SERIKALI YASITISHA VIBALI VYA MATANGAZO YA WAGANGA WA JADI KWENYE VYOMBO VYOTE VYA HABARI

Serikali
imesitisha vibali vya kurusha matangazo ya tiba za asili na mbadala
kwenye vyombo vyote vya habari baada ya kubaini kuwa yanapotosha jamii.
Taarifa
iliyotolewa na Baraza la Tiba za Asili na Tiba Mbadala kwa vyombo vya
habari jana, inaeleza kuwa katika siku za karibuni kumekuwapo na
matangazo mbalimbali ya tiba hizo ambayo baadhi yake hayaisaidii jamii.
Kutokana
na taarifa hiyo ya baraza, vyombo vya habari havipaswi kupokea kibali
chochote cha kutangaza matangazo ya tiba hizo hivi sasa, kwa kuwa ni
batili.
“Hivyo
basi kituo chochote cha redio, luninga, mitandao na magazeti
hayaruhusiwi kurusha tangazo lolote linalohusiana na mambo ya tiba asili
na mbadala kwa kipindi hiki,” ilisema taarifa iliyosainiwa na Lucy
Mziray.
Pia
taarifa hiyo inaeleza kuwa, chombo chochote kitakachorusha tangazo au
kipindi kitatozwa faini na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizungumzia
uamuzi wa Serikali uliochukuliwa, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania
(MAT), Dk Primus Saidia alisema kuwa matangazo ya tiba mbadala na asili
kwa muda mrefu yamekuwa yakipotosha umma kwa kukiuka Sheria ya Waganga
na Tiba Mbadala ya mwaka 2002 inayowazuia kujiita madaktari na
kujitangaza kwenye vyombo vya habari.
“Wanakwenda
kinyume wanajiita madaktari, wengine maprofesa, halafu wanakwenda mbali
zaidi na kuvaa vifaa vya udaktari kwenye televisheni ili kuwavutia
watu,” alisema Dk Saidia.
Aliongeza:
“Kuna watu wanatangaza kuwa wanatibu figo kwa siku saba jambo ambalo
haliwezekani duniani kote, wanachofanya ni kuwachelewesha wagonjwa
kwenda hospitali mapema.”
Naye
mtaalamu wa tiba za asili, John Kidua, alisema serikali imefanya kosa
kuyazuia matangazo yote badala ya kuwaadhibu watu waliobainika
kuipotosha jamii pekee yao.
Alisema
upo uthibitisho kuwa baadhi ya dawa za asili zinatibu vizuri kuliko
dawa za hospitali jambo ambalo limekuwa kikiokoa fedha nyingi za
kuwasafirisha wagonjwa nje ya nchi.
Post a Comment