Jinamizi la serikali tatu laibuka upya

Mjumbe wa Bunge Maaalum,Said Arfi.
Jinamizi la muundo wa serikali mbili au tatu limeibuka tena katika Bunge Maalumu la Katiba, baada ya wajumbe wachache kuwapinga wenzao wanaounda maoni ya wengi kwa hatua yao ya kufuta pendekezo la serikali tatu lililomo katika rasimu ya katiba mpya na badala yake kutaka muundo wa sasa wa serikali mbili uendelee kwa kufanyiwa maboresho.
Suala hilo, ambalo lipo katika sura ya kwanza na ya sita katika rasimu ya katiba iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, ndilo kiini
kikuu cha mvutano ndani ya Bunge hilo.
Sura hizo ziliibua mvutano mkubwa wakati Bunge hilo lilipoanza awamu ya kwanza kabla ya kuahirishwa, baada ya wabunge wengi kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 kupingana na pendekezo la Tume la muundo wa serikali tatu, huku wajumbe wanaotoka Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 wakitaka rasimu hiyo izingatiwe.
Mvutano huo ndiyo uliosababisha wajumbe wa Ukawa kususia Bunge hilo, wakipinga kuachwa kwa maoni yaliyopendekezwa na Tume hiyo.
Hata hivyo, pamoja na Ukawa kususia Bunge hilo, huku wajumbe wanaounda maoni ya wengi wakiwa wametupilia mbali pendekezo la muundo wa Muungano wa serikali tatu uliomo katika rasimu iliyopendekezwa, suala hilo limeibuka tena katika vikao vya Bunge linaloendelea mjini Dodoma.
ALLY OMARY JUMA
Akiwasilisha maoni ya wachache ya Kamati Namba Mne, Mjumbe wa Kamati hiyo, Ally Omary Juma, alisema mabadilko yaliyofanywa kwenye sura ya saba ni ushahidi tosha kwamba, wajumbe walio wengi kwenye kamati walikuwa na lao jambo kwa kuufutilia mbali muundo uliopendekezwa katika Rasimu ambayo ndiyo inapaswa kuwa msingi wa mjadala.
Alisema kitendo cha kuifanya Tanganyika ndiyo Jamhuri ya Muungano kinaondoa dhana ya Muungano wa hiyari, baina ya Tanganyika na Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kuendelea kuifanya Tanganyika ndiyo serikali ya Muungano kunaiweka Zanzibar mbali na Muungano na kamwe kumfanya Rais wa Zanzibar kama Makamu wa Pili wa Rais siyo kigezo cha kuipa Zanzibar mamlaka kamili katika mambo yasiyo ya Muungano,” alisema.
Kuhusu nafasi ya wakuu wa mikoa, alisema wajumbe walio wengi wamerejesha nafasi hizo katika Katiba ya Muungano, wakati hilo siyo jambo la Muungano na hata utekelezaji wake hautendwi kimuungano.
Alisema licha ya kwamba, jambo hilo siyo la Muungano, maoni ya wananchi yalipendekeza kufanya ukarabati mkubwa wa tawala za mikoa na wilaya.
“Kwa mantiki hiyo, kama yanayoandikwa na kutangazwa katika vyombo vya habari kuhusu majadiliano na mapendekezo ya Kamati ya Bunge Maalumu ili yawe katika katiba inayopendekezwa si sahihi, basi kinachoandikwa Dodoma sasa siyo tena katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali ni katiba ya Tanganyika kwa maana imejaza mambo mengi yasiyo ya Muungano na hivyo, matumizi ya ibara hizo hayatavuka na kutumika Zanzibar,” alisema Juma.
Aliongeza: “Sisi tulio wachache maoni yetu ni maoni ya wananchi katika rasimu, yaheshimiwe na si kuyabadilisha hata tukapoteza umbo la msingi na mantiki ya pendekezo, tunapendekeza kutokuwekwa kwa mambo, ambayo kidesturi ni mambo ya Tanganyika katika Katiba ya Muungano na kwa maana hiyo ibara za rasimu katika sura saba vyote zibaki kama ilivyo kwenye rasimu.”
SAID ARFI
Akiwasilisha maoni ya wachache ya Kamati Namba 10 kuhusiana na sura namba 7,8,14 na nyinginezo mpya juzi, Mjumbe wa Bunge hilo, Said Arfi, aliponda hatua ya wajumbe walio wengi kuachana na pendekezo la tume la muundo wa serikali tatu, akisema muundo wa serikali mbili hauwezi kuondoa kero za Muungano zilizopo.
Alisema mfumo wa serikali mbili umeshindwa kufanya kazi na hautaweza kuondoa kero zilizopo iwapo haitatafutwa suluhu ya kudumu, ambayo ni muundo wa serikali tatu.
“Mfumo wa serikali mbili umeshindwa na hautaweza kuondosha kero. Ni lazima tukubali hivyo na kutafuta suluhu ya kudumu juu ya kero tulizonazo, nayo ni mapendekezo ya serikali tatu kama ilivyoainishwa katika rasimu ya katiba,” alisema Arfi.
Aliongeza: “Hatuwezi kuwa na katiba bora kwa hadaa…hatuwezi kuwa na katiba bora mkiwa wengi, kwa kuwa mko wengi hakuna katiba bora bila maridhiano na muafaka wa kitaifa.”
“Mheshimiwa mwenyekiti, ukweli utabakiwa kuwa ukweli, kwamba mapendekezo yaliomo katika rasimu juu ya muundo wa serikali tatu, ndiyo ufumbuzi wa matatizo tuliyonayo leo…na kutoa haki kwa nchi washirika.”
Arfi, ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), alisema mfumo wa serikali mbili unaopendekezwa na walio wengi ni wa kuahirisha matatizo na si wa kupata ufumbuzi wa matatizo.
“Naomba niwaambie kuwa ufumbuzi wa matatizo ni serikali tatu na wala si vinginevyo,” alisema.Aliongeza: “Hivi ni busara ipi inatamalaki kwa walio wengi kutengeneza katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inatoa haki kadhaa upande mmoja na haitoi haki upande mwingine…kwamba katiba hii tunayoitengeneza itazingatia masuala ya Tanganyika kwa kiwango fulani na itazingatia masuala ya Zanzibar kwa sehemu fulani.”
Aliwataka viongozi kutokuwa na majibu mepesi kwa maswali magumu na kuwataka kutafakari kama Muungano huo upo kinadharia au kivitendo.“Fanya ulinganifu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sura ya Kwanza, Sehemu ya Kwanza, Ibara ya Kwanza…Nanukuu Tanzania ni nchi Moja na ni Jamhuri ya Muungano, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Toleo ya 2010, Sura ya Kwanza, Ibara ya pili, Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…Katiba ya Zanzibar inatamka kwamba Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
“Nchi ya pili ni ipi…nchi ya pili ni lazima turudi sasa katika hati ya Muungano ambayo nchi ya pili ni Tanganyika…kwa nini leo mnakataa Tanganyika isiwepo…ni nani mwenye haki ya kuiondoa Tanganyika wakati mkataba wa makubaliano ya Muungano ulizihusisha nchi mbili ambao Wazanzibari wanatambua hivyo na wameweka hivyo katika Katiba yao.”
Kuhusu kuondolewa kwa baadhi ya sura na ibara, alisema wajumbe wachache wa kamati hiyo, wamepinga kuondolewa kwa baadhi ya sura na ibara katika rasimu ya katiba kwa madai kuwa zinalenga kuongeza mambo, ambayo si ya Muungano.
Sura zilizoondolewa katika rasimu hiyo ni sura ya tatu, tano, saba, tisa, 10, 14 na 15.Alisema hawakubaliani na sura na ibara mpya zote zilizopendekezwa, kwani zinalenga kuongeza mambo, ambayo siyo ya Muungano katika Rasimu ya Katiba.
“Walio wengi walikubali kuingizwa kwa sura mpya kadhaa, na mambo mengine mengi kama vile ardhi, maliasili mazingira, madaraka ya umma…sisi wajumbe wachache hatuzikubali Sura na Ibara mpya zote zilizopendekezwa na kwani zinalenga kuongeza mambo ambayo siyo ya muungano katika Katiba…hivyo basi Rasimu ya Katiba ibaki na Sura zilizopo,” alisema.
Hata hivyo, alisema wajumbe wengi kati ya wachache waliunga mkono kuingiza Sura mpya katika Rasimu lakini walipendekeza katika Sura ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuongeza suala la utatuzi wa migogoro kati ya wafugaji na wakulima na kuanzishwa kwa Tume Huru ya Ardhi ili kuweka Taasisi imara, huru, wazi, zinazowajibika na bobevu za kudumu na kusimamaia ardhi na matumizi yake.
RAIS ZANZIBAR KUWA MAKAMU WA RAIS?
Mapendekezo yanayotaka Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, yaliyowasilishwa bungeni na kamati za Bunge Maalumu la Katiba jana yaliibua mjadala ndani na nje ya Bunge hilo.
Wakati baadhi ya kamati zinataka Rais huyo ashike nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais huku ya makamu wa pili ikishikwa na Waziri Mkuu au Mgombea mwenza, Wachache katika kamati ya Nne jana walisema hata kama hilo likiingizwa kwenye Katiba ijayo, haitamaanisha kuipa Zanzibar mamlaka kamili katika mambo yasiyo ya muungano.
Ally Omar Juma, akisoma mapendekezo ya wachache bungeni jana alisema hatua ya wengi kupendekeza ongezeko la masuala yasiyo ya muungano, kunamaanisha kuivua Tanganyika koti inalodaiwa kuvaa na kuivika kanzu ya muungano.
“Kwa msukumo wa walio wengi, suala la ardhi lipendekezwa kuwekwa katika Rasimu ilhali siyo la muungano, tunapendekeza masuala yasiyo ya muungano yawekewe misingi na siyo maelekezo mahususi katika Rasimu ya Muungano,” alisema Juma.
PROFESA BAREGU
Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, alisema Katiba ikatamka Rais wa Zanzibar ni Makamu wa Rais wa Muungano, itamaanisha haitatokea Rais wa Muungano akatokea visiwani humo au Tanzania kuna wakati itaongozwa na Rais, Makamu wote kutoka Zanzibar.
“Haya mambo tuliyachambua sana, tofauti na wenzetu hatukuchukulia kero za muungano kuwa ni tatizo bali ni dalili na tukabaini tatizo ni mfumo wa muungano, ndiyo maana tuliubadili,” alisema Profesa Baregu.
Alisema mapendekezo hayo yanaashiria kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum, wamechanganywa na kujipa kazi ya kufumua Rasimu ya Pili, yenye uwezo wa kulinda maslahi ya muungano bila kuwa na migongano ya maslahi.
Alitaka ifahamike haikuwa kazi rahisi kuchanganua maoni ya maelfu ya wananchi na kuyaandikia rasimu, ambayo kama ingeboreshwa kwa misingi iliyokusudiwa ingekuwa mzizi wa fitna.
Alitabiri katiba itakayopendekezwa na Bunge hilo kupata upinzani akitoa mfano wa kumpa Rais wa Muungano jukumu la kugawanya mikoa na wilaya Zanzibar, jambo ambalo kwa mujibu wa Katiba yao linatekelezwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi na kulibadili lazima kupiga kura ya maoni visiwani humo.
PROFESA RUTINWA
Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Boneventure Rutinwa, alisema mfumo huo wa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano ulikuwepo na kuondolewa mara baada ya nchi kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.
“Kinachotakiwa ni kutafakari kilichosababisha nafasi hiyo kuondolewa na kwanini sasa inatakiwa kurejeshwa, kwasababu iliaminika kuwa
ikitokea upande mmoja wa muungano ukapata Rais anayetoka chama tofauti
na aliyeshinda kuwa rais wa upande mwingine wa muungano, ingesumbua,” alisema Profesa Rutinwa.
Alisema kwa mtazamo wake, lolote linaweza kutokea kwa sababu ikiangaliwa kwa awamu tatu mfululizo wa chaguzi kuu zilizopita, inabainika vyama vikuu vya siasa kwa upande wa Zanzibar katika kiti cha urais vimekuwa vikitofautiana kwa kura chache.
Alisema hata kama mapendekezo ya kutaka Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano itaafikiwa na kuingizwa kwenye katiba itakayopendekezwa, jukumu la uandishi liachwe kwa wataalamu wa kuandika sheria nchini ili kuepuka makosa ya kiuandishi.
PROFESA MKUMBO
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Kitila Mkumbo, alisema haoni ya kusema Rais wa Zanzibar awe Makamu wa Rais badala yake kama ni lazima jambo hilo kuwa hivyo, katiba ieleze kuwa Rais wa Tanzania akitoka upande mmoja wa muungano, makamu wake atoke upande wa pili.
Awali, taarifa ya wengi katika kamati namba nne ambayo mwenyekiti wake ni Christopher Olesendeka, ilipendekeza kuwepo makamu wa rais wawili; makamu wa kwanza awe mgombea mwenza na wa pili awe Rais wa Zanzibar.
KAMATI NAMBA MOJA
Nayo kamati namba moja katika mapendekezo ya wengi yaliyosomwa na Mwenyekiti wake, Ummy Mwaimu, Rais wa Zanzibar alipendekezwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano awe Makamu wa Pili wa Rais, watakaomsaidia katika mambo yanayohusu Jamhuri ya Muungano.
Pendekezo hilo katika kamati ya kwanza halikupata maoni ya wachache, huku kamati ya nne likiwa miongoni mwa yaliyopingwa na wachache na kusomwa bungeni na Juma.
Imeandikwa na Editha Majura, Abdallah Bawazir na Jacqueline Massano, Dodoma.
SOURCE:
NIPASHE
Post a Comment