Ukraine na Urusi zafanya mazungumzo
Marais wa Urusi na Ukraine
wamekuwa na mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja kuhusu mgogoro wa eneo
la mashariki mwa Ukraine, lakini inaonekana hakuna welekeo wa mgogoro
huo.
Kiongozi wa Ukraine Petro Poroshenko amesema "mpango" utaandaliwa haraka iwezekanavyo kumaliza mapigano kati ya majeshi ya Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga.
Ukraine imekuwa ikiishutumu Urusi kwa kuwapatia silaha waasi, madai ambayo yanakanushwa na Urusi.
Kabla ya mkutano wao wa ana kwa ana katika mji mkuu wa Belaruse, Minsk, viongozi hao wawili pia walishiriki katika mazungumzo na afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton.
Mwanadiplomasia Ashton ameyaelezea mazungumzo yaliyowashirikia viongozi mbalimbali wa Ulaya kuhusu mgogoro wa Ukraine kuwa una mwelekeo"sahihi".
Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani zimeiwekea Urusi vikwazo vya uchumi kwa kushindwa kuwadhibiti waasi.
Zaidi ya watu 2,000 wameuawa katika mapigano kati ya majeshi ya Ukraine na waasi katika majimbo ya Donetsk na Luhansk.
Majimbo hayo mawili yamejitangazia uhuru kutoka Kiev kufuatia hatua ya Urusi ya kujinyakulia eneo la kusini la Crimea kutoka Ukraine mwezi March 2014.
Mazungumzo kati ya Bwana Poroshenko na Bwana Putin yalidumu kwa takriban saa mbili bila kuruhusu vyombo vya habari.
SOURCE: BBC
Post a Comment