande wa kushoto kwani mara nyingi mipira yake ilifika sehemu sahihi na washambuliaji walipiga vichwa au mabeki kuokoa.
Beki Juma Abdul alionekana mara kadhaa akimwanzishia mipira Coutinho ambaye alikuwa akiiwahi na kisha kupiga krosi zilizokuwa zikiingia katika eneo la hatari na kuunganishwa na washambuliaji.
Jirani ya Coutinho alikuwepo kocha msaidizi anayeshughulikia vijana, Shadrack Nsajigwa, ambaye alikuwa akimwelekeza jambo Abdul namna ya kumfikishia mipira Coutinho ambaye alionekana yupo makini muda wote.
SOURCE: MWANASPORT

No comments

Powered by Blogger.