FAHAMU UTAMADUNI WA WAZARAMO
Mji wa Dar es Salaam hapo awali ulijulikana kama
MZIZIMA wala hapakupata kuwapo na habari zenye ukamilifu juu ya chanzo
cha jina hilo, bali kuna mapokeo mbalimbali yenye kueleza tu chanzo
chake.
Mathalani, yapo mapokeo yanayoelezea kuwa katika
mwaka 1866 Sayid Majid (Mwarabu) Mtawala na mfanyabiashara tajiri toka
Oman inasemakana uliujenga mji wa Dar es Salaam kwa kiasi Fulani na
hasa Bandari ili kumrahisishia upakuaji na upakiaji wa bidhaa zake
mbalimbali ziingiazo na zitokazo kwa njia ya baharini.
Kutokana na hali nzuri sana ya utulivu na usalama
wa bandari walivyoiona wakati wakishughulikia mizigo yao,
wakaamua kuita Bandari hiyo kuwa ni ya salama. Jina hili
lilizoeleka mno hatimaye likawa ndio chanzo cha mji wote kuitwa
Bandari ya salama na baadae ikawa Dar es Salaam kama
ijulikanavyo hadi hivi sasa.
Mapokeo mengine juu ya jina Dar es Salaam ni
kwamba, inasemakana kuwa walikuja Mzizima wahindi wawili wafanya
biashara enzi hizo mmoja akiitwa Butu na mwingine Salama. Wahindi
hao walijenga nyumba mbili kubwa, kila mmoja na yake. Nyumba hizo za
biashara ziliitwa mabanda. Wakulima kutoka shamba walikuja Mzizima
kuuza na kununua bidhaa mbalimbali kwa wahindi hao.
Katika hali isiyoeleweka wakulima hao walivutiwa
mno kufanya biashara ya kuuza ama kununua kwenye banda la
Salama kuliko Banda la Butu.
Hivyo basi wakulima hao walipokuwa wakikutana
njiani walipoulizana kama walinunua ama kuuza wapi bidhaa zao, jibu mara
nyingi lilikua Banda la Salama ama kama ilivyozoeleka hivi
sasa Dar es Salaam. Kuna mapokeo mengine juu ya
kupatikana kwa jina la Dar es Salaam kama ifuatavyo.
Inasemekana kuwa Wazungu walipotaka kuingia nchini
Tanganyika (Tanzania) Waarabu ambao walitangulia kuja humu nchini kabla
yao yalizuka mapigano makubwa kati yao hususan wajerumani na Waarabu,
enzi hizo mtawala mzalendo alikuwa Mwinyimkuu Mshindo,
mapigano hayo yalipofika mzizima ikapatikana suluhu kupitia
mazungumzo, mapigano yakaisha. Hivyo sehemu hii ya mzizima
ikapata jina la Bandari ya Salama kutokana na amani iliyopatikana
wakati huo. Kwa hivyo jina la mzizima likabadilika badala yake
pakaitwa
Banda la salama
Bandari salama
Bandari ya salama
Na hatimaye pakaitwa D’Salaam, Jina litumikalo hadi hivi sasa.
Wakati huo huo Bwana Hatimi Mfanya Biashara ya
Chumvi Mwarabu alifika kwenye mwambao huo akaleta chumvi na akaoa
mjakazi, binti wa Kishirazi na akabahatika kupata mtoto mmoja wa kiume.
Kwa kuwa Bw. Hatimi ndiye aliyeleta chumvi basi
mtoto huyo akaitwa chomvi (chumvi) na baadae jina la chomvi
likabadilika na kuwa shomvi, na kizazi chake kikaitwa Wamashomvi.
Inasemekana kuwa Wamashomvi ni mchanganyiko wa Waarabu na wenyeji wa pwani ya Dar es Salaam.
NB:
Kutokana na maelezo ya Bwana B.A. Kando ya juu ya
upatikanaji wa chumvi bila shaka kuna tofauti ya ugunduzi wa chumvi na
uchuuzi wa chumvi kama ilivyokuwa kwa Bwana Hatimi. Yeye hatimi
alikua mchuuzi wa chumvi, lakini siye aliyegundua chumvi.
SULTAN SEYYID MAJID NA WAJERUMANI.
Sayyid majid hapo mwanzoni aliogopa sana utawala wa Pazi. Wazalendo aliowakuta akitokea kwao Oman Uarabuni.
Kwa sababu ya kutafuta mali kwa ajili ya maisha,
Sultani majid alilazimika kuhamia Mzizima kunako Mwaka 1862 na
Mwaka 1865 alianza kuujenga mji wa Dar es Salaam kwa kiasi Fulani.
Lakini, mnamo mwaka 1885 Wajerumani waliingia
Mzizima na katika mwaka 1886 walianzisha utawala wao. Wajerumani
waliweza kuitawala Tanganyika walipomtumia mtu wao mjanja mjerumani Karl
Peters ambae mnamo 1885 alifanikiwa kufanya mikataba ya kitapeli kwa
kuwahadaa Machifu wazalendo hapa nchini. Chifu Mangungu ni mmojawapo
aliyetiliana mkataba na Karl Peters. Hatimaye kuanzisha dola yao mnamo
mwaka 1885. Katika mwaka huo huo Wajerumani waliweka mpaka ya nchi
Tanganyika ili waweze kuendesha dola yao bila hofu ya kuingiliwa na
mataifa mageni mipaka hiyo inatambulika kimataifa hadi hivi sasa.
Mwaka 1893, Wajerumani wakiunganisha na msaada wa
mfanyabiashara Mwarabu tajiri wa Bagamoyo Sheikh Sewa Bin Hadji
walijenga Hospitali kubwa ya kulaza wagonjwa pale palipokuwa
pakijulikana kama Malindi, eneo la Bandari ambalo karibu na kituo cha
kati cha Polisi (Central Polisi Stn). Sewa Hadji alichangia Rupees
12,400 ambazo kwa wakati huo zilikuwa pesa nyingi sana.
Mwaka 1894 Wajerumani walianza kujenga Reli ya
kati (Central line). Na katika mwaka 1914 Wajerumani walijenga soko la
Kariakoo.
Lengo na madhumuni ya ujenzi huo hasa ilikuwa
kuadhimisha kutawazwa kwa mfalme wao Kaiser Wilhem huko
Ujerumani . Lengo hilo hata hivyo halikutimia, kwani mwaka huo huo
vita kuu ya kwanza ya dunia ilianza na kuvuruga mpango
mzima.
Vita hii huku kwetu ilikua kati ya Waingereza na
Wajerumani na hata Wazalendo walihusishwa kwa namna moja ama
nyingine. Waliposhindwa Wajerumani, Waingereza
walichukua hatamu ya uongozi wananchi hii kunako mwaka
1921.
Jengo hilo la soko likatumika kama kambi ya Jeshi
ya kuwekea vifaa vyao vya vita. Kwa Kiingereza waliita “Carrier Crops”
Waswahili katika kukosea matamshi waliita” Kariakoo” Jina maarufu
ambalo linatumika hadi hivi sasa.
Kama ilivyokuwa kwa Wajerumani, Waingereza nao
walianza na Ujenzi wa shule ya Uhuru wavulana Mwaka 1921. Enzi hizo
ilijulikana kama Kichwele Boys Middle School. Na mwaka 1935 wakajenga
shule ya Uhuru Girls Middle School. Wakati huo ilijulikana kama
Kichwele Girls Middle School. Na kunako Mwaka 1939 walijenga shule
ya Mchikichini Primary School.
Mwaka 1949 ilianzishwa Kampuni ya usafiri Dar es
Salaam iliyoitwa kwa kifupi DMT ama Dar es Salaam Motor Transport.
Kampuni hiyo ilibadilishwa jina baada ya uhuru wa Tanganyika na kuwa
shirika la usafiri la Taifa na kuligawa sehemu mbili (UDA/KAMATA).
UDA – Usafi Dar es Salaam na KAMATA – Kampuni ya
Mabasi Tanzania ambapo Kampuni hiyo ya mabasi hayo
yalibuniwa ili kusafiri mbali, Bara na nje ya Tanzania, kama vile Kenya
Mombasa na Nairobi, Kampala Uganda, Ndola Zambia na kadhalika. Mpango
huu ulianzishwa rasmi mnamo mwezi Julay 1969 uamuzi wa
kuunda Kampuni hizi za usafiri Dar es Salaam na bara ulianza
kutokana na ongezeko la haraka la idadi ya wakazi wa Dar es Salaam
hasa, na ingawa nchi nzima ya Tanzania idadi ya watu ilikuwa
ikiongezeka kwa kasi kila uchao lakini toka hapo mwanzo ilionekana kuwa
Dar es Salaam ndio mji ambao watu wake wanaongezeka kwa kasi zaidi
kuliko maeneo mengine ya nchi.
Mr. L. W. Swants, Mwandishi mmoja kati ya vile vitabu vinne alivyozungumzia
mwandishi wa simulizi hii. Katika kitabu chake The Zaramo of Dar es
Salaam, amesimulia jinsi ya kuongezeka kwa wakazi wa Dar es
Salaam kuanzia Mwaka 1957. Bw. Swants ameainisha kuwa pamoja na
wakazi wengine kufikia mwaka huo Wazaramo pekee walikuwa 33, 960 Dar es
Salaam. Idadi hiyo ilikuwa ni asilimia 18.5% ya wakazi
wote wa Dar es Salaam kwa wakati huo. Na baada ya hesabu za sensa
katika mwaka huo idadi ya wakazi wote wa Dar es Salaam walikuwa 183,260.
MUHIMBILI HOSPITAL
Itakumbukwa kuwa , hapo
nyuma kidogo kabla ya kujengwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.
Hospitali kubwa ambayo ilifananishwa na Muhimbili ni Sewa Hadji
Hospitali. Hospitali hii ilijengwa wakati wa utawala wa Wajerumani
kama tulivyokwisha eleza hapo nyuma.
Hospitali ya Sewa Hadji
ilikuwa pale Malindi karibu na Central Polisi Station eneo ambalo hivi
sasa linatumika na Bandari baada ya Jengo hilo kubomolewa kwa upanuzi
wa Bandari hiyo.
Wajerumani vile vile katika
Mwaka 1897 walilifungua rasmi jengo jingine la Hospitali ijulikanayo
hadi hivi leo The Ocean Road European Hospital. Hospital
ambayo kwa hivi sasa inatumika maalum kwa magonjwa ya Saratani.
Waingereza walipokaribia
kutoa uhuru wa Tanganyika walijitahidi katika kujenga baadhi ya majengo
kama vile walivyojenga majengo ya Hospital ya Muhimbili. Hapo zamani
Muhimbili palikuwepo na mabanda madogo tu eneo la sasa ilipo
University of Dar es Salaam Facult of Medicine ambayo yalikuwa
yanajulikana kama Muhimbili Hospitali na matumizi yake ilikuwa utibabu
hasa wa kina mama wazazi wajawazito na huduma nyinginezo ndogondogo.
Hapakuwa pakilazwa wagonjwa
kama hivi sasa. Waingereza kwa hivyo wakajenga
Hospital kubwa ya kulaza wagonjwa walipomaliza kuijenga Hospital hiyo
kwa fedha zao Princess Magret mdogo
wa Malkia Elizabeth II alikuja kufungua rasmi mnamo Mwaka 1957
alipokuwa ziarani Tanganyika. Jengo hilo likaitwa Princes
Margreth Hospitali kwa heshima yake. Princess Magreth ameshafariki
hivi sasa.
Jina la Sewa Hadji lilipendekezwa kuwepo pale
Muhimbili kwa madhumuni ya kumuenzi mfadhili huyo.Kwani
ilipobomolewa Hospitali ya Sewa Hajji kule karibu na
kituo cha kati cha Polisi, enzi zile palijulikana kama Malindi
hapakuwahi kuwepo jina la Sewa Hadji popote Tanganyika bila shaka
wakubwa waliona haingekuwa ni uungwana kumsahau mtu aliyejitolea
kuwahami wananchi wengi wa Tanganyika siku hizo bila ya kuwepo
kumbukumbu yake ndipo jina lake likaingizwa katika mashujaa wetu. Na
bila shaka Mashujaa wetu wazalendo Kibasila na Mwaisela habari zao
zinaeleweka vyema katika Historia ya nchi yetu ya Tanzania.
UTAMADUNI WA WAZARAMO (LUGHA)
Bila shaka kila kabila duniani lina utamaduni wake na
lugha yao ya asili ya mawasiliano. Wazaramo halikadhalika wanautamaduni
wao na lugha yao ya asili ya mawasiliano. Lugha yao ya kizaramo ni
maarufu na ni moja kati ya lugha za zamani sana katika jamii ya
Watanzania . Wazaramo baadhi yao hasa wazee wale wa vijijini ni
mahiri sana wa kuongea lugha yao hadi hivi sasa kinyume na wale
wazaramo waishio mijini hususani Dar es Salaam. Wengi wao hawawezi
kuongea lugha hiyo kwa ufasaha, napengine si ajabu kutoifahamu kabisa.
Athari ambayo huenda imeanzia toka kuzaliwa kwao. Hii imetokana na
wazee wenyewe kutowafundisha vizazi vyao, tokea udogoni. Kutokana na
taathira hiyo basi lugha ya kizaramo imekuwa ikipoteza umaarufu wake
kadri ya miaka inavyosonga mbele.
Lawama , hii kwa hivyo moja kwa moja inabebwa na
wazee wenyewe kwa kutokuwa makini kwa kutoitilia lugha yao mkazo toka
zamani katika kuiongea mara kwa mara ili na vijana wao wapate kuiga,
kwa hivyo basi polepole lugha hiyo ikaanza kusahaulika hususan kwa wale
waishio mijini hasa na hivyo basi hatimaye hata huko vijijini pia.
Pamoja na kwamba bado kuna baadhi ya Wazaramo ambao
wanaongea lugha yao hiyo lakini hawaongei kwa ufasaha na wala si
wazungumzaji wanaoipa umuhimu wa kutosha.
Kwa kuwa si Wazaramo wengi wanaoiongea lugha hii
hivi sasa hata huko vijijini dalili za kutoweka kabisa ni dhahiri katika
muda si mrefu sana ujao, iwapo kama hatua za dhati kuinusuru
hazitachukuliwa haraka.
Kumbukumbu zetu zinaonesha kuwa lugha ya Kizaramo
katika ukoo wetu wa Seseme, imeachwa kabisa kuzungumzwa toka wakati ule
wa Mababu na Mabibi zetu kina mzee Hussein Hussein
Seseme takriban sasa miaka mia na hamsini
iliyopita hivi. Mzee Hussein na nduguze wawili mzee Omar na Mzee Abdalah
hawakuwa na mazoea ya kuzungumza lugha ya kizaramo waziwazi badala
yake waliipa kipa umbele lugha ya Kiswahili, lugha ambayo
wameichukulia kama lugha yao mama. Hapakuwepo na mkazo kabisa katika
kuzungumza kizaramo matokeo yake vizazi vyote katika ukoo huu wa Seseme
hatuna taalum ya lugha hii.
Lakini janga hili la kutokomea kwa lugha ya
kizaramo halikuanzishwa na ukoo wa Seseme tu
bali ni kosa lililotendeka na jamii
NGOMA ZA HARUSI NA SHEREHE ZINGINEZO.
Inasemekana kuwa Wazaramo walikuwa na mkusanyiko
mkubwa mno wa ngoma za asili hata yawezekana kuwa ni moja kati
ya makabila yenye ngoma nyingi mno katika Tanzania ingawa
nyingi sasa zimeanza kutoweka. Ngoma hizo hasa huchezwa nyakati za
sherehe mbalimbali kama vile kwenye harusi unyago, mkole kwa mabinti
wanawari, suna ama jando kwa wavulana ambapo mangariba hucheza ngoma ya
msewe na sherehe zingine kadhalika katika kutekeleza kazi yao.
Ngoma za Wazaramo baadhi y ake zina mgawanyiko wa
tofauti ya watu umri na jinsia. Vijana wadogo huwa na aina yao ya
ngoma, watu wa makamo pia huwa na namna yao. Hali kadhalika wazee wake
kwa waume kila mmoja huchezwa kivyake. Lakini kuna vile vile ngoma za
mjumwiko wa jinsia zote na umri wowote, hizo ndizo nyingi mno na ndio
hizo furaha za Wazaramo na ngoma zao hizo za asili Ngoma mathalani mkole
na msondo ni ngoma zinazowahusu kina mama na kina dada vijana na
kadhalika.
Ngoma hizo kwa kuzitaja majina yake ambazo nyingi mno ni, Mdundiko, Msondo, Vanga ama Mkinda, Mkwaju Ngoma, Matarumbeta ama Beni bati Mnanda ama Mchiriku, Mganda, Buti na kadhalika.
Na hapo siku za nyuma kidogo palikuwepo na ngoma
ambazo hivi sasa husikika kwa nadra sana ama hazipo tena, kutokana na
kupoteza kabisa umaarufu wake, ngoma ya Tokomile kwa mfano ilipoteza
umaarufu wake kutokana na kufutwa kwa uhasama wa kijadi wa ngoma hiyo
ambapo Mbango na Mizia mahasimu wakubwa walisababisha mapigano
yasiyo na faida yoyote zaidi ya kumwaga damu bure tu kwa wananchi ambapo
kinyume chake walikuwa wajenge umoja ili kuundoa ukoloni wa Mwingereza
enzi zile kabla ya uhuru badala ya kuwa mbwa na chatu .
Mwalimu Nyerere wakati ule akiwa Mwenyekiti wa TANU
chama kilichodai Uhuru wa nchi hii Tanganyika, rai yake kwa wananchi
kuwa ngoma hiyo ichezwa bila ya silaha ili kuepusha mapigano na
kumwaga damu kwa kuwataka Mbago na Mizia mahasimu hao wa jadi wapatane
ili wawe kitu kimoja jambo ambalo lilionekana kama gumu sana hapo
mwanzo lakini iliwezekana baadae uhasama ukamalizika na hatimaye
ngoma yenyewe kufa kabisa. Siku hizi si rahisi kuisikia ngoma ya
Takomile.
Kwa hakika ngoma ya Tokomile haikuwa ngoma ya amani,
kama ilivyo desturi ya ngoma nyingi, kwani watu badala ya kufurahi
walifanyiana uadui, ingawa Wazaramo wenyewe waliita ngoma ya mashujaa,
hasa kutokana na yale mapigano baina ya pande mbili Mbango na Mizia
lakini sababu hii haikuwa ya msingi hata kidogo.
Visa vingi viliwahi kutokea enzi hizo vya umwagaji
wa damu na mara nyingine hata kusababisha vifo, kwa hivyo badala ya
furaha ikawa ni misiba na vilio, jambo ambalo halikuwa na maana yoyote.
Ngoma ya Tokomile kwa makusudi kabisa wahusika
walianzisha vurumai wakapigana ati kuonesha nani mbabe zaidi kati yao,
hilo tu basi. Wala hapakuwepo na lolote la maana. Mwisho wa yote
wakajikuta katika hasara kubwa. Ngoma zingine zilikufa kifo cha
kawaida. Ngoma kama vile Ndalandala Mtondoo Lelemama Kasangwa,
Ndekule. Sikinde na kadhalika. Ngoma hizo zilipata kuchezwa zama hizo
za wazee wetu, Mababu na Mabibi, Vijana wa kizazi cha sasa si wengi
walioweza kubahatika kuzishuhudia ngoma hizo zikirindima. Hivi sasa
ngoma hizi imebakia hadithi tu kusimuliwa hamna la zaidi.
Kuna baadhi ya wanamuziki wa sasa wameziingiza baadhi
ya ngoma hizo katika Bendi zao za dansi kama mtindo wao, kwa maana ya
ubunifu katika kuboresha miziki yao .
Ngoma ya kina mama ya msondo kwa mfano. OTTU JAZZ
imeungiza kama mtindo wao. Sikinde imeingizwa katika Band ya Mlimani
Park na hata Ndekule iliwahi kuingizwa kwenye Safari Sound Band ya Huggo
Kissima Mfanya biashara maarufu Dar es Salaam Band hiyo hivi sasa
haipo tena. Hata hivyo uasilishaji huu wa mitindo ya ngoma hizo za
Wazaramo katika miziki ya dansi hazikuweza kuzirudisha tena ulingoni
bali ni kumbukumbu tu iliyobaki ngoma hizo kuwa zilikuwepo. Kulikuwepo
pia vanga vanga Band ya Polisi Jazz zote hizo ni Ngoma za Kizaramo,
ambazo Band za Music zilizitumia kama kitambulisho chao
NGOMA ZA MASHETANI NA TAMBIKO.
Ukiachana na ngoma za sherehe mbalimbali ambazo kwa
kawaida ni za furaha, kuna ngoma zingine ni maalum kwa uganga. Ngoma
hizo wateja hupunga mashetani, ni ngoma za tiba kwa wenye kupagawa na
Pepo wabaya ama hupata maradhi yanayohusisha mashetani ambao
inaaminika kuwa pepo hao huleta madhara kwa watu, kuumwa hata pengine
kufa kama ukipambana na madudu hayo. Sasa , ili kumponya muathirika
basi hupungwa mashetani kwa ngoma ya madogoli, pepo hao maarufu sana ni
kinyamkera na mwanambago inaaminika kuwa ni lazima watolewe kutoka mwili
wa mteja. Mteja ni Yule aliyepatwa na mashetani hao, hivyo mganga wa
mashetani hulazimika kupigisha ngoma ya madogoli ili kumnusuru mgonjwa
wake (Mteja)
Kwa upande mwingine kuna tambiko za jadi. Kwa
kizazi hiki cha sasa, si rahisi sana kuelewa ama hata kukubaliana na
mawazo ya wazee wa zamani hususani juu ya tambiko za jadi. Wazee wa
zamani walisisitiza mno juu ya kufanya tambiko hizo za mizimu ya
wahenga ambayo wanasema isipokumbukwa basi huenda ikaleta madhara
makubwa kwenye ukoo mzima kama vile maradhi na hata vifo. Tambiko huwa
kinga kwa husuda na kadhalika. Wazee waliamini hivyo.
Katika ukoo wa Seseme kwa mfano kuna tambiko la jadi
linajulikana kwa jina la “GOMBO” Bado kuna kumbukumbu ya mzee mmoja
mganga mahiri sana katika tambiko hii.
Akijulikana katika ukoo maarufu kwa jina la mzee
“MCHAFU” Hata hivyo walikuwepo akina mzee Mchafu wengine wengi
walioifahamu vyema “GOMBO” ala za ngoma hii ya Tambiko ni ungo wa
kupetea nafaka, pamoja na udananda aina ya upinde mdogo ambao huwambwa
kwenye ungo huo. na kisha mzee Mchafu ama mganga mwingine huvuta
kamba ya upinde huo kama ilivyo namna ya udananda wa mwari wa kike
afanyavyo ama mtu apigae gitaa upinde huo hutoa sauti ya kama mnyama
Fulani aliyae kwa sauti ya chini chini ama sauti hiyo inaweza
kufananishwa na gitaa la besi la Band hizi za sasa, lakini Gombo hutoa
mlio mdogo zaidi wa chini chini.
Kwa hivyo washiriki wanaukoo wote hujumuika katika
kucheza kwa kuzunguka zunguka wale wapigaji wa hiyo ngoma na kuimba
kwa sauti kufuatisha maneno ya mganga aimbavyo.
Aghalabu nyimbo zenyewe hazipendezi masikioni mwa
watu Tambiko hili huanza usiku kwani huwa za matusi makubwa bila kujali
mjumuiko wenyewe umehusisha watu mnaostahiyana kiuzawa,
kinachozingatiwa tu kwenye mkusanyiko huo ambao huwepo Baba, Mama, Babu,
Bibi, Mjomba, Shangazi, Watoto, Wajukuu vilembwe na kadhalika ni ile
miiko yao inayoruhusu kufanya hivyo ilimradi uganga utimie tu,
wanavyoamini, hakuna tusi lolote litamkwalo litakalochukuliwa kama ni
uvunjifu wa adabu, lau kama mtu atatukuna mbele ya mamaye ama babayake
mzazi ama mzee yoyote ilimradi tu yupo katika tambiko hiyo basi yeye
ni ruksa tu. Na hiyo ndiyo hasa maana ya “GOMBO”
Kwa hakika nachelea mno iwapo kamaTambiko la sampuli
hii linawezekana kufanyika tena kwa uwepesi sana katika nyakati zetu
hizi zenye nidhamu bora ya kidini, hususani dini yetu hii ya Kiislam,
kama ilivyokuwa hapo zamani.
Kwa mujibu wa mafunzo ya dini ya Kiislamu ni
kwamba Uislam haushirikishwi kwa vyovyote vile na mashetani, kwani
mambo ya kishetani tayari yamelaaniwa kwenye Quraan Tukufu hivyo basi
hayakubaliki Abadan.
Kwa asilimia kubwa sana Gombo linahusisha ushetani na si ajabu hata ushirikina pia umo. Hivyo tahadhari inalazimika sana.
Nyimbo ziimbwazo katika Gombo ni za matusi ya
nguoni, lakini hakuna mwiko katika kuimba matusi hayo, hata kama
utaimba mbele za watu mnaostahiliana kinasaba.
Gombolillaga x 2 kolila naumoyo Gombo kolilla naumoyo” x 2
Waganga huimbisha hivyo na wanandugu hulazimika
kuitikia kwa kufuatisha maneno hayo kwa sauti kubwa ya kuhinikiza huku
ngoma ya Gombo ikirindima.
Wengi katika sisi wanandugu, wajukuu wa akina mzee
Makumbitu tukiwa tumechanganyika na wazee wetu, Baba zetu mama zetu
shangazi zetu na kadhalika tumekuwa ni watu wa kufuata amri tu kutoka
kwa wazee hao, lakini hatukupewa nafasi hata chembe kuhoji jambo lolote
lile juu ya utamaduni huo wa Gombo, kwani kufanya hivyo ni kutaka
kujua kile kinachoendlea katika tambiko hilo linalochukuliwa na wadau
kama ni kuwakosea adabu wazee. Bila shaka jambo likishafikia hatua
kama hiyo basi huwa halina sululu tena, bali ni kuacha tu amri ya wazee
ichukue mkondo wake, na hivyo basi ndivyo ilivyokuwa.
Ngoma hii watu hukesha wakicheza na kuimba usiku
kucha wakiwazunguuka zunguuka wale waganga walioketi katikakati yao,
mithili ya mchezo wa kitoto wa Foriti.
Hakuna staili maalum ya uchezaji ngoma hiyo, ila
wewe cheza tu vile uwezavyo na tamka matusi uyajuayo wala usiogope
jambo lolote kwani hakuna mtu atakayekukosoa atakayesema kuwa wewe huna
nidhamu. Kwani hivi ndivyo hasa Tambiko ya Gombo litakiwavyo. Tusi
huwa si tusi katika Gombo bali huwa kinga kubwa dhidi ya maadui wetu
kwa mujibu wa wazee wetu walivyoamini. Tambiko la ukoo wa Seseme”
Ifikapo Alfajiri wakati adhana inaposikika swala ya
Kiislam huwa ndio kikomo cha Tambiko. Nyimbo za mwisho mwisho kumalizia
shughuli nzima ya Tambiko, wanganga husikika wakiimbia:
“Sanze Mnumanunma, Sanze Mnumanuma, Kupitita bahano kadimanula manu, Sanze mnumanuma x 2”
Wimbo huo hurudiwa tena na tena, wanandugu hufikia na hatimaye mwimbo humalizika kuashiria kwisha kwa Tambiko.
Mganga Mkuu huamrisha wanandugu waliopo kwenye Gombo
wakusanyike chini ya mti mkubwa ambao Gombo hufanyika, na kuamuru kila
mtu kumega tonge moja la ugali uliopoa, ugali wenyewe huwa aidha wa
ulezi au mtama lakini si wa mahindi. Pia kunyofaoa kipande cha nyama
ya kuku wa kubanika wa dawa aliyepoa na kumeza mchangayiko bila kunywa
maji wala kutafuna mfupa.
Kawaida miti iliyopendekezwa hasa kwa tambiko ni Mbuyu Mvule Mwembe na kadhalika.
Mifupa ya kuku, manyoya na utumbo hufukiwa pale chini ya mti pamoja na chungu kile kilichopikiwa ule ugali.
Wakati wa kuchimbia na kufukia chungu hicho cha dawa mganga mkuu huomba kwa niaba ya wanadungu mambo ya manusura katika Afya na kipato katika mwaka mzima husika maombi hayo hupitishwa kwenye mti ule.
Baada ya hapo mganga mkuu hutoa ruhusa ya wanandugu kurudi majumbani mwao hadi mwaka mwingine kwa ajili ya tambiko jingine.
Masharti ya Gombo ni kwamba nyimbo zile za Tambiko za
Matusi ni lazima ziimbwe tena kwa sauti kubwa ili walio mbali waweze
kusikia vyema nini kinachoimbwa.
Tena ziimbwe nyimbo hizo bila kuona haya wala kuweka
staha kwa wazee mliojumuika nao, na bila ya kujali aina gani ya matusi
yaimbwayo.
Wazee wetu waliamini ya kuwa gombo ni lazima katika
ukoo huu wa Seseme, pamoja na kwamba hapakuwepo na maelezo yoyote ya
kisayansi waliyoyaacha wazee hao juu ya umuhimu na ukweli hasa wa
jambo hilo wanaloliamini kupita kiasi.
Jambo la ajabu kuhusu wazee wetu ni kwamba pamoja na
wao huwa waumini wa dini ya Kiislam, dini ambayo inakemea vikali sana
ushetani, lakini wao waling’ang’ania utamaduni wao huo walioachiwa na
wazee wao, wa Tambiko la Gombo. Waliamini kuwa Gombo ni kinga kubwa
sana katika ukoo.
Jambo hili kwa sasa linamvutano mkubwa sana baina ya Wazee na vijana, kuhusiana na Tambiko hilo la Gombo.
Sikuhizi Gombo hutekelezwa kwa shinikizo la wale wenye umri mkubwa kwa kuwapa maelekezo wadogo kama amri tu.
Lakini hapana shaka kuwa wakubwa hao katika ukoo nao
ni waathirika wa mawazo ya wazee wao, Babu zetu. Kwa mantiki hii bila
shaka Gombo sasa linaelekea kwenye hatima yake.
MARUHANI
Maruhani ni aina nyingine mojawapo ya mashetani,
lakini husemekana kuwa ni mashetani wema kwa Binadamu. Kwani hufanya
kazi ya tiba za maradhi mbalimbali badala ya kuwadhuru.
Wazee waliyatilia maanani sana Maruhani . Inasemekana kwamba yanaweza hata kuagua uchawi kwa mtu aliyerogwa.
Kwa kawaida huwepo waganga wanaotumia hawa maruhani katika ukoo.
Kwamba mtu aliyerogwa, shetani wa maruhani huwa na uwezo wa kugundua maradhi na mchawi aliyemroga mtu huyo.
Hivyo basi mganga wa maruahani huitwa kuja kumuagua mteja aliyerogwa .
Maruhani kwa jumla huwepo takribani katika kila
ukoo hususan enzi hizo. Madhumuni hasa ya kuwepo hao maruhani ni kutibu
inapotokea mtu kurogwa na kadhalika.
Hata hivyo kwa kusema hivyo sina maana ya kuwa
Wazaramo walipendelea majini na uchawi la hasha bali hii ni kujulisha
tu kwamba Wazaramo kama walivyo binadamu wengine wanafikwa na mambo
mengi ya kidunia kama ilivyo kwa watu wengine wote hapa ulimwenguni.
UTANI KATIKA UZARAMO.
Kuna baadhi ya watu walikuwa wanawachanganya
Wasukuma kama vile Wanyamwezi kwamba na wao pia ni watani wa wazaramo
lakini kwa uhakika Wasukuma si watani wa Wazaramo ila tu kwa vile
wasukuma na Wanyamwezi wanafanana mno katika mambo yao mengi hivyo
basi moja kwa moja nao wamekuwa watani wa wazaramo.
Katika kutafiti ili kujua utani huo wa makabila haya
ulianza vipi kwa kweli jibu lake halikupatikana bila shaka wazee wa
zamani wanaweza kupata ukweli ulivyokuwa. Vile vile ndani ya Wazaramo
wamo watani wanaotaniana wenyewe kwa wenyewe kwa mfano wanzala ni
watani wa wavilindi na kadhalika.
Kuna utani pia kati ya Babu ama bibi na wajukuu
zao. Utani kati ya mtoto wa mjomba na shangazi. Muhile kwa muhile na
kadhalika.
Kwa mfano kuna utani wa mjukuu wa kiume na Babu na
Bibi yake ulioandikwa na mtunzi mmoja BW. M. R. KIZARA katika kitabu
chake UTANI wa TANZANIA (1975) Tunanukuu.
Mjukuu - Babu lelo nokwiza ikilo kuwasa na mtwanzi wako,
minyusile vinhugwe kwisha tena - “Zua diswa”
Babu: - Ikimbigalo kunacho mina cha kuwasa na
mtwanzi wangu.
Mjukuu: - Nielekelelo ulole
Babu: Segela hano govijo
Mjukuu: - Mbona koninga kodomba choni, nielekele ulole
Bibi: - Ikimbigalo kunacho avo cha kuwasa na nie?
Mjukuu: - Kama na bule mbona babu koninga kodumba msiwase
nangwe, leka aniluhusu ulole
Japo kuwa utani huu, unahisia kali sana, za ndani
kihalisia, bado ulikua unakubalika katika jamii ya Kizaramo pasipo
lawama zozote. Sina hakika sana kama hadi sasa utani kama huo
unawezekana ukavumilika hata hivyo.
Bwana KIZARA ambaye amewahi kutembelea sehemu
nyingi waanakoishi Wazaramo kama vile Msanga, Sungwi, Masaki na
kadhalika, ametubainishia kuwa Wazaramo hawana watani wengi kama
ilivyokuwa baadhi ya makabila mengine Tanzania
Bwana Kizara ameongeza kusema kuwa Wazaramo ni kabila
tulivu mno ambalo halikupenda mapigano na jirani zao katika zama hizo
na hata hivi sasa.
Ndugu wa Wazaramo hasa toka hapo asili ni Wakutu,
Wadoe, Waluguru, Wakwele kwa vile wote hawa wanatokana na ukoo wa Pazi
Kilama Lukali. Wazaramo toka enzi hizo walikuwa ni watu wapendao
ushirikiano, urafiki, utani hasa kwa watani wao. Kwa jumla ni watu
waliopendelea sana amani, hawakuwa wachokozi kwa hivyo hawakupenda
kabisa vita kama ilivyo kwa baadhi ya makabila mengine Tanzania.
POSA ZA JADI ZA WAZARAMO.
Kwa kuwa tumepitia katika maeneo mengi mno kuhusu
maisha ya Wazaramo na Tamaduni zao tumeona ni vyema pia tukaingiza jambo
hili muhimu sana katika maisha ya binadamu duniani, jambo lenyewe si
jingine bali ni “ndoa”.
Katika siku za nyuma kidogo mnamo Mwaka 1920 na
kurudi nyuma masharti ya ndoa ya Kizaramo yafuatayo hapa chini ilikuwa
ni lazima yafuaatwe iwapo wanandoa wawili inapofikia wakati wa
kuhalalishwa kuoana vinginevyo ni vigumu mume kupata mke kwa namna
yoyote ile, mambo yenyewe ni :-
Mahari
Mkaja
Kilemba
Behobeho
Kanyaga lubuga
Kisamula ndevu
Kilomo kinona
Mama Ngwaya
Kakulongela nani hano kama kuna Mtwanzi na kadhalika.
Baada ya Msululu wote huo kutimizwa ambayo tafsiri
yake ni pesa ndipo ridhaa ya wazee kutolewa kwa binti yao kuolewa
na muhusika.
SOURCE: SESEME FAMILY
Post a Comment