CCM kuwakaanga wabunge ‘watoro’
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
Dodoma. Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kinakusudia kuwachukulia hatua wabunge wake zaidi ya 25 kwa makosa
ya kutoshiriki kikamilifu vikao vya Bunge Maalumu la Katiba
vinavyoendelea Dodoma.
Mpango huo ulitangazwa juzi usiku na Katibu wa
Wabunge wa CCM, Janister Mhagama kwenye kikao kilichoitishwa kwa ajili
ya kuwajulisha wabunge wa chama hicho mwongozo wa mjadala katika Bunge
Maalumu.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Mhagama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, alitoa maelezo hayo mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Hata hivyo, mtoa habari wetu alisema Kinana
hakuzungumza chochote zaidi ya kusikiliza hoja za wajumbe wa kikao
hicho, wakati Pinda alitoa maneno machache ya ufunguzi na baadaye
kufunga.
Alisema wabunge hao wataandikiwa barua wajieleze kwa nini hawafiki kwenye vikao vya Bunge Maalumu tangu limeanza.
Habari hizo zimepasha kuwa baada ya Mhagama
kuanzisha hoja hiyo aliinuka Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde ambaye
alisema lazima suala hilo lifanywe kwa umakini.
Lusinde alinukuliwa akiwatetea wabunge hao akisema
baadhi yao hawapo bungeni kwa vile wapo watu wanaoyashambulia majimbo
yao kwa malengo ya 2015.
Alisema baadhi ya wanaoshambulia majimbo hayo ni
makatibu na wenyeviti wa CCM wa wilaya na mikoa, hivyo wabunge hao
hawawezi kutulia bungeni wakati majimboni kunawaka moto.
Hoja hiyo ya Mhagama iliibua maswali mengi yasiyo
na majibu kutoka kwa baadhi ya wabunge waliosema CCM haina mamlaka ya
kumwadhibu mjumbe isipokuwa Mwenyekiti wa Bunge.
“Huko ni kutapatapa. Kanuni za Bunge hili ziko
wazi kama kuna mjumbe ana udhuru atalazimika kutoa taarifa kwa
mwenyekiti siyo CCM au taasisi aliyoingia nayo,” alidokeza mbunge mmoja.
Kifungu Namba 15 (1)(4) cha Kanuni za Kudumu za
Bunge hilo kinaeleza adhabu ya mjumbe asiyehudhuria vikao hatalipwa
posho ya kikao na kama atakuwa tayari amelipwa atairudisha.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye alisema Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM iliwahi kuomba
baraka za Kamati Kuu ya chama hicho ili iweze kuwachukulia hatua watovu
wa nidhamu na kwamba ilipewa mamlaka hayo.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI
Post a Comment